Bukobawadau

WALLET ILIYOBEBA HADITHI NZURI YA MAPENZI

MAJIRA ya jioni nikielekea nyumbani, macho yangu yaligota kwenye wallet iliyodondoshwa njiani. Niliiokota na kuifungua ndan ili kuona kama kuna vitambulisho vitakavyowezesha kupata namba za mhusika ili nimpigie. Lakini ndani ya wallet mlikuwa na kiasi kidogo tu cha pesa pamoja na barua iliyooneka kuhifadhiwa mle kwa miaka mingi.
Bahasha iliyohifadhi barua ilikuwa shakavu mno; maandishi pekee yaliyoonekana vizuri ni anuani ya makazi ya mtumaji wa barua hiyo. Niliamua kuifungua barua ili kujaribu kutafuta walau dokezo la kusaidia kumpata mhusika. Mshangao wa kwanza ulionikumba baada ya kuifungua, ni tarehe iliyoandikwa barua hiyo: September, 1977. Barua iliandikwa takribani miaka 40 iliyopita.
Mwandiko mzuri wa kike ulipangwa vema juu ya karatasi ya rangi ya buluu, huku kwenye kona ya juu ya karatasi likipachikwa ua zuri jekundu - ua la upendo. Umahiri na utundu wa maneno ya mahaba uliotumika kuandika barua ile, vilinisismua ngozi ya mwili wangu. Mwandishi wa barua ile, ambaye mwishoni alijitambulisha kwa jina la Hudah, alikuwa akilalamika kwa uchungu, akimfahamisha mpenzi wake aitwaye Adrian, kwamba hawatoonana tena kwa sababu mama yake amemkatalia kuolewa, na ameamua kumhamisha. Pamoja na hayo, Hudah alisisitiza kwamba atampenda daima.
Kwakuwa zaidi ya anuani ya makazi iliyoandikwa juu ya bahasha, hapakuwa na mawasiliano mengine, nililazimika kuwapigia watu wa mamlaka za makazi ili kuona kama wanaweza kunisaidia.
Baada ya mhudumu wa simu kupokea nilisema, "Kumradhi, nina ombi binafsi. Ninajaribu kumtafuta mmiliki wa wallet niliyoiokota. Je, kuna namna yoyote ya kupata namba za simu endapo nitakutajia anuani ya makazi iliyoandikwa kwenye bahasha?"
Kwa uzito wa ombi hilo, mhudumu alipendekeza nizungumze na bosi wake, ambaye baada ya kunisikiliza na kusuasua kufanya maamuzi hatimaye alisema, "Sawa, tunayo orodha hapa ya namba za simu kwenye anuani uiliyotaja, lakini siruhusiwi kukupatia." Alinifafanulia kiuadilifu kabisa kwamba, kwa misingi yao ya kazi itabidi yeye ndiye apige namba hizo na kuwasimulia habari ya wallet kisha endapo wataruhusu, ndipo ataniunganisha nao.
Nilisubiri kwenye simu kwa dakika kadhaa. Kisha akarudi hewani na kuniambia: "Kuna mtu nimempata, nafikiri anaweza kukusaidia."
Baada ya kuniunganisha kwa simu na huyo anayehusika na anuani niliyoikuta kwenye bahasha, nilimuuliza kama anamjua mtu aitwaye Hudah. Baada ya kutafakari akajibj, "Ooh, tulinunua hii nyumba kutoka kwa familia iliyokuwa na binti aitwaye Hudah. Lakini hiyo ilikuwa ni miaka karibu 40 iliyopita."
"Unaweza kujua mahala wanakopatikana kwa sasa?" Nilimuuliza.
"Hapana. Ila nachokumbuka, miaka kadhaa iliyopita Hudah alimpeleka mama yake kuhudumiwa na kulelewa kwenye moja kati ya nursing home (taasisi za kuhudumia na kulea wazee)," alinijibu. "Labda ukiwasiliana nao, wanaweza kumpata huyo binti."
Akanipa jina la hiyo taasisi, na papo hapo nikawapigia na kumuulizia mama Hudah. Walinijibu kwamba mama huyo alishafariki miaka kadhaa nyuma, lakini wanazo namba za simu za mahala wanapoweza kunisaidia kumpata Hudah. Niliwashukuru kwa msaada wao, kisha nikapiga hizo namba. Aliyepokea simu, alinijibu kwamba kwa sasa Hudah amekuwa mtu mzima sana, hivyo naye anaishi kwenye taasisi nyingine ya kuhudumia wazee, kama ilivyokuwa kwa marehemu mama yake.
Kufikia hapo, nilianza kujiona mpuuzi kwa kumfuatilia mtu aliyedondosha wallet, isiyokuwa hata na pesa nyingi zaidi ya barua chakavu yenye zaidi ya miaka 40. Pamoja na hayo, nilijaribu kupiga namba za huko anakulelewa Hudah. Aliyepokea simu alisema, "Ndiyo, Hudahh anaishi nasi hapa."
Nikashusha pumzi. Ingawaje ilikwisha kutimu saa nne usiku, niliomba kama wataniruhusu niende kumwona usiku uleule. Walinikubalia. Niliwashukuru na kuanza kuendesha gari yangu hadi hapo kwenye taasisi yao.
Walionilaki baada ya kuwasili ni mlinzi pamoja mhudumu wa zamu. Baada ya kujuliana hali na kujitambulisha, mhudumu alinichukua hadi hadi ghorofa ya pili, tulipomkuta bi mkubwa mmoja akitazama runinga huku akinywa kahawa. Mhudumu alinitambulisha kwake; alikuwa Hudah.
Pamoja na uzee kukaribisha mvi kichwani na makunyanzi usoni, lakini bado tunu ya urembo iliupamba wajihi wake. Baada ya kusalimiana huku akionesha tabasamu na bashasha, nilimsimulia kuhusu wallet niliyoiokota huku nikimwonesha ile barua. Baada ya kuitazama kwa muda barua ile ikiwa na ua lake jekundu kwa juu, Bi Hudah alishusha pumzi kwa nguvu na kufuta machozi yaliyoanza kutengeneza mifereji mashavuni. Mara akasema, "Kijana, barua hii ndiyo iliyotamatimisha mawasiliano yangu na Adrian."
Baada ya ukimya kutanda kwa muda akaendela, "Hakika nilimpenda sana. Lakini wakati huo, nilikuwa na umri wa miaka 16 tu. Hivyo, mama yangu akanikomesha kuwasiliana naye. Ooh, Adrian alikuwa kijana mtanashati na muungwana sijapata kuona ... Aah, Adrian Majumbi ... Kama utabahatika kumpata, mwambie bado nampenda."
Baada ya macho yake kuanza tena kutirirsha machozi, alitulia kidogo akaendelea, "Unajua, tangu kutenganishwa naye sikutaka tena kuolewa, nikiamini sitapata mwingine wa kufanana naye."
Mwisho mazungumzo, nilimshukuru Hudah na kumuaga. Nikaingia kwenye lifti na kuteremka hadi chini. Nikiwa natoka ndani ya lifti, nikamsikia yule mlinzi aliyenipokea mwanzo akinisemesha, "Vipi, bi mkubwa ameweza kukusaidia?"
"Si sana. Lakini walau nimepata jina la mwisho la huyo mmiliki wa wallet hii nimtafutaye. Japo itachukua muda, si kwa sasa tena. Leo nimetumia muda wangu mwingi kumsaka." Nilijibu huku nikiingiza ile wallet kwenye mfuko wa suruali.
"Hey, hebu ngoja kidogo," mlinzi alisema huku mkono na macho yake vikielekea kwenye ile wallet. "Nadhani nimeijua hiyo wallet, itakuwa ni ya mzee Majumbi. Amekwisha idondosha karibu mara tatu humu, na mimi ndiye nimekuwa nikimuokotea, hivyo popote niionapo huitambua, hasa hicho kiji-capet chekundu kwa juu hunisaidia kuijua."
"Ni nani huyo mzee Majumbi?" Haraka nilimuuliza baada ya kukumbuka kuwa nimetajiwa jina hilo pia na bi Hudah.
"Naye ni mzee anayehudumiwa na kuishi hapa. Nina hakika hiyo ni wallet yake, na atakuwa aliidondosha alipokuwa matembezini."
Mungu wangu! Isije ikawa ndiyo huyo ninayemtafuta. Haya kweli yatakuwa maajabu.
Nilimshukuru mlinzi, kisha haraka nilirudi kwa mhudumu wa zamu. Nikamjuza nilichoambiwa na mlinzi. Tukatoka na kuongozana pamoja kwenye lifti na kupanda hadi ghorofa ya tano. Niliendelea kufanya maombi ili huyo mzee awe ndiye mwenyewe. Tulipofika, tulimkuta mzee Majumbi akijisomea kitabu katika chumba cha mapumziko.
Baada ya kuamkiana, mhudumu alimuuliza kama alipoteza wallet yake. Upesi akajipekua mifukoni na kukiri, "Ooh, haipo. Nimeipoteza tena."
"Basi huyu kijana ameikota, akawa anajaribu kukutafuta akiamini ni yako!"
Nilimkabidhi wallet yake. Na mara baada ya kuitupia jicho, alitabasamu na kunishukuru. Alipotaka kunipa pesa kama bahshishi nilikataa. Nikamwambia, "Labda nina jambo moja tu la kukwambia. Nimesoma barua iliyokuwemo kwenye wallet wakati nikijaribu kumjua mmiliki."
Tabasamu lililotamalaki usoni mwake tangu alipopokea wallet yake, liliyeyuka mfano wa theluji iliyowekwa jikoni. "Umeisoma barua?"
"Sikuishia tu kuisoma, bali mpaka nimemtafuta Hudah na kumpata."
"Hudah?!" Mzee Majumbi aliruka kwa mshituko. "Unapajua anapopatikana Hudah? Siamini. Unaweza kunithibitishia urembo ungali maungoni mwake? Tafadhali nipe habari zake."
"Hudah hajambo, nafikiri ukimwona utakubaliana nami kwamba amekuwa mrembo zaidi ya alivyokuwa ujanani," nilijibu huku nimetabasamu.
Mzee Majumbi alitabasamu kwa faraja na kuuliza tena, "Unaweza kunielekeza anapoishi? Ngoja. Nikwambie kitu, kijana? Kipindi napokea barua hii uliyoisoma, nilikuwa nimezama katika bahari ya huba la Hudah. Kama ulivyoona kilichoandikwa humo, kinaweza kumuumiza na kumsambaratisha yeyote aliyezama penzini. Basi ilikuwa hivyo kwangu - nilikataa tamaa na sikuoa tena. Na mpaka hii leo, niliendelea kumpenda yeye tu."
"Mzee Majumbi," nilimkatisha, "tufuatane huku."
Tulitoka na kwenda mpaka kwenye lifti iliyotuteremsha hadi ghorofa ya pili. Kwa sababu ya usiku kuzidi kuwa mkubwa, utulivu ulihanikiza jengo zima. Wengi walikuwa wamelala. Kwa bahati, tulimkuta bi Hudah peke yake akiendelea kuangalia runinga. Mhudumu akamsogelea.
"Bi Hudah," alimwita kwa utulivu, huku akimnyooshea kidole mzee Majumbi. "Unamfahamu huyo mzee?"
Hudah alivua miwani yake taratibu, akamtazama kwa muda mzee Majumbi bila kusema chochote. Hudah akiwa angali ameduwaa, mzee Majumbi alisema kwa sauti isiyo kubwa wala ya kunong'ona, "Hudah - siamini macho yangu. Ni wewe kweli?"
"Mungu wangu! Adrian ni wewe? Ooh, sitaki kuamini. Adrian wangu!"
Walipovamiana na kukumbatiana, mimi na mhudumu tukatoka zetu nje.
"Tazama maajabu ya Mungu," mhudumu aliniambia wakati tukishuka na lifti, "Hivyo ndivyo Mungu anavyofanya kazi zake, kwa ufundi na malengo mahsusi."
Nilibaki kimya huku nikitafakari endapo ningeipuuza wallet ile ningetenda kosa kubwa sana. Hakika hatupaswi kupuuza vitu hata kama ni vidogo namna gani.
Takribani wiki tatu baadaye, nikiwa kazini kwangu nilipokea simu toka kwa yule mhudumu: "Tafadhali jitahidi siku ya Jumapili uhudhurie harusi. Hudah na Adrian wanafunga ndoa!"
Salaale!
Naam. Nilihudhuria. Hakika harusi ilifana vilivyo. Wazee wote wanaohudumiwa katika taasisi hiyo walihudhuria wakiwa wamependeza mno. Bi Hudah alionekana mrembo mara dufu akiwa ndani ya shela, huku bwana Adrian akionekana mtashati ndani ya suti yenye rangi ya samawati. Muda huo mimi nikiwa ndani ya suti ya rangi ya hudhurungi, nilisimama pembezoni mwao kama mshenga. Amaa kweli hawakukosea wahenga waliosema "Kama ipo, ipo tu.". Yaani penzi lililopotea miaka takribani hamsini, limechipua upya baada ya wapenzi waliokuwa wakisubiriana, kukutana tena.
Kama hujawahi kuona wapenzi wazee; mume mwenye miaka 70 na mke miaka 65, wakifurahiana na kupendezana kama vijana wa miaka 30, nitafute nikuoneshe picha yao siku ya harusi.
- Maundu Mwingizi (Mwanabalagha)
Next Post Previous Post
Bukobawadau