Bukobawadau

WAZIRI KALEMANI AFURAHISHWA NA UTAYARI WA WADAU MKOANI KAGERA KUCHANGAMKIA FURSA ZITAKAZOPATIKANA KUTOKANA NA UJENZI WA BOMBA LA MAFUTA GHAFI

Waziri wa Nishati Medard Kalemani afurahishwa na utayari wa wadau na wananchi wa mkoa wa Kagera katika kuchangamkia fursa na ajira wakati mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga kilometa 1445 pale utakapokuwa umeanza ujenzi wake.
Waziri Kalemani aliyasema hayo Juni Mosi 2019 katika Ukumbi wa Hoteli ya ELCT Bukoba akifungua na kuongoza kongamano la wadau wa mkoa wa Kagera kuhusu mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka nchini Uganda hadi Tanga Tanzania ambapo aliwaeleza wadau hao fursa mbalimbali za mradi huo na ni hatua gani mradi umefikia kabla ya kuanza kwasasa.
Waziri Kalemani alisema kwa kuwa Mkoa wa Kagera ndipo bomba la mafuta kutoka nchini Uganda litaaingilia Tanzania Wizara pamoja na wadau wa ujenzi wa mradi huo kwapamoja walipanga na kuamua kuleta kongamano la wadau Kagera ili wananchi waelewe vizuri ni namna gani watanufaika na kwasasa mradi upo katika hatua gani ili elimu iwafikie wananchi kule bomba litakapopita.
“Nimefurahishwa na utayari wa mkoa kwa namna mlivyochangia mawazo yenu unaweza kuona utayari wa kushiriki katika mradi huu mkubwa wa kimataifa, mradi huu unatarajia kuajiri watu 10,000 wakati wa ujenzi na watu 20,000 wakati ukikamilika lakini naona Kagera tayari mmeulewa mradi vizuri na kati ya ajira hizo lazima mhakikishe ajira na fursa za wazabuni mbalimbali zinabaki hapa.” Alisistiza Waziri Kalemani
Mradi wa Bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga Tanzania utakuwa na urefu wa kilometa 1445 na asilimia 80% ya kilometa hizo zitakuwa upande wa Tanzania ambazo ni kilometa 1147 na asilimia 20% zinazobaki zitakuwa upande wa Uganda ambapo bomba hilo litapita katika mikoa minane ya Tanzania, Wilaya 24 na Kata 134.
Mikoa hiyo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma Manyara na Tanga aidha, katika Mkoa wa Kagera bomba litapita katika Wilaya za Missenyi, Bukoba (vijijini), Muleba na Biharamulo. Pia litapita katika Kata 20 za Mkoa wa Kagera, Vijiji 34, na Vitongoji 117.
Mafuta ghafi yaligunduliwa Ziwa Albert nchini Uganda na kuonekana kuna mapipa bilioni 6.5 na inatarajiwa mapipa bilioni 1.7 kuuzwa nchi za nje kupitia bomba litakalopita nchini Tanzania na gharama ya ujenzi wa mradi mzima wa bomba la mafuta kutoka Hoima hadi Chongoleani mpaka kukamilika utagharimu jumla ya Dola bilioni 3.5 za Kimarekani (3.5 billion USD).
Bomba la mafuta ghafi litakuwa linasafirisha mapipa ya mafuta 216,000 kwa siku na kila pipa moja litakuwa linalipiwa kodi ya dola 12.5 za Kimarekani ukiachilia mbali na kodi nyinginezo zitakazokuwa zinalipwa kwa nchi ya Tanzania. Makampuni makubwa matatu ndiyo yatatekeleza mradi huo nayo ni TOTAL kutoka Uingereza, TULLOW kutoka Ufaransa na CNOOC kutoka nchini China.
Katika mradi mzima wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi vitajengwa vituo sita vya kusukuma mafuta viwili upande wa Uganda na vinne upande wa Tanzania na kati ya vituo vinne vitakavyojengwa Tanzania kituo kimoja kitajengwa Kyaka Wilayani Missenyi Mkoani Kagera, kingine kitajengwa mkoani Singida na viwili vitajengwa mkoani Tanga.
Pia katika mradi huo zitajengwa kambi 12 za wafanyakazi na yadi 10 za kuhifadhia mabomba, kati ya kambi 12 zitakazojengwa kambi 2 zitajengwa mkoani Kagera katika Wilaya za Missenyi na Muleba ambapo wananchi watakaokuwa karibu na kambi hizo watanufaika kwa kupimiwa ardhi katika maeneo yao, kuunganishiwa umeme kwa vijiji ambavyo vitakuwa havijapata umeme pia na fursa mbalimbali kama kufanya biashara.
Waziri Kalemani aliwahakikishia wadau wa kongamano la bomba la mafuta mkoani Kagera kuwa Serikali ya Tanzania na Serikali ya Uganda zimefikia asilimia 80% ya majadiliano ya utekelezaji wa mradi tangu kusainiwa mkataba wa makubaliano Mei 26, 2017 na mara baada ya majadiliano hayo kukamilika kwa asilimia 100% ujenzi wa bomba unatarajia kuanza Septemba 2019 na muda wa utekelezaji mradi hadi kukamilika utakuwa miaka mitatu.
Vilevile Waziri Kalemani alisema kuwa wananchi waliotathminiwa mali zao kupisha bomba la mafuta wataanza kupatiwa taarifa za tathmini zao ni kiasi gani watalipwa kuanzia wiki ya pili ya mwezi huu wa Juni 2019. Jumla ya wananchi 10,000 walitathminiwa katika mikoa minane na kwa mkoa wa Kagera ni wananchi 2017 ndiyo watapisha bomba la mafuta ghafi.
Katika hatua nyingine wadau wa kongamano walimshauri Waziri Kalemani kuwa mradi uzingatie kutoa kipaumbele kwa wazawa (Local Content) ili waweze kunufaika na mradi huo ambapo Profesa Anna Tibaijuka Mbunge wa Muleba Kusini alimshauri Waziri kuangalia namna ya kupata ufadhili wa elimu ili Watanzania wakasome masuala ya mafuta kuliko kuendelea kuwa walinzi tu bali na wataalam wapatikae ukizingatia mradi ni wa muda mrefu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti akifunga kongamano la wadau wa bomba la mafuta alimshukuru Waziri Kalemani kwa kuleta kongamano hilo mkoani Kagera kwani ndiyo mkoa ambako bomba linapoingilia nchini Tanzania. Pia alitoa ushauri kwa wadau kuwa tayari kwa vigezo katika ajira na kujipanga kimtaji ili fursa zitakapotangazwa wasishindwe kutokana na ushindani kutoka nje ya mkoa.
 Taswira wakati mjadala ukiendelea ukumbini
 Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu pichani
 #Bukoba Na: Sylvester Raphael


Next Post Previous Post
Bukobawadau