Bukobawadau

SOMA HII UNAWEZA KUJIFUNZA KITU KUTOKA KWA KIJANA LEVITH LEVELIAN MUUZA KARANGA MANISPAA YA BUKOBA

Inafikirisha sana na ni ngumu kuamini mpaka uamue kwa moyo wa dhati hasa kijana wa mkoa wa Kagera ambaye pengine umehitimu masomo yako iwe Elimu ya Msingi, Sekondari au Chuo Kikuu bado upo nyumbani unasubiria ajira na kulalama kuwa Serikali haijatoa ajira au unasubiri Makampuni makubwa na Mashirika binafsi yakuajili.
Ukisikiliza watu wengi waliofanikiwa na ni matajiri wakubwa duniani (hata Bukoba Wapo) wanaendesha makampuni makubwa ya biashara wanatoa ajira kwa wenzao wengi historia zao ukizisikiliza vizuri wanasema walianzia chini kabisa kwa biashara ndogo ndogo na baadae biashara zao ziliweza kukua kwasababu walithubutu, wakachapa kazi kwa nguvu, wakavumilia na kuweka aibu kando.
Wasomi wengi wanatufundisha juu ya ujasiliamali tena kwa kuthubutu kuanza na wazo dogo, kujikubali na kufanya kazi kwa bidii. Profesa Faustin Kamzora anasema jiamini kwa kile unachokifanya lakini pia kila siku ipitayo jitahidi kukiboresha ilimradi kinakuingizia kipato, pia anasema dunia inaenda kasi sana tumia simu yako (smart phone) kusoma mara kwa mara juu ya unachokifanya ili usipitwe na dunia inayoenda kasi kutokana na teknolojia.
Leo wewe kijana au mtu yeyote ambaye huna ajira hebu jifunze kwa huyu kijanaLevith Levelian ambaye nilikutana naye na kumtafiti kwa muda kidogo na nikapendezewa na stori yake ya maisha na anachokifanya pengine akili yako inaweza kufunguka kuanzia sasa ukaamua kujiajili na ukatajirika.
Levith Leveliani ni kijana wa umri wa miaka 26 mwenyeji wa Kashai Kilimanjaro Manispaa ya Bukoba ni mjasiliamali mdogo wa kuuza karanga za kutembeza mitaani. Kijana huyu nyumbani kwao anakozaliwa ni Kagondo Muhutwe Wilayani Muleba, alihitimu Elimu ya Msingi mwaka 2009 Shule ya Msingi Kagondo “B”.
Mwaka 2010 Levith alikuja Bukoba Manispaa kutafuta maisha ambapo alifikia kwa mama Aisha mwenyeji wa Kashai aliyemwajili kuuza vitumbua kwa kutembeza mitaani ambapo kwa siku alikuwa anauza vitumbua vya shilingi 7000/- hadi 8000/-. Levith alidumu katika ajira hiyo ya kuuza vitumbua kwa miezi mitatu na baadae akampata mwajili mwingine aliyemwajili kuuza (CDs) na kuchaji simu kibandani Kashai na kudumu na ajira hiyo kwa miaka miwili.
Levith wakati wote huo alikuwa akiishi kwa waajili wake lakini Mwezi Juni 2012 alifanya uamuzi wa kujiajili ambapo alipanga chumba kwa kodi ya shilingi 10,000/- kila mwezi na kununua bidhaa kama pipi, bisukuti, na sigara na kuanza kutembeza mitaani akiuza rejareja ambapo biashara hiyo aliifanya kwa miezi minne lakini hakufanikiwa na alifirisika kabisa.
Kijana Levith anasema alijipanga upya na kubuni biashara mpya ambapo alinunua kisanduku cha kuuzia karanga kwa shilingi 15,000/= na kununua kilo moja na nusu ya karanga kwa shilingi 3,750/- (kilo moja shilingi 2,500/-kwa wakati huo) na kuanza kutembeza karanga hizo katika mitaa na viunga vya mji wa Manispaa ya Bukoba na kujipatia kipato chake.
Kuanzia wakati huo kijana Levith akaanza kujulikana kama muuza karanga hadi mwaka 2014 alipokutana na mama mmoja aliyekuwa anafanya kazi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera aliyemuomba awe anamletea karanga kwaajili ya chai na kujiburudisha wakati akichapa kazi zake. Hapa ndipo biashara ya kijana huyu ilianza kupata mwangaza wa soko.
“Baada ya mama huyo kuonja karanga zangu aliniambia niwe namletea kila siku kwani alizisifia na kuniambia kuwa nazikaanga vizuri lakini pia akanipatia wateja wengine ambao walizipenda sana na kuanzia wakati huo nikaanza kuuza kilo tano hadi saba kwa siku kwa mtaji wa shilingi 12,500/- na kupata faida ya wastani wa shilingi 6,000/- kila siku kutoka kilo moja na nusu ya awali” Alieleza Kijana Levith
Hadi sasa kijana amejipatia soko la kudumu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera na anasema kuwa kutokana na biashara yake ya karanga kuwa na uhakika tayari amefanikiwa kuoa mke mwaka 2017 na tayari wana mtoto mmoja. Amehama katika chumba cha awali na kupanga chumba kipya kizuri zaidi cha shilingi 20,000/- kila mwezi.
Aidha, Levith anasema kuwa kutokana na biashara yake ya karanga tayari amejenga nyumba yake mwenyewe yenye vyumba 3 na sebule moja kijijini kwao Kagondo Muhutwe. Pia anaishukuru Serikali kwa kumtambua na kumpatia kitambulisho cha mjasiliamali mdogo ili akafanye biashara yake kwa uhuru zaidi.
Malengo yake ya mwaka huu 2019 ni kununua kiwanja mjini Bukoba ili aanze kujenga nyumba yake na kuachana na nyumba za kupanga, aidha, matarajio yake mengine ni kuanziasha duka la rejareja jambo ambalo analipenda pia kulifanya katika maisha yake lakini pia ikiwa ni pamoja na kuboresha biashara yake ya sasa ya kuuza karanga.
Wito wa kijana Levith kwa vijana wenzake ambao hawana ajira ni kuondokana na mitazamo potofu kuwa hakuna ajira wajipange kwa kuanza kidogo kidogo bila woga na aibu na wachape kazi kwa nguvu mafanikio watayapata tu vijiweni si mahala pazuri pa kupata mawazo ya kujenga.
Ewe kijana mwenzangu ushuhuda huu unaweza kukufungua macho na akili ukaanza na wazo dogo sana ambalo baadae utakuja kuwa utajiri wako, yaweza kuwa sekta ya kilimo, biashara, uvuvi, ufundi, na mengineyo mengi. Nimeona nikuletee stori hii unaweza ukajifunza kitu tukashirikiana kupunguza tatizo la ajira mkoani kwetu Kagera.
Na: Sylvester Raphael
Next Post Previous Post
Bukobawadau