Bukobawadau

TAARIFA YA JULIUS MTATIRO KUHUSU VURUGU ZA WANACHAMA CUF

MUNGIKI WA LIPUMBA WAVAMIA “PRESS” YA CUF, WAPIGA WAANDISHI WA HABARI NA VIONGOZI, MUNGIKI MMOJA AJERUHIWA NA WANANCHI WENYE HASIRA KALI!
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
(Imetolewa na Julius Mtatiro, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi, The Civic United Front - CUF) 22 April 2017.
Ndugu zangu, Leo, Jumamosi, 22 Aprili 2017, Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Juma Mkumbi (ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa) alikuwa anazungumza na vyombo vya habari katika Hotel ya VINA iliyoko Kata ya Mabibo, wilaya ya Kinondoni (jijini Dar Es Salaam), juu ya masuala mbalimbali yanayohusu wilaya yake.
Akiwa anaelekea kumaliza mazungumzo na wanahabari, ghafla, watu waliovalia KININJA/VINYAGO walipaki magari mawili karibu na hoteli na kuvamia ukumbi wa PRESS ya Mhe. Juma Mkumbi.
Wavamizi hao maarufu kama MUNGIKI, (ambao hutumwa na Prof. Lipumba) leo wakiwa na BASTOLA MOJA na MAPANGA walianza kuwapiga viongozi wa CUF akiwemo Juma Mkumbi na kuwasababishia majeraha kadhaa.
Watu waliopigwa zaidi kwenye kadhia hiyo ni waandishi wa Habari, wengi wao wameporwa simu zao na vitendea kazi mbalimbali. Hata hivyo, juhudi za wasamaria wema na wananchi wa eneo hilo zilifanyika na wananchi wakapandisha ghorofani baada ya kusikia kelele za kuomba msaada, MUNGIKI wa Lipumba wakazidiwa nguvu na kukimbilia kwenye magari yao, wakatokomea kusikojulikana.
Katika kadhia hiyo, baadhi ya MUNGIKI hao walichelewa kuwahi magari waliyokuja nayo na inasemekana walianza kukimbilia vichochoroni ambako wananchi walishakusanyika, mifukuzano ikaanza. Tunaambiwa kuwa baadhi ya MUNGIKI hao, ( akiwemo huyu pichani) wamejeruhiwa vibaya na wananchi.
The Civic United Front (CUF) tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa hizo za kusikitisha, kughadhibisha na kutia aibu katika nchi yetu. Iweje leo katika nchi hii watu wavamiwe na makundi ya wahuni na kupigwa na kuumizwa? Iweje leo waandishi wa habari wazuiwe kuchukua habari za mambo muhimu ilimradi tu kuna genge la wahuni limeachwa lifanye litakavyo? Iweje leo, vyombo vya dola viendelee kulikumbatia kundi hili la Lipumba ambalo linaajita “MUNGIKI” huku likiachwa tu lijiite hivyo na kutenda hivyo.
Tukio hili la leo la Mabibo linanifanya niwakumbushe matukio mengine kadhaa ambayo MUNGIKI wa Lipumba wameyasimamia tena wakisaidia na POLISI ama wakati wa matukio hayo, au wakati wako chini ya vyombo vya Ulinzi na Usalama. Nitawakumbusha baadhi ya matukio hayo:
1. TUKIO LA KWANZA
Tukio la kutekwa kwa mhe. Joran Bashange (Kaimu Naibu Katibu Mkuu - Bara na Mkurugenzi wa Fedha wa chama). Watekaji walifanya tukio hilo majira ya saa 1.30 asubuhi tarehe 16/08/2016 mtaa wa Madenge, Buguruni wakiwa na PINGU na gari aina ya Noah yenye namba za Usajili T 670 CEX. Walimbeba Mhe. Bashange mzobemzobe na kumuingiza kwenye gari.
Bashange aliokolewa na wananchi waliolizunguka gari hilo na kuliwekea magogo, kisha wakawataka watekaji wajisalimishe na Polisi wakaitwa wakawakamata kwenye eneo la tukio wakawakuta na PINGU za Polisi, mikanda ya kijeshi n.k. Watekaji hao wanafahamika kwa majina ya Samweli Richard, Ramadhan Said na Shaibu Issa (Maarufu Mrangi) na walipohojiwa wakakiri kuwa wametumwa na Prof. Lipumba.
Bashange alipewa PF3 kwani aliumizwa kwenye zile purukushani, akapata matibabu kisha jalada ya upelelezi la kesi ya jinai la RB Namba BUG/IR/5937/2016 likafunguliwa. Baada ya siku chache watuhumiwa wote wakaachiwa, chama chetu kikaripoti suala hilo kwenye ofisi ya ZCO Dar Es Salaam, akamuamuru OCD wa Buguruni awafikishe watuhumiwa hao kwa ZCO. Watuhumiwa hao walipelekwa kwa ZCO na tokeo hapo hakuna kilichoendelea, walishaachiwa huru na hawakuwahi kufunguliwa mashtaka yoyote.
__________________________
2. TUKIO LA PILI
Tukio la Lipumba na kundi la MUNGIKI likisaidiwa, likilindwa na kuongozwa na POLISI lilipovamia, kupiga wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CUF mwezi Agosti 2016, kusababisha uharibifu mkubwa Blue Pearl Hotel, kusababisha Mkutano Mkuu wa CUF uhairishwe kwa sababu za kiusalama kabla ya kukamilisha ajenda ya pili ya mkutano ambayo ilikuwa imeanza, ya uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti wa CUF Taifa. Uhuni huo wa Mungiki na Lipumba ulikisababishia chama kulipa Shs Milioni 8.5 kwa Hotel ya Blue Pearl ili kufidia hasara ya uharibifu wa samani mbalimbali, lakini pia likakisababishia chama hasara ya Shs Milioni 800 ambazo ziliandaa Mkutano Mkuu huo maalum.
Tukio hili la uvamizi na upigwaji na uumizwaji wa Wajumbe wa Mkutano Mkuu liliripotiwa Kituo cha Polisi Magombeni na kupewa RB Namba MG/RB/9072/2016 ya 22/8/2016, maelezo ya walipigwa na kujeruhiwa yalichukuliwa, wakapewa PF3 wakapata matibabu, Jeshi la Polisi likapewa CD za tukio zima likionesha picha za video za MUNGIKI waliovamia na kujeruhi watu pamoja na majina yao, lakini hadi leo hajakamatwa wala kufunguliwa mashtaka yeyote kati yao.
__________________________
3. TUKIO LA TATU
Tukio la Lipumba na MUNGIKI kuvamia Ofisi Kuu ya CUF Buguruni tarehe 24/09/2017. Katika uvamizi huo, walinzi wa ofisi na walinzi maalum wa kampuni ya Ionsides Security Company walipigwa na kunyang’anywa Bunduki moja (ambayo baadaye MUNGIKI waliikabidhi kwa jeshi la Polisi). Jambo la kusikitisha ni kuwa, MUNGIKI na LIPUMBA walikuwa wanaongozwa na kusaidiwa na maafisa wa Jeshi la polisi na Askari Kanzu ambapo Polisi walikuwa na gari mbili wakiwa na silaha za moto, LIVE bila chenga!
Uvamizi huo ulihusisha kupiga na kuumiza vibaya walinzi wa zamu, na walinzi maalum wa Ironsides Security, kubomoa milango na mageti ya Ofisi kuu na kuharibu mali za chama (kwa kusindikizwa na kusaidiwa na Polisi). Chama kiliripoti suala hili Kituo Kikuu cha Buguruni (kwa ajili ya kutimiza matakwa ya kisheria – kesi ya nyani kwa ngedere) na likafunguliwa jalada la uchunguzi kupitia RB Namba BUG/RB/8741/2016 ya tarehe 24/9/2016. Hadi leo hii hakuna uchunguzi uliofanywa wala hatua zilizochukuliwa.
__________________________
4. TUKIO LA NNE
Tukio la kutekwa mwanachama wa CUF Mohamed Said, ambalo lilitokea tarehe 10/11/2016 katika eneo la Mahakama Kuu ya Tanzania mbele ya Polisi, baada ya kundi la MUNGIKI kuendesha vurugu kubwa huku Polisi wakishuhudia. Hii ilikuwa mojawapo ya siku ambazo kesi ya Bodi ya Wadhamini ya CUF dhidi ya Lipumba, Msajili wa Vyama na wenzao, ilikuwa inatajwa.
Baada ya Mohd Said kutekwa, alipelekwa hadi Ofisi Kuu ya CUF Buguruni akaingizwa ofisini kwa Lipumba akahojiwa na Lipumba kisha baadaye wakamuacha. Vipigo alivyopewa kwenye utekaji huo vilipelekea apate majeraha makubwa usoni na mdomoni.
Bwana Mohamed Said aliripoti Kituo cha Kati (Central Police) akapewa PF3 na kwenda kupata matibabu ikiwemo kushonwa nyuzi kadhaa na jalada la uchunguzi wa kijinai likafunguliwa kupitia RB Namba CD/CID/PE/88/2016.
Watekaji wale wanajulikana, polisi walipewa picha zao halisi za video na mnato, tangu wakati wanamkamata Bwana Mohd Said hadi wanamuingiza kwenye magari na kuondoka naye, bila ridhaa yake, tena mbele ya Polisi waliokuwa wamtanda mahakamani ili kulinda hali ya usalama. Lakini hadi leo hii, hakuna MUNGIKI aliyekamatwa wala kuhojiwa.
__________________________
5. TUKIO LA TANO
Tukio la kutekwa mhe. Joran Bashange (kwa mara ya pili) lililotokea tarehe 14/12/2016 kata ya Buguruni mkabala ya Shule ya Msingi Hekima. Kundi la MUNGIKI wa Lipumba zaidi ya 30 likajitokeza na kuanza kumshambulia likimlazimisha aingie kwenye gari ambayo haikujulikana (kwani ikimbia na baadhi ya watekaji waliotoroka).
Bashange akapiga kelele na mayowe ndipo wananchi waliokuwa karibu wakawadhibiti watekaji, wengine wakakimbia. Watekaji kadhaa waliowekwa chini ya ulinzi na wananchi wakakamatwa na POLISI baada ya wananchi kuomba msaada kwa njia ya simu. Walipohojiwa POLISI Kituo cha Buguruni wakadai wametumwa na Prof. Lipumba.
Baadhi ya waliokamatwa kwenye eneo la tukio na kufikishwa Kituoni wanajulikana kwa majina ya Twaha Ngozoma, Miraji Mtwibiliko. Jalada la upelelezi lenye RB Namba BUG/PE/116/2016 lilifunguliwa katika Kituo cha Polisi Buguruni siku hiyo hiyo.
Watuhumiwa hao (MUNGIKI) wakiwa bado rumande alifika Prof. Lipumba na kufanya mazungumzo na OCD kisha mmoja akaachiwa na mwingine akaachiwa kesho yake. Hadi leo tuongeavyo, hakuna mtuhumiwa aliyefikishwa mahakamani kutokana na tukio hilo la jinai.
__________________________
6. TUKIO LA SITA
Tukio la kuchomwa kisu mwanachama aitwaye Robert Samsoni eneo la shingo, lililotokea tarehe 14/12/2016 eneo la Mahakama Kuu ya Tanzania, mbele ya Polisi! Tukio hili lilifanywa na MUNGIKI wa Lipumba mbele ya kamera za waandishi wa habari wakiwepo na waliripoti hadi kwa picha za VIDEO, wachomaji na mchomwaji wako dhahiri kwenye video hizo.
Tukio hili lilianza baada ya MUNGIKI na Lipumba kuanza kupiga wanachama wa CUF waliohudhuria mahakamani katika kesi ya Bodhi ya Wadhamini wa CUF dhidi ya Lipumba na wenzake, ambapo mkakati wao ni kuhakikisha kwamba wananchama wanaogopeshwa ili wao tu (Mungiki) na Lipumba ndiyo wahudhurie mahakamani.
Tukio likaripotiwa Kituo cha Polisi Kati (Central Police) na PF3 ikatolewa, majeruhi akashonwa nyuzi takribani 12 (jeraha kubwa sana), majina ya MUNGIKI waliompiga na kumchoma kisu yakawasilishwa polisi, picha zao, makazi yao n.k.
Polisi wakafungua majalada ya uchunguzi namba CD/RB/12671/2016 na CD/IR/4567/2016 yote ya tarehe 14/12/2016. Hadi hivi leo tuzungumzavyo, hakuna mtuhumiwa aliyekamatwa wala kuhojiwa, sembuse kufikishwa mahakamani.
______________________________
Matukio yote haya ni ushahidi tosha kwamba, Vyombo vya Dola ndivyo vinalilea, kulipa mbinu na kuliendekeza hili kundi la Lipumba, na kwamba vinashirikiana nalo kuleta vurugu, kuumiza watu na kutisha wananchi kwa kutumia mgongo wa kile kinachoitwa "Mgogoro wa Uongozi ndani ya CUF."
Mathalini, Katibu wa CUF wa wilaya ya Kinondoni, hivi karibuni yeye na mtu mwingine aitwaye Ali Makwiro, waliongea na vyombo vya habari wilayani Kinondoni na kusisitiza kuwa wao wawili wanamuunga mkono Lipumba na harakati zake za sasa. Chama chetu na uongozi wake (Mimi na Kamati ya Uongozi ya chama, Katibu Mkuu Maalim Seif, Baraza Kuu, Kamati ya utendaji ya Taifa, Bodi ya Wadhamini), hata siku moja hatukuwahi kukaa na kufikiria achilia mbali hata kupanga HUJUMA zozote juu ya wanachama wachache wanaomuunga mkono Lipumba, au viongozi wachache wanaomuunga mkono, bali hata kuombea jambo hilo litokee.
Pamoja na Usaliti alioufanya Lipumba kwa chama, pamoja na kuungwa mkono na dola ili akivuruge chama, pamoja na upuuzi na ujinga wote aliousimamia tangu alipotangaza kuwa anarejea kuwa Mwenyekiti kwa lazima, sisi viongozi wa chama tunaotambulika na vikao vyote halali vya chama, hatukuwa kufikiria ku OPT njia ya mapambano na umwagani damu kama namna ya kumshinda Lipumba na genge lake.
Mara zote tumekuwa tunawasisitiza wanachama wetu kuwa watulivu na wasijihusishe na vitendo vya matumizi ya nguvu na vurugu. Hata wabunge wetu na wanachama wa Dar Es Salaam walipopanga tarehe ya kwenda kuipokonya Ofisi Kuu ya Buguruni kutoka kwa Lipumba, nilijitokeza hadharani na kuzuia zoezi hilo na mnakumbuka nilisisitiza kuwa siko tayari kuona damu ya hata mwanachama mmoja wa CUF inamwagika ati kwa sababu sisi ni wengi na tunataka kutumia wingi wetu kumtoa Lipumba na kigenge chake pale Buguruni.
As long as, Makao Makuu ya chama (Headquarter) yanayotambulika kikatiba yako Zanzibar, niliwaambia wanachama kuwa tumuachie Ofisi Kuu (Main Office) ili yeye atambe kwa kusaidiwa na dola na nikasema mimi ntafanyia shughuli zangu na Kamati ya Uongozi kutokea Makao Makuu na nikatoa mfano kwamba mbona CCM wanaendesha chama chao kutokea Dodoma? Msimamo huu ndiyo pia msimamo wa Katibu Mkuu wa CUF.
_______________________
Sisi ambao tunatambuliwa na vikao vya chama tumeamua kutumia njia sahihi kutatua mgogoro huu wa kutengenezwa, kwa nini upande huu unaoungwa mkono na vyombo vya dola, na serikali na chama kinachoongoza dola, unatumia njia za hatari namna hii katika kumpigania Lipumba waliyemtengeneza?
Kwa nini basi Mkutano wa Mwenyekiti wa Wilaya ya Kinondoni (anayeunga mkono chama na kumpinga Lipumba) uvamiwe na kuhujumiwa na watu waliotumwa na Lipumba huku nchi yetu ina vyombo vya dola? Mbona ule wa Katibu wa Kinondoni (anayemuunga mkono Lipumba) sisi hatukutuma wahuni wauvamie? Kwani sisi hatuwezi kufanya hivyo? Kwani kazi ya vyombo vya dola ni kusimamia wavaa vinyago na wabeba silaha za moto na baridi ili kuvamia shughuli halali za vyama au utoaji wa maoni?
Chama chetu kinasikitishwa sana na vitendo hivi vya watu kuvamiwa na MUNGIKI wanaoongozwa na Lipumba, kupigwa, kuchomwa visu, kutekwa n.k. ambapo kwenye masuala yote hayo, vyombo vya dola vimeendelea kumlinda Lipumba na genge lake dhidi ya chama na viongozi wake.
Kubwa kuliko yote, tumesikitishwa mno na kitendo cha hatari sana cha leo ambapo waandishi wa habari na viongozi wa chama wakiongoza na Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Kinondoni, wavamiwa na kupigwa na kundi hili la Lipumba lijiitalo “MUNGIKI’ (kama ilivyotokea leo Mabibo). Je, tukio hili lina maana gani? Lina maana kuwa waandishi wa habari wanatakiwa kuripoti habari za Lipumba tu, na kuhudhuria mikutano yake - na kwamba wasithubutu kusogelea mikutano ya viongozi halali wa chama (kama ilivyokuwa Mkutano huu wa leo wa Mkt wa CUF Kinondoni). Je, watanzania wanaona hali hii ni sawa tu? Je tukae kimya tu?
Je, dola, hata kama imewekeza nguvu kubwa kabisa kwenye mpango wa kuisambaratisha CUF kwa kumtumia Lipumba, na kwamba nguvu hiyo inawauma na lazima wamtumie wawezavyo hadi mwisho, kwa nini basi zisitumike mbinu za hujuma za kawaida kuliko hizi za kuteka viongozi, kuwapiga, kuwajeruhi, kuwavamia, kuwachoma visu na kuzuia shughuli zao?
Kwani usalama wa Taifa, ambao wanampangia Lipumba hujuma za namna hii hawana mbinu mbadala za kukimaliza chama cha siasa kisichotakiwa bila kutumia nguvu hii na makundi yenye mapanga na silaha za moto? Hivi unapotaka kukiua chama fulani cha siasa, ni lazima utumie nguvu za kijinga namna hii, zinazoweza kupelekea umwagaji damu bila sababu?
Natoa wito kwa IGP Mangu, Kamishna Sirro wa kanda maalum na ZCO wa Dar Es Salaam, kwamba haya yanayoendelea hivi sasa hadi viongozi wa juu wa CUF na waandishi wa habari kuanza kuvamiwa na mapanga na silaha za moto, kupigwa na kujeruhiwa, kutekwa, kuchomwa visu na kuumizwa, ni matunda ya JESHI LA POLISI ya kulilea kundi linalojiita MUNGIKI, lililoasisiwa na Lipumba na ambalo huenda linapata msaada mkubwa sana wa kiutendaji kutoka SERIKALINI!
Ndiyo maana mtu anaweza kushangaa, iweje kundi hilo litende mambo yote hayo, mpaka haya ya leo na hakuna MUNGIKI hata mmoja ambaye amewahi kufikishwa mahakamani. Mtanzania wa kawaida anaweza kujiuliza, MUNGIKI hawa wa Lipumba wanapata wapi Bastola za kutumia kuvamia mikutano halali kabisa? Dola inadhani kuwa tumeshasahau kitendo cha Nape Nauye kutolewa bastola na Ofisa wa Usalama wa Taifa?
Dola inadhani kuwa tumeshapoteza kumbukumbu kuwa watekaji wa msanii ‘Roma Mkatoliki’ na wenzake waliwatishia kwa Bastola kabla ya kuwatoa Tongwe Records. Hizi bastola ambazo sasa viongozi wa CUF na waandishi wa habari wanatishiwa na kundi la “Lipumba na Mungiki” tena hadharani mchana kweupe, wamepewa na nani? Hawaogopi dola?
Siku kundi hili la MUNGIKI litakapoendesha MAUAJI ntasikitika sana ntajapoona IGP na wenzake wakijitokeza kulaumu mauaji hayo na kudai kuwa wanawasaka wauaji. Nimeshaeleza huko awali kuwa wauaji huanza polepole, huanza kuvamia wakalindwana dola; hupiga na kuumiza wengine wakalindwa na dola; huteka, kutisha, kuchoma watu visu na wakalindwa na dola, huvamia mikutano halali na bastola na mapanga na kuumiza watu na wakalindwa na dola, na mwisho huanza kuua.
Tusubiri kundi hili la Lipumba lianze uuaji ndipo tubane pua kuwa tunalisaka! Na ifahamike kuwa chokochoko hizi ambazo zimefanywa na kundi la MUNGIKI tangu Agosti mwaka 2016 hadi leo bila kuchukuliwa hatua, ni uthibitisho mwingine dhahiri kuwa DOLA, POLISI n.k. wana HISA za kutosha kwenye kila kinachoitwa "Mgogoro wa Ndani ya CUF".
Mwisho, kwa niaba ya The Civic United Front (CUF) napenda kutoa pole zangu za dhati kwa waandishi wote wa habari waliopigwa katika kadhia hiyo, kunyang’anywa simu zao, vitendea kazi na fedha. Nawaomba waandishi wa habari na majukwaa yao tushikamane pamoja kuvibana vyombo vya dola vichukue hatua kali dhidi ya wahuni na MUNGIKI wote waliopanga njama na kutekeleza tukio la leo.
Naviomba pia vyombo vya habari vitathmini kama ipo haja ya kuendelea kutangaza habari za kundi hili la IBRAHIM LIPUMBA ambaye ndiye kiongozi mkuu wa kundi hili la MUNGIKI. Lakini Ofisi ya Katibu na sisi Kamati ya Uongozi tutatoa ushirikiano wote ambao unahitajika kwa viongozi wa vyombo vya habari na majukwaa yao katika kuhakikisha kwamba wahuni hawa wanaofugwa na Lipumba na dola, wanafika mwisho wao.
Nampa pole Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Kinondoni, Mhe, Juma Mkumbi, yeye na viongozi na wanachama wa CUF TAASISI walioko Kinondoni. Nameshawapigia simu na kuwataka waweke kumbukumbu sahihi za matukio yote yaliyotokea leo ikiwa ni pamoja na kusaidiana na Ofisi ya Katibu Mkuu kuyaripoti kwa IGP Mangu na wenzake ili kuweka rekodi sahihi bila kujali kuwa jeshi la Polisi litachukua hatua zozote au la!
(Pichani, ni mmoja wa MUNGIKI akiwa ameumizwa na mamia ya wananchi wenye hasira kali ambao walijitokeza kuwaokoa viongozi wa CUF na waandishi wa habari dhidi ya uvamizi. Nimejulishwa kuwa pia, wananchi hao wamepasua na kuharibu magari mawili yaliyokuwa yakitumiwa na MUNGIKI na kwamba MUNGIKI wengine walifanikiwa kutoroka, akiwemo yule aliyekuwa na BASTOLA. Kijana huyu anayeonekana pichani huonekana akimlinda LIPUMBA sehemu nyingi aendazo).
Julius Mtatiro,
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi,
22/04/2017.
Next Post Previous Post
Bukobawadau