Bukobawadau

RUGE MUTAHABA, JINA KUBWA, MWILI MDOGO, MAMBO MAKUBWA!

Anaandika Privatus Karugendo 
RUGE MUTAHABA, JINA KUBWA, MWILI MDOGO, MAMBO MAKUBWA!
Mwaka 2015, nilishiriki kiasi kizima kampeni za uchaguzi mkuu kwa asilimia zote. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kushiriki kampeni za uchaguzi. Nilijifunza mambo mengi na hasa kuwafahamu kwa karibu wanasiasa. Kusema ukweli zoezi hili lilinifundisha mengi na kunikutanisha na watu wengi, miongoni mwao ni Ruge Mutahaba. Nilikuwa ninamsikia Ruge, kwenye vyombo vya habari, lakini nilikuwa sijawahi kukutana naye hadi mwaka 2015. Ninakumbuka tulikuwa kwenye ofisi ya January Makamba, akaingia mtu mdogo mdogo na kukaa kwenye kiti. Sikufahamu ni nani. January Makamba, akashangaa kwamba hatufahamiani. Nilipotambulishwa kwake, nilicheka… yeye akasema “Ninajua kwa nini unacheka, ulitegemea Ruge, jitu, sasa unakutana na bwana mdogo”. Tulicheka sote. Kweli mimi nilikuwa na picha ya Ruge, jitu. Jinsi jina la Ruge, lilivyokuwa likitajwa, nilifikiri huyu ni “Jitu”. Kumbe ni Ruge, mwenye jina kubwa, mwili mdogo, lakini mambo yake makubwa!
Ninajua kabisa kuna watu wataiandika historia ya Ruge Mutahaba, watatufahamisha alizaliwa mwaka gani, alizaliwa wapi, alisoma wapi, amewaacha watoto wangapi, alifanya nini katika maisha yake haya mafupi sana. Wataandika juu ya THT, Fiesta na kamapeni nyingine nyingi kama Nyumba ni choo na nyingine nyingi. Ninajua kabisa kuna watu watamlilia Ruge, kwa unafiki na machozi ya mamba. Ninajua pia kuwa kuna wale watakao mlilia Ruge, kwa vile hatakuwepo tena kuwaelekeza, kuwafundisha na kuwasimamia ili wafanikiwe maishani.
Sote tunajua jinsi Ruge Mutahaba, alivyowainua wasanii wengi na kuhakikisha wanafanikiwa maishani. Amewasaidia kutengeneza majina makubwa; amewasindikiza kwenye uwanja wa mafaniniko bila wivu wala kijicho. Hata baada ya mafanikio aliendelea kuwahimiza wasibweteke. Tumeanza kuvisikia vilio vya “ Baba, baba umeondoka, ni nani atanihimiza kuendelea kuimba..?”. Ruge, alikuwa msingi na nguzo ya wasanii wengi hapa Tanzania.
Ninajua kuna wale ambao hawakufurahishwa na Ruge, wengine walifikiri anawatumia kujinufaisha yeye au anawanyanyasa na kuwatapeli. Pia wanasiasa waliopenda kumtumia Ruge, ili kujinufaisha na kutafuta “Kick” za kisiasa, watakuwa na namna yao ya kumlilia Ruge.
Ruge Mutahama,Watakusifia, watakupamba na kuyaazima maneno yote yanayoweza kuelezea sifa zako; uwezo wako mkubwa, ushauwishi wako na roho yako nzuri. Mabaya yako watayaweka kapuni. Kila mmoja atahakikisha ni rafiki yako mkubwa na amesikitika sana umeondoka mapema hata kama alitamani sana kuondoka kwako. Binadamu tuko hivyo, daima tunalia wakati tunacheka na tunacheka wakati tunalia.
Ninajua kabisa kwamba wewe ni binadamu kama binadamu wengine wote. Una kasoro zako kama binadamu, una mapungufu yako, una mazuri yako pia. Sijasimama hapa kuyataja mapunfugu yako, watayataja wengine wenye shida nayo, pia siko hapa kukusifia, kazi hiyo wataifanya wenye utamaduni wa kusifia kila kitu hadi maadui zao.
Nitakuwa tofauti! Nimesikia wosia wako, ni kututaka kuyasherehekea maisha yake! Huo ndio mwelekeo wa Tanzia hii! Ni bahati mbaya kabisa kwamba Ruge Mutahaba, umeondoka bila kuona kwa macho yako Tanzania, uliyoitamani. Tanzania yenye mshikamano na uzalendo, Tanzania ya vijana wanaojisimamia, wamejikomboa kifikra na kujitegemea kiuchumi, lakini wakishirikiana. Tanzania inayotanguliza utaifa badala ya kutanguliza vyama vya siasa, Tanzania inayotanguliza utanzania badala ya faida binafsi. Tanzania ya watanzania wote. Ulitamani kitu hiki, ninajua hivyo, maana jitihada zako zote ulizielekeza huko. Umeizunguka nchi nzima ukifundisha kwa vitendo, umeanzisha kampeni mbali mbali na kuelekeza kwa vitendo, umepandikiza mbegu ambayo ilikuwa bado kuchipuka na kuchanua.
Hivyo, ninatamani kulia na kusaga maneno. Ninatamani niongee na wewe Ruge Mutahaba: Je mlango umefungwa? Ji tumepotea njia au tusipotee njia? Ruge Mutahamba! Umetuacha njia panda? Umetuacha kwenye njia sahihi au tumepotea njia? Je wasanii wote uliowasaidia walikuelewa? Walichangia kuijenga Tanzania tuitakayo, Tanzania yenye mshikamano na uzalendo? Tanzania yenye kujaliana na kuchukuliana? Au waliishia kununua magari makubwa, kujenga majumba makubwa na kuvaa mikufu ya dhahabu? Nimemsikia Mpoto akisema kwamba alipopata fedha nyingi kama milioni 50, alitaka kununua gari, ukamkataza na kumshauri anunue shamba, hadi leo anakukumbuka kwa ushauri wako wenye busara. Je, wengine walikusikia? Kama walikushikia, wanaruhusiwa kuyasherehekea maisha yako… kama hawakusikia, walie na kusaga meno!
Ninaju wakati mwingine ulikuwa na misuguano na watu wenye majina makubwa; wasaniii na wanasiasa. Mara zote nimeshangaa jinsi ulivyoweza kutafuta upatanisho, mazungumzo na kumaliza tofauti hizo ambazo wakati mwingine zilikuwa ni kubwa kiasi cha kuwagusa watu wengi. Na hii haikukuvunja moyo wala kukutanisha tamaa, uliendelea kufanya kazi na watu walewale, maana ninafikiri uliamini kwamba Tanzani ni yetu sote, piga ua ni lazima tuiijenge wote hata kama wakati mwingine tunatofuatiana kimawazo.
Ninajua kwamba wewe una marafiki wengi wanasiasa. Mbali na wanasiasa hawa kutaka kukutumia wewe ili kufanikisha malengo yao ya kisiasa, walifahamu vizuri malengo yako? Walitambua kwamba wewe ulilenga kuwaunganisha vijana wote wa Tanzania, bila kuangalia itikadi za vyama? Ili vijana washikamane, wasaidiane na kuinuana katika maisha na hatimaye walijenga taifa letu la Tanzania?
Siku moja tulisafiri pamoja ukitokea Mwanza. Nilipokuuliza kama ulikuwa kwenye “Fiesta”, wewe ulisema, ulikuwa kwenye “Fursa”. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kusikia neno hili, kwamba “Fiesta” ni “Fursa”. Huu ni mtizamo mpana ambao kama ungefuatwa kwa ungalifu na umakini, ungelifikisha taifa letu mbali.
Hivyo kukulilia wewe haitoshi, kuyasherehekea maisha yako hakutoshi, tunalazimika kuyatekeleza yale uliyo yakusudia. Kuijenga Tanzania yenye mshikamano, Tanzania yenye uzaleno, Tanzania yenye vijana wanaoshirikiana na kuinuana kiuchumi, Tanzania yenye vijana wanaofundishana na kufikishiana ujummbe kupitia kwenye sanaa ya nyimbo na maigizo. Tanzania yenye vijana wanaojitambua.
Ruge Mutahaba, nitakuimbia kwa machozi na furaha, nitakuimbia wimbo wa kusherehekea uhai wako, wimbo wa ushindi na utukufu, wimbo mzuri, dunia nzima ikae kimya kuusikiliza na Mungu, mbinguni akitabasamu. Upumzike kwa amani.
Next Post Previous Post
Bukobawadau