Bukobawadau

WAZIRI UMMY AWAPONGEZA WAWEKEZAJI VIWANDA VYA DAWA -KIBAHA PWANI

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kiwanda cha Madawa cha Kairuki, kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

Msimamizi wa Kiwanda cha Madawa cha Kairuki Pharmaceutical Industrial Ltd (KPIL), Dk. Muganyizi Kairuki akitoa taarifa ya ujenzi wa kiwanda hicho kwa Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu

Mbunge wa Kibaha akitoa neno kwa wawekezaji wa Viwanda vya Dawa.

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema katika kila Sh. 100 ambayo Serikali inatumia kununua dawa nchini, Sh. 94 inapelekwa nje ya nchi kwa ajili ya ununuzi wa dawa hizo.
Waziri Ummy alisema hayo jana wilayani Kibaha, Pwani wakati wa ziara yake ya kutembelea na kuangali maendeleo ya ujenzi wa Viwanda vya dawa ambavyo ni Kampuni ya Kairuki Pharmaceutical Industrial Limited (KPIL) na Vista Pharma Ltd.

Alisema fedha hiyo inayokwenda nje kwa ajili ya ununuzi wa dawa ni kubwa na ili kuikoa ni muhumu kwa wawekezaji kuendelea kuwekeza nchini hasa katika ujenzi wa viwanda vikiwemo vya dawa na vifaa tiba ambavyo ndivyo vinapewa kipaumbele na serikali.
“Changamoto tunayopitia Serikali mbali na kwamba tunatumia fedha nyingi katika uagizaji wa dawa, bado dawa hizi zinachelewa kufika, Bohari ya Dawa (MSD) imekuwa ikiagiza dawa nje ya nchi na dawa hizo hukaa takribani zaidi ya miezi sita ndio zinaingia nchini, jambo hili ufanya upatikanaji wa dawa usiwe rahisi.
“Hivyo tunaposema upo umuhimu wa ujenzi wa viwanda vya dawa tunamaanisha,” alisema.

Alisema ujenzi wa viwanda nchini utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za uagizaji wa dawa hizo nje ya nchi, gharama za upatikanaji wa dawa nchini kushuka na kuokoa fedha zinazonunulia dawa hizo.
“Kati ya wadau 72 wa masuala ya afya nchini walioomba kujenga viwanda vya dawa hapa nchini, ni nane mpaka sasa ndio wameanza kujenga na kati ya hao sita viwanda vipo Kibaha.

Moja ya majengo ya ofisi katika kiwanda cha Vista Pharma

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, akiangalia ramani ya ujenzi wa Kiwanda cha Kairuki Pharmaceutical Industrial Limited (KPIL).

Kwa Upande wake, Msimamizi wa Kiwanda cha Kairuki, Dk.Mganyizi Kairuki, alisema kiwanda chao kinatarajia kuanza uzalishaji wa dawa za maumivu na nyingine aina 10 ambazo ni za maji ifikapo mwakani.
Alisema mbali na uzalishaji wa dawa, kiwanda hicho pindi kitakapokamilika kinatarajia kutoa ajira za moja kwa moja 200 na zisizo za moja kwa moja 1,000. “Zaidi ya Sh. Bilioni 38 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa kiwanda hiki fedha ambazo ni mikopo kutoka benki, hivyo tunazidi kuziomba baadhi ya benki kukopesha maana suala hili limekuwa ni changamoto,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya Bandari Pharmacy inayojenga kiwanda cha Vista Pharmacy, Churchill Katwaza, alisema kiwanda chao kinatarajia kuzalisha dawa sita ikiwemo ya kutuliza maumivu ya tumbo, kuongeza damu kwa wajawazito pamoja na inayotibu ushambulizi wa vidudu vya bakteria mwilini.
“Tutazalisha jumla ya vidonge milioni 702 kwa mwaka na takribani chupa milioni 32 za dawa ya maji zenye ujazo wa milimita 100,”alisema Katwaza.


Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Madawa cha Vista Pharm, Churchil Katwaza, akisoma taarifa za kiwanda hicho kwa Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Waziri akiagana na Msimamizi wa Kiwanda cha Kairuki, Dk.Mganyizi Kairuki. 








Next Post Previous Post
Bukobawadau