Bukobawadau

SERIKALI: MATUMIZI YA DOLA NCHINI HAYAATHIRI KUSHUKA KWA THAMANI YA SHILINGI


Serikali imesema kuwa kushuka au kupanda kwa thamani ya shilingi nchini hakusababishwi na bidhaa na huduma mbalimbali kutozwa kwa dola bali kunatokana na misingi ya shughuli mbalimbali za kiuchumi (Macroeconomic fundamentals) pamoja na hali halisi ya uchumi wa nchi zinazofanya biashara na Tanzania.
Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Vwawa Mhe. Japhet Hasunga (CCM), aliyetaka kujua mikakati ya Serikali katika kuimarisha thamani ya shilingi ya Tanzania na kupiga marufuku matumizi ya fedha za kigeni nchini.
Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji aliainisha kuwa nakisi ya urari wa biashara, mfumuko wa bei na tofauti ya misimu (seasonal factors) ni sababu kuu zinazosababisha kushuka na kupanda kwa thamani ya shilingi nchini.
Dkt. Kijaji aliliambia Bunge kuwa ili kuimarisha thamani ya shilingi Benki Kuu inaendelea kuthibiti mfumuko wa bei ili usitofautiane sana na wabia wa biashara nchini.
“Benki Kuu imethibiti biashara ya maoteo (speculation) katika soko la fedha za kigeni ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa miamala ya fedha za kigeni inafanywa na benki kwa ajili ya shughuli za kiuchumi tu na sio biashara ya maoteo, hali hii itasaidia upatikanaji wa fedha za kigeni katika soko la rejareja ili kupunguza shinikizo la kuporomoka kwa thamani ya shilingi.”Alisema Dkt Kijaji.
Dkt. Kijaji alifafanua kuwa pamoja na hatua zinazochukuliwa na Benki Kuu ufumbuzi wa kudumu wa kutengamaa kwa thamani ya shilingi nchini hutegemea zaidi kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho wa mali nchi za nje.
Imetolewa na:

Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
11/9/2017
Next Post Previous Post
Bukobawadau