Bukobawadau

BODABODA ALIMAARUFU ASEKDO MKOANI KAGERA MSHINDWE WENYEWE LAKINI MKUU WA MKOA TAYARI KAWASAFISHIA NJIA KAZI KWENU

Na: Sylvester Raphael
Badala ya kuwasukuma ndani kuwakimbiza kwasababu ya kutofuata sheria mbalimbali za usalama barabarani, kuwaona ni wahuni na kuwanyanganya vyombo vyao vya moto vya kutafutia riziki na kujipatia kipato waelimishe juu ya sheria zinazohusu kazi yao, wape elimu ya ujasiliamali, itambue kazi yao iwe rasmi ili kushirikiana nao katika kusukuma maendeleo ya mkoa mbele.
Hilo ni kundi kubwa ambalo limejiajili katika sekta ya usafirishaji wa abiria kwa njia ya pikipiki maarufu kama bodaboda au Asekdo mkoani Kagera ambapo vijana hawa hapo awali walikuwa wakitekeleza kazi yao ya kubeba abiria kwa tabu kweli kutokana na baadhi ya Askari wa Jeshi la Polisi kuwasumbua kwa kuwakamata hovyo kuwanyanganya bodaboda zao na kuwatoza faini kila mara zisizokuwa na mpangilio.
Baada ya kilio chao Bodaboda kumfikia Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti na kufanya nao kikao kwanza aliamua kuwa mlezi wa vijana hao na kuwaagiza Jeshi la Polisi Mkoani Kagera badala ya kuwabughudhi liwasimamie wafanye kazi zao kwa amani ikiwa ni pamoja na kuwapa mafunzo ya sheria za usalama barabarani ili vijana watekeleze ajira yao kwa amani na utulivu
Nia ya Mkuu wa Mkoa Gaguti ni kuwaona bodaboda wakifanya kazi zao na kujiingizia kipato bila kusumbuliwa na mtu yeyote. Ili kulitekeza hilo chini ya usimamizi wake Mkuu wa Mkoa aliwaagiza bodaboda wote kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wasajili vijiwe vyao ikiwa ni pamoja na kujisajili majina yao katika vijiwe hivyo ili kutambulika rasmi na Serikali ya mkoa.
Pili, ili wananchi ambao ni wateja wawaamini bodaboda Mkuu wa Mkoa alitoa viaksi mwanga (Reflectors) zenye namba mgogoni ili kila bodaboda atambulike kwa namba yake. Tatu Mkuu wa Mkoa Gaguti ili kuwaunganisha bodaboda ambalo ni kundi kubwa lililojiajili aliamua kuanzisha ligi ijulikanayo kama JPM BODABODA CUP KAGERA 2019 iliyoanza rasmi tarehe 30 Machi, 2019.
Ligi ya JPM BODABODA CUP KAGERA 2019 inahusisha timu za mpira wa miguu 16 (Timu za vijiwe 16) zilizoundwa na kupendekezwa na Bodaboda wenyewe ambapo mshindi wa kwanza anatarajiwa kuzawadiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera shilingi milioni 3, Mshindi wa pili Milioni 2, na mshindi wa tatu Milioni 1 ikiwa ni pamoja na makombe kwa mshindi wa kwanza wapili na watatu.
Lengo kuu la ligi JPM BODABODA CUP KAGERA 2019 anasema Mkuu wa Mkoa Gaguti kuwa ni kuimarisha vikundi vya Bodaboda ili viweze kuwa na uwezo wa kuwa ujasiliamali tofauti na kazi ya bodaboda ili ikitokea kijana anapata matatizo mfano ajali na kukaa mda mrefu bila kuendesha bodaboda awe na kipato ambacho hakitahitaji kuendesha bodaboda. Lakini pia kuinua vipaji kwa makundi yaliyosaulika na kuwa na timu ya mpira yenye vipaji kutoka katika kundi hilo.
 Katika kuboresha hilo Mkuu wa Mkoa Gaguti tayari ametenga Bodaboda mpya tano kwa vikundi vitakavyoonekana ni bora zaidi katika kufuata sheria za usalama barabarani chini ya usimamizi wa Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani na bodaboda hiyo itakuwa mali ya kikundi au kijiwe hicho. Vikundi hivyo vitapatiwa bodaboda kila kimoja ili bodaboda hiyo iwe ya kikundi na kukiingizia mapato.
Manispaa ya Bukoba tayari imetenga shilingi milioni 20 kwaajili ya mkopo usiokuwa na riba kwa vijana hao ili wakakope na kuimarisha vikundi vyao na maisha yao kwa ujumla. Lengo kuu la kuliangalia kundi hili la bodaboda mkoani Kagera kuhakikisha kuwa vijana wanajiajili bila bughudha lakini pia watekeleze ajira yao kwa kufauata sheria za nchi kwa kuwajibishana wao wenyewe kwa wale ambao hawatafuata sheria za usalama barabarani badala ya Jeshi la Polisi kuwawajibisha.
Mwisho kama kiongozi wa Mkoa Mhe. Gaguti anasema nia yake ni kuona vijana wanashamiri katika kazi zao kwa kutekeleza sheria na kuzitii bila shuruti lakini pia Bodaboda wa Kagera kuwa mfano kwa nchi nzima kama usafirishaji huo ulivyoanzia mkoani Kagera.
Tayari hamasa ni kubwa mno kwa wakazi wa Bukoba kushuhudia mechi za mpambano wa bodaboda kila siku wakishuhudia JPM BODABODA CUP KAGERA 2019 Je nani anatanyakua milioni 3? Je ni kijiwe gani kitanyakua bodaboda mpya? Kazi kwenu ASEKDO BUKOBA
Next Post Previous Post
Bukobawadau