BENKI KUU KUDHIBITI UKWASI WA MABENKI NA WANANCHI
Serikali
imesema kuwa Benki Kuu inatekeleza sera ya fedha inayolenga kudhibiti ukwasi
ili uendane na mahitaji halisi ya uchumi kwa lengo la kuuimarisha na kudumisha
utulivu wa mfumuko wa bei.
Kauli
hiyo imetolewa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Same
Magharibi Mhe. Mathayo David Mathayo (CCM), aliyetaka kujua mikakati ya
Serikali ya kuongeza ukwasi katika mabenki na wananchi ili washirikiane na
Serikali katika kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja, kaya na Taifa kwa ujumla
Dkt.
Kijaji alisema kuwa, hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Benki Kuu
zimesababisha hali ya ukwasi katika Sekta ya Fedha hususan benki mzuri na
hakuna vihatarishi vinavyoweza kusababisha madhara hasi katika uchumi.
Dkt.
Kijaji alifafanua kuwa kati ya Julai 2016 na Julai 2017, kiwango cha ukwasi
katika benki kwa ujumla wake kiliongezeka kutoka asilimia 35.53 hadi asilimia
38.41.
“Kiwango cha ukwasi wa asilimia 38.41 ni mzuri
zaidi katika uchumi, ikilinganishwa na kiwango cha chini cha asilimia 20
kinachotakiwa na Benki Kuu ya Tanzania”. Alisema Dkt. Kijaji.
Alisema
kuwa kuimarika kwa ukwasi kunatokana na hatua mbalimbali za kisera zilizochukuliwa
na Benki Kuu, miongoni mwa hatua hizo ni kutoa mikopo ya muda mfupi kwa benki,
kununua fedha za kigeni katika soko la jumla la fedha za kigeni na kushusha
riba inayotozwa kwa benki za biashara na Serikali wanapokopa Benki Kuu.
Dkt.
Kijaji aliongeza kuwa Benki Kuu itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za
kuimarisha masoko ya fedha kwa lengo la kuhakikisha kwamba yanaendeshwa kwa
ufanisi na ushindani ili kusaidia kuongeza ukwasi miongoni mwa mabenki na
Taasisi nyingine za kifedha.
Imetolewa
na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
11/9/2017