Bukobawadau

THRILLER IN NYAMAGANA

 Leo ni kumbukumbu ya miaka 43 tangu kufanyika kwa pambano la kihistoria la Yanga na Simba kwenye uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Pambano hilo la fainali ya mashindano ya kutafuta klabu bingwa ya taifa(ligi), lilibatizwa jina la Thriller in Nyamagana kutokana na mvuto lililoutengeneza. Waliolishuhudia wanasema ndilo pambano kali zaidi la Yanga na Simba katika historia ya wababe hawa.
Hili ndilo pambano la kwanza la kimashindano kuwakunanisha Yanga na Simba nje ya Dar Es Salaam. Pambano la kwanza lilikuwa la kirafiki lilifanyika Dodoma 1959.
Mashindano ya kutafuta klabu bingwa ya taifa 1974 yalifanyika kwa mara ya kwanza nje ya Dar Es Salaam, kuanzia Julai 18 mpaka Agosti 10(kama leo).
Kama kawaida, Yanga na Simba zilikiwepo sambamba na timu nyingine maarufu za wakati huo kama Nyota ya Mtwara, Mwadui ya Shinyanga na Jumuiya ya Arusha. Halafu kulikuwa na timu mpya kabisa kutoka Dodoma iliyoitwa Ntomoko.
Ukiziacha timu hizi, nyingi zilizobaki zilikuwa za taasisi au makampuni(timu za kazini) ikiwemo shule ya Rungwe Sekondari kutoka Mbeya.

Katika kujiandaa na mashindano haya, Yanga ilienda kuweka kambi nchini Brazil wakipata nafasi ya kutembelea uwanja wa Maracana na kupiga picha ziligeuka kuwa maarufu wakati huo. Simba waliokuwa mabingwa watetezi, walikwenda barani Ulaya nchini Poland.
Matokeo ya mechi za mwanzo
Magunia Kilimanjaro 5 - 4 Jeshi Zanzibar
Mwadui Shinyanga 8 - 0 Madaraka Ruvuma
Nyota Tanga 1 - 0 Polisi Bukoba
Nyota Afrika Morogoro 3 - 0 Jeshi Lindi
Nyota Mtwara 6 - 0 Coastal Stars Pwani
Kigoma Comworks 4 - 1 Kaye Iringa
Miembeni Zanzibar 4 - 2 Comworks Rukwa
Jumuiya Arusha 2 - 0 Mwatex Mwanza
Ntomoko Dodoma 3 - 0 Comworks Singida
Jeshi Tabora 4 - 1 Rungwe Sekondari Mbeya
Yanga 9 - 0 Kazi Mara
Magunia Kilimanjaro 2 - 1 Mwadui Shinyanga
Jeshi Tabora 2 - 1 Nyota Tanga
Nyota Mtwara 1 - 0 Nyota Morogoro
Simba 2 - 0 Ufundi Kigoma
Miembeni Zanzibar 3 - 1 Jumuiya Arusha
Yanga 5 - 1 Ntomoko Dodoma
Jeshi Tabora 2 - 1 Magunia Kilimanjaro
Simba 2 - 1 Nyota Mtwara
Yanga 2 - 1 Miembeni Zanzibar
Simba 3 - 0 Jeshi Tabora

Baada ya michezo ya awali iliyoendeshwa kwa mtindo wa mtoano, Yanga na Simba wakakutana fainali.
Dakika ya tano tu, Saad Ali wa Simba aliumia baada ya kugongana na Gibson Sembuli wa Yanga, akatolewa nje. Ilisemekana mahali walipongania, paliota kichuguu. Awali kulikuwa na taarifa kwamba mchezaji huyo alifariki alipofikishwa hospitali, lakini haikuwa hivyo.
Adam Sabu, aliyeingia kuchukua nafasi ya Saad Ali, aliipatia Simba bao la kuongoza dakika ya 16. Matokeo yaliendelea kubaki hivyo mpaka dakika ya 87 pale Gibson Sembuli alipoisawazishia Yanga. Mashabiki wa Yanga walishakata na kuanza kuondoka uwanjani...lakini bao hilo likawarudisha.
Dakika 90 zikaisha kwa sare na ikabidi ziongezwe 30 za ziada. Dakika ya 97, Sunday Manara, akipokea pasi ya kifua ya kaka yake, Kitwana Manara, akaifungia Yanga bao la ushindi.
Hiki kilikuwa kisasi kwa Yanga cha kufungwa na Simba kwenye nusu fainali ya mwaka 1973 na kuvuliwa ubingwa waliokuwa wameutwaa kwa miaka 5 mfululizo.
KUMBUKUMBU:
1. Mechi hii ndiyo ilikuwa ya mwisho kwa ligi ya mtindo wa mtoano, mwaka 1975, ikaanza ligi ya kuhesabu pointi, atakayepata pointi nyingi ndiyo mshindi
2. Baada ya mchezo huu, beki mashuhuri namba nne wa Yanga, Hassan Gobbos maarufu kama ‘King Hassan wa Morocco’, aliamua kutundika daruga na kumkabidhi majukumu Leodegar Chilla Tenga.
Zaidi ya Yanga, Gobos pia alizitumikia Mzizima United (timu ya Mkoa wa Dar Es Salaam). Tenga alipomrithi, alirithi na majukumu yote hayo.
VIKOSI
1. Yanga:
Elias Michael/Muhidin Fadhil
Ally Yussuf
Selemani Saidi Sanga
Hassan Gobbos/Boi Iddi 'Wickens'
Omari Kapera
Abdulrahman Juma (nahodha)
Bona Max Mwangi
Sunday Manara
Kitwana Manara
Gibson Sembuli
Maulid Dilunga

Kocha Tambwe Leya
2. Simba
Athumani Mambosasa
Shaaban Baraza
Mohammed Kajole
Athumani Juma
Omari Chogo
Omari Gumbo
Willy Mwaijibe/Kessy Manangu
Haidari Abeid 'Muchacho' (nahodha)
Saad Ally/Adamu Sabu
Abdallah Kibadeni
Abbas Dilunga ‘Sungura

Kocha: Paul 'West' Gwivaha
PICHANI
Kipa wa Simba, Athuman Mambosasa akiudaka mpira huku mshambuliaji wa Yanga, Kitwana Manara akimuangalia kwa makini. Hii ilikuwa kwenye mchezo huo.

Na Zaka Zakazi
Next Post Previous Post
Bukobawadau