Bukobawadau

SERIKALI KUONGEZA FURSA ZA WAHANDISI


Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John Kijazi, akihutubia wahandisi (hawapo pichani), katika sherehe za ufunguzi za Mkutano wa 15 wa mwaka wa wahandisi uliofanyika leo mjini Dodoma.

Baadhi ya wahandisi wakimsikiliza Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John Kijazi (hayupo pichani), katika sherehe za ufunguzi za Mkutano wa 15 wa mwaka wa wahandisi uliofanyika leo mjini Dodoma.

Baadhi ya wahandisi wakila kiapo cha utii cha kihandisi katika Mkutano wa 15 wa mwaka wa wahandisi uliofanyika leo mjini Dodoma.

Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John Kijazi, akimkabidhi cheti Mbunge wa Bagamoyo ambaye pia ni Mhandisi  Dkt, Shukuru Kawambwa mara baada ya kula kiapo katika sherehe za ufunguzi za Mkutano wa 15 wa mwaka wa wahandisi uliofanyika leo mjini Dodoma. Watatu kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Edwin Ngonyani, akishuhudia tukio hilo.

Mmoja wa wanafunzi bora wa kike waliofanya vizuri katika masomo ya kihandisi akipokea cheti kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John Kijazi, katika sherehe za ufunguzi za Mkutano wa 15 wa mwaka wa wahandisi uliofanyika leo mjini Dodoma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB), Profesa Ninatubu Lema, akimpa zawadi Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John Kijazi yenye picha yake katika sherehe za ufunguzi za Mkutano wa 15 wa mwaka wa wahandisi uliofanyika leo mjini Dodoma.


SERIKALI KUONGEZA FURSA ZA WAHANDISI
Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John Kijazi, amesema Serikali inafanya jitihada za kipekee kuongeza idadi ya wahandisi nchini ili kuiwezesha nchi kuwa na rasilimali watu ya kutosha katika fani ya Uhandisi, Sayansi, Hisabati na Teknolojia na hivyo kuharakisha ujenzi, ustawi, maendeleo ya viwanda na miundombinu.
Akizungumza katika madhimisho ya 15 ya Wahandisi yaliyoanza leo mjini Dodoma, Mhandisi Balozi Kijazi ameitaka Bodi ya Usajili wa Wahandisi Nchini (ERB), kuhakikisha wahandisi wanaoongezeka  wanakuwa na viwango vya kutosha vya kitaaluma, kiujuzi na maadili ili kuleta matokeo chanya ndani na nje ya nchi.
"Serikali itahakikisha inafanya kila namna kuongeza nguvu kazi ya kutosha hasa  katika kipindi hiki cha kujenga uchumi wa viwanda ili kuweza kuzipatia ufumbuzi changamoto za miundombinu, kiuchumi na kijamii", amesema Mhandisi Balozi Kijazi.
Ameongeza kuwa kutokana na mahitaji makubwa ya mafundi sanifu kwenye uendelezaji wa viwanda, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), itatenga fedha kwa ajili ya kusomesha wataalamu hao kwa kiwango cha Stahahada (Diploma), katika vyuo mbalimbali nchini ili kupunguza uwiano baina ya wahandisi, mafundi sanifu na mafundi mchundo.
Aidha, ameipongeza Bodi hiyo kwa kusimamia utoaji wa mafunzo ya kuendeleza taaluma ya kihandisi yenye lengo la kuhakikisha wahandisi wanaendana na mabadiliko ya kisayansi na kiteknolojia katika utekelezaji wa majukumu yao.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, amesema kuwa Sekta ya Ujenzi itahakikisha taaluma ya uhandisi inakua kwa kuwaendeleza wahandisi kielimu na kimitaji ili waweze kujenga uchumi imara wa nchi na kuharakisha maendeleo.
Ameongeza kuwa Wahandisi wanaunga mkono nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kufikia uchumi wa kati kwa kupitia viwanda ili kukidhi matarajio ya wananchi katika nyanja mbalimbali ifikapo 2025.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa ERB Mhandisi Prof. Ninatubu Lema, amemhakikishia Katibu Mkuu Kiongozi kuwa wahandisi wataendelea kufanya kazi zao kwa weledi, nidhamu na kuzingatia maadili yao ya kazi kama wanavyoapa kufanya hivyo.
Amemuomba Katibu Mkuu Kiongozi, kuboresha mazingira ya  Wahandisi nchini kwa kuwapa miradi mikubwa ya ujenzi wahandisi wazalendo ili kuwajengea uwezo wa ujenzi na usimamizi wake.
Zaidi ya wahandisi 2000 wameshiriki katika maadhimisho hayo ya 15 ya wahandisi yenye kauli mbiu "Jukumu la Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati katika Kukuza Viwanda kwa Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi", ambapo  wahandisi 150 wamekula kiapo cha utii na uaminifu.
Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Next Post Previous Post
Bukobawadau