Bukobawadau

KAGERA KUIBUA VIPAJI VIPYA KATIKA MICHEZO MBALIMBALI UMISETA 2019 YAFUNGULIWA RASMI KUUNDA TIMU BORA YA KUNYAKUA USHINDI KITAIFA MTWARA.

 Na: Sylvester Raphael
Mashindano ya Michezo kwa wananfunzi wa shule za Sekondari UMISETA Mkoa Kagera yafunguliwa rasmi ili kuibua vipaji katika michezo mbalimbali na kuunda timu ya mkoa itakayokwenda kuuwakilisha mkoa katika mashindano hayo ngazi ya Taifa mkoani Mtwara.
Akifungua mashindano hayo kwaniaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Bw. Isaya Tendega Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji aliwataka wananfunzi wanaounda kambi hiyo kucheza kwa nidhamu kubwa na kuonesha vipaji vyao wakifuata maekezo ya walimu wao ili kuunda timu imara na bora itakayoleta ushindani katika mashindano hayo Kitaifa.
Bw. Tendega aliwataka wanafunzi hao kuwa wazalendo, kwa kuwa wakakamavu, waadilifu kuwa na nidhamu pia uzalendo wanaposhiriki mashindano hayo kwani michezo si ugomvi bali ni upendo na kucheza kwa upendo ndipo kipaji cha mchezaji huonekana vyema zaidi. Pia aliwaasa waamuzi wa michezo yote kuamua bila upendeleo ili kupata vipaji vinavyolengwa vitakavyouwakilisha mkoa vyema kitaifa.
 Aidha, katika hotuba yake Katibu Tawala wa Mkoa Profesa Faustin Kamzora aliwaagiza Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha idara za michezo katika Halmashauri zao zinawezeshwa kwa vifaa na fedha ili kuendeshea michezo na kukuza vipaji katika mkoa wa Kagera kwani hivi sasa michezo ni ajira.
“Michezo imewasaidia vijana wengi kuepukana na mdawa ya kulevya kama bangi, mirungi, cocaine na mengineyo lazima tuitilie mkazo sana ili vijana wetu wasiharibikiwe. Pili kumbukeni kuwa Michezo ni ajira mfano katika mkoa wetu tunaye mwamuzi wa mpira wa miguu tena mama anachezesha liku ligi kuu ya Tanzania ni kwasababu aliichukulia michezo kwa kipaumbele na amepata ajira ya kudumu sasa.” Alisisitiza Bw. Tendega kwaniaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Kagera.
Aidha, Bw. Kepha Elias Afisa Michezo Mkoa wa Kagera ambaye ni meneja wa kambi ya UMISETA katika Shule ya Sekondari Nyakato Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba alisema kuwa kuna jumla ya wananfunzi wanamichezo 640 wavulana wakiwa 341 na wasichana 306 na wanamichezo hao wanashiriki katika michezo ya soka, fani za ndani, kwaya, mpira wa wavu, mpira wa pete, mpira wa mikono na riadha.
Naye Bw. Mbaraka Maya aliyemwakilisha Afisa Elimu Mkoa katika ufunguzi huo wa mashindano ya UMISETA mkoa wa Kagera alisema kuwa Maafisa Elimu wote wa Wilaya wapo katika kambi hiyo ya Shule ya Sekondari Nyakato kusimamia nidhamu ya wanafunzi wanamichezo ili kupata timu bora ya mashindano hayo itakayoleta changamoto katika michezo mbalimbali Kitafa mkoani Mtwara.
Ikumbukwe kuwa Mashindano ya michezo kwa wanafunzi wa Shule za Sekondari UMISETA na Shule za Msingi UMITASHUMTA yaliwahi kusitishwa mwaka 2000 na Waziri aliyekuwa na dhamana ya Michezo wakati huo wa Awamu ya Tatu Mhe. Joseph Mungai na yalirejeshwa kwa majaribio mwaka 2007 na Mhe. Magreth Sitta akiwa waziri mwenye dhamana ya michezo wakati huo.
 Mashindano hayo kwa shule za Sekondari UMISETA na Msingi UMITASHUMTA yaliporejeshwa tena mwaka 2007 na yalifanyika majaribio kwa Mikoa mitatu tu ya Dar es Salaam, Morogoro na Tanga na yalifanyikia Kibaha Mkoani Pwani. Aidha, Serikali iliamua kuyarejesha rasmi mashindano hayo mwaka 2009 kwa waraka namba 1 wa mwaka 2009.
Katika Mkoa wa Kagera Mashindano ya wanafunzi kwa shule za Sekondari UMISETA yanafanyika katika Shule ya Sekondari Nyakato Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba ambapo yalianza Mei 25, 2019 na yanatarajia kukamilika Juni 7, 2019.
Next Post Previous Post
Bukobawadau