Bukobawadau

HIVI PUNDE:VINARA WA NASA WAENDELEA KUDAI ODINGA NDIYE MSHINDI!!

Muungano wa upinzani Kenya umeendelea kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais yanayotangazwa na tume hiyo kwenye mtandao wake.

Viongozi wa muungano wa National Super Alliance wamesema walikutana na wakuu wa Tume ya Uchaguzi Kenya na kuwasilisha rasmi malalamiko yao kupitia barua.
Ajenti mkuu wa upinzani Musalia Mudavadi, ambaye ni naibu waziri mkuu wa zamani, amesema upinzani umepata maelezo zaidi kwamba matokeo ya uchaguzi yalivurugwa baada ya kudukuliwa kwa mitambo ya IEBC.
Wakuu wa IEBC wamekanusha kwamba mitambo ilidukuliwa. Mwenyekiti Wafula Chebukati amesema kulikuwa na jaribio la kudukua mitambo hiyo, lakini halikufanikiwa.

Bw Mudavadi amedai mgombea wa upinzani Raila Odinga ndiye aliyeshinda uchaguzi huo.
“Twamtaka mwenyekiti wa IEBC atangaze matokeo na kumtangaza Odinga na Kalonzo rais mteule na naibu rais mteule wa Kenya mara moja,” amesema Bw Mudavadi.

Nchini Kenya, ni kinyume cha sheria kwa mtu yeyote kutangaza matokeo au kusambaza matokeo ambayo hayajatoka kwa tume ya taifa ya uchaguzi. Ni tume hiyo ya uchaguzi pekee inayoruhusiwa kutangaza matokeo.

Bw Mudavadi ameendelea kuwaomba Wakenya kuwa watulivu.

CREDIT BBC
Next Post Previous Post
Bukobawadau