Bukobawadau

WAZEE MKOANI KAGERA WANUFAIKA NA VITAMBULISHO VYA KUPATIWA HUDUMA ZA AFYA BURE NA MAPAMBANO DHIDI YA MALARIA YAENDELEA

Mkuu wa Mkoa Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu afanya ziara ya kukagua huduma za afya Mkoani Kagera na kuzindua unyunyiziaji wa dawa ya kuua viluilui katika mazalia ya mbu ili kupunguza tatizo la malaria mkoani hapa.
Ziara hiyo iliyoanza tarehe 12 Septemba, 2017 katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Mhe. Kijuu alizindua ugawaji wa vitambulisho vya kupata huduma ya afya kwa wazee ili watibiwe katika vituo vya afya bure bila malipo yoyote.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa alilenga kukagua na kujihakikishia uwepo wa dawa katika vituo mbalimbali vya afya kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi. Pili alilenga kuhamasisha wananchi kujikinga na kuchukua hatua za kupambana na ugonjwa wa Malaria ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo katika Mkoa wa Kagera.
Aidha, Mkuu wa Mkoa alilenga kuhamasisha vituo vyote vya afya kutumia mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielekitroniki ili kuongeza mapato yatayoboresha huduma kwa wananchi. Katika ziara hiyo Mhe. Kijuu alijihakikishia kuwa dawa zipo za kutosha kwenye vituo na kutoa rai kwa wananchi kufika katika vituo hivyo pindi wanapohisi wanaumwa ili kupatiwa huduma za matibabu.
Katika ziara hiyo Mhe. Kijuu aliwasistiza watendaji wa Halmashaui za Wilaya kuhakikisha wazee wanapatiwa vitambulisho na kusema kuwa wazee hao wakati wa ujana wao walizalisha na kulitumikia taifa kwa nguvu zao zote na sasa ni wakati wao kuhudumiwa hasa kupatiwa huduma za afya bure bila kutozwa fedha zozote.
Aidha, Mhe. Kijuu alimpongeza Rais John Pombe Magufuli ambaye naiongoza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwakumbuka wazee na kuwapatia vitambulisho ambavyo vitawaruhusu wazee wa Tanzania kupatiwa huduma za afya bure bila malipo.
Katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba tayari wazee 900 wametambuliwa na kupewa vitambulisho, Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi tayari wazee 1500 wametambuliwa na wanatarajiwa kupatiwa vitambulisho na Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Zaidi ya Wazee 200 tayari wamepatiwa vitambulisho vya kupatiwa huduma ya afya bure.
Agizo ni kuwa Halmashauri zote zinatakiwa kuwatambua wazee na kuwapatia vitambulisho hivyo. Aidha Mhe. Kijuu aliziagiza Halmashauri zote kuhakikisha zinanyunyizia dawa ya kuua viluilui katika madimbwi, kandokando ya mito ili kuharibu mazalia ya mbu, pia kuhakikisha Halmashauri zote zenye shehena ya dawa katika maghara ya dawa, dawa hizo zisambazwe vituoni ili kutoa huduma kwa wananchi.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Dk. Thomas Rutachunzibwa katika ziara hizo alitoa rai kwa watendaji wa Halmashauri kuona umuhimu wa kufunga mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielekitroniki ili kuongeza mapato katika vituo hivyo jambo ambalo litaboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na kuacha utegemezi na vituo kujiendesha vyenyewe kwa makusanyo yao wenyewe.
Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu alitembelea vituo vya afya Rubale Wilayani Bukoba, Buyango na Bunazi Wilayani Missenyi, pia na Kituo cha Afya Zamzam Manispaa ya Bukoba. Vilevile alitembelea maeneo dawa ya kuua viluilui inakonyunyiziwa hasa katika madimbwi na maji yaliyotuhama
Next Post Previous Post
Bukobawadau