Mkuu wa Mkoa ametoa taarifa kwa vyombo vya Habari juu ya suala hilo kama ifuatavyo:
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI TAREHE 13 SEPTEMBA, 2O17
Ndugu Waandishi wa Habari, Nimewaiteni hapa ili kutoa maagizo na
Maamuzi ya Serikali juu ya ubainishaji na uendelezaji wa nyanda za
malisho katika eneo la Mwisa II katika Wilaya za Muleba na Karagwe.
Uendelezaji wa eneo la Mwisa II kwa ajili ya ufugaji ni mpango ulioanza
miaka ya nyuma na ulianza kwa mradi wa kuzuia ndorobo ulioendeshwa na
Wizara yenye dhamana ya Mifugo kwa wakati huo kwa lengo la kuufanya
uwanda wa Mwisa II kuwa na ufugaji wenye tija na endelevu. Eneo la Mwisa
II ni eneo linaloanzia katika mipaka ya Ranchi ya Kagoma, kupitia Bonde
la Ziwa Burigi hadi Pori la Akiba la Burigi.
Ndugu Waandishi wa
Habari, Lengo la uendelezaji wa eneo la Mwisa II ni kuviendeleza vijiji
vinavyogusa eneo la Mwisa II na kuongeza kipato kwa kupunguza umasikini
kwa wananchi katika ngazi za Vijiji, Halmashauri husika, Mkoa na Taifa
kwa ujumla. Mpango huu ni fursa kwa Mkoa wa Kagera kujikwamua kiuchumi
na kutoka nafasi unaoshika kwa sasa ambayo ni ya tatu toka chini kwa
kipato Kitaifa.
Mpango huu utaondoa ufugaji holela na ukataji wa
miti ovyo na kuwezesha uzalishaji mifugo kisasa na kibiashara bila
kuharibu mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo. Pia,
mpango huu unatarajiwa kuwezesha upatikanaji wa maeneo ya malisho kwa
ajili ya wafugaji wa Kitanzania walioondolewa kwenye Misitu ya Hifadhi
na Mapori ya Akiba na hivyo kutatua migogoro baina ya wafugaji na
watumiaji wengine wa ardhi.
Ndugu Waandishi wa Habari, Mpango huu
wa uendelezaji wa Mwisa II ni utekelezaji wa Maagizo na Maelekezo ya
Viongozi Wakuu wa Serikali ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Rais wakati wa
ziara yake Mkoani Kagera mwezi Julai, 2017 ambaye alisisitiza hifadhi
endelevu ya Misitu ya Hifadhi na Mapori ya Akiba na wananchi kupunguza
mifugo yao na kufuga kisasa na kibiashara kufuatana na ardhi waliyonayo.
Aidha, utekelezaji wa mpango huu unaenda sambamba na Maagizo
yaliyotolewa na Mheshimiwa Makamu wa Rais mwaka 2016 kwa Mikoa kutenga
maeneo ya wafugaji pindi agizo litakapotolewa la kuondoa mifugo toka
kwenye maeneo ya Hifadhi ambapo Mkoa uliainisha eneo la Mwisa II kuwa ni
nyanda za malisho. Aidha, Mwezi Juni 2017, Mheshimiwa Waziri Mkuu
alipokutana na Maafisa Mifugo wa Mikoa na Halmashauri zote Tanzania
Mkoanii Dodoma aliagiza maeneo ya wafugaji yatengwe, yapimwe na
yamilikishwe kwa wafugaji.
Ndugu Waandishi wa Habari, Mpango huu
wa uendelezaji wa Mwisa II utawezesha upatikanaji endelevu wa mali ghafi
za viwanda vya nyama, maziwa na bidhaa zake, ngozi na bidhaa zake na
kadhalika. Pia mpango huu ni utekelezaji wa Sera ya Serikali ya Awamu ya
Tano ya uwekezaji wa viwanda ili kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka
2025 na kuongeza ajira kwa Watanzania.
Ndugu Waandishi wa Habari,
(angalizo) Ili kutekeleza azima ya uendelezaji wa eneo la Mwisa II
hatua mbalimbali zitatekelezwa bila kuathiri mipaka ya Vijiji,
kunyang‘anya ardhi ya Vijiji au kuathiri miradi iliyopo ikiwa ni pamoja
na mradi wa umwagiliaji wa IKAKI unaogusa vijiji vya Itunzi, Kashalala
na Kiteme. Hatua hizo ni kama zilivyoainishwa hapa chini:-
Ndugu
Waandishi wa Habari, Hatua ambazo tayari zimechukuliwa au
zitakazochukuliwa ni kama ifuatavyo: Kwanza Timu ya Wataalam ngazi ya
Wizara, Mkoa, na Halmashauri husika tayari imekutana na wajumbe wa
Halmashauri za Vijiji na Madiwani kwa ajili ya kuwaelimisha juu ya zoezi
la ubainishaji wa eneo la Mwisa II katika maeneo yao na elimu
inaendelea kutolewa. Pili, Wataalamu kwa kushirikiana na Watendaji wa
Vijiji na viongozi wa Vijiji wanaendelea kubaini eneo la Mwisa II na
kuliwekea alama kwenye mipaka ya nje.
Tatu, Baada ya Timu
kukamilisha hatua mbili za mwanzo eneo la Mwisa II litagawiwa katika
Vitalu kwa kuweka alama kulingana na jiografia ya eneo husika,
upatikanaji wa nyanda za malisho, maeneo ya maji, maeneo ya makazi,
huduma za kijamii na miundombinu mbalimbali inayopatikana katika eneo
hilo.
Ndugu Waandishi wa Habari, Hatua ya Nne itakuwa ni
kukamilisha kazi ya Upimaji kwa kutumia (GPS set). Tano, ni kusajili
vitalu na kuvipa namba za usajili utakaofanywa na Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Hatua ya Sita na ya mwisho itakuwa
ni ushirikishwaji kuanzia ngazi za Vijiji, Wilaya na Mkoa kwa
kuwatambua wananchi watakaopendekezwa kumilikishwa vitalu aidha,
kipaumbele kitakuwa kwa Wanavijiji watakaojiunga katika ushirika wa
wafugaji.
Ndugu Waandishi wa Habari, (Maagizo) Ili kufanikisha
mpango huu ambao upo kwa ajili ya faida ya wananchi, Vijiji husika,
Wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla naagiza yafuatayo yatekelezwe;
Moja, Viongozi, Watendaji na Wataalam wa ngazi zote washirikiane wakiwa na msimamo na Dira moja.
Pili, Waheshimiwa Mawaziri wa Sekta zinazohusika naomba watoe
ushirikiano na uwezeshaji unaohitajika ikiwemo Ofisi ya Rais – TAMISEMI,
Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi,
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Viwanda
Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Waheshimiwa
Wabunge wa Mkoa wa Kagera, na Wawakilishi wengine wa Wananchi.
Ndugu Waandishi wa Habari, Mwisho napenda kuwakumbusha wananchi wote
kuwa ni wajibu wa kila mmoja wetu kuwajibika ipasavyo katika kulinda,
kuhifadhi na kutunza maliasili za misitu, Mapori ya Akiba, Maeneo ya
Hifadhi na vyanzo vya maji ili kuepusha Mkoa wetu kugeuka jangwa na
kuendeleza ufugaji wenye Tija na Kibiashara.
Ilitolewa na; Mhe. Meja Jenerali (Mst) Salum M. Kijuu
Mkuu wa Mkoa
KAGERA
13 Septemba, 2017
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comment:
Post a Comment