Bukobawadau

PROFESA KAMUZORA ASHAURI SEMINARI YA KATOKE KUANZISHA MASOMO YA PROGRAMU ZA TALAKILISHI ILI KUENDANA NA DUNIA YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA

• Wahitimu Kidato cha Sita 24 Sita Tu Kuendelea na Wito wa Upadre
Na: Sylvester Raphael
Profesa Faustin Kamuzora Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera aushauri uongozi wa Seminari ya Mtakatifu Karoli Lwanga Katoke alikosoma Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kuanzisha maabara ya Talakilishi (Computer Labaratory) na kutoa elimu juu ya ubunifu na uanzishwaji wa programu (software) mbalimbali badala ya kujikita kwenye matumizi ya talakilishi tu (yaani namna ya kutumia Computa tu).
Profesa Kamuzora alitoa ushauri huo katika maafali ya 29 ya kidato cha sita katika Seminari ya Katoke Wilayani Biharamulo alipokuwa mgeni rasmi Mei 18, 2019 ambapo alisistiza kuwa Seminari hiyo imekuwa na mchango mkubwa kwa taifa la Tanzania ni lazima iendane na ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia mfano kuanzisha program za wa watu kuweka ulinzi majumbani mwao kwa kutumia simu au kuwasha na kuzima umeme ukiwa mbali na nyumbani.
 Katika mahafali hayo Profesa Kamuzora aliwaasa wahitimu 24 wa kidato cha sita pamoja na wananfunzi wanaobaki kuchapa kazi kwa bidii sana kuheshimu misingi ya maadili waliyofundishwa na walimu wao ili kuyafikia mafanikio kama wanafunzi waliotangulia katika Seminari hiyo walivyopata mafanikio katika sehemu mbalimbali ndani na je ya nchi.
“Naomba kujitolea mfano mimi mwenyewe ambaye nilipita katika Seminari hii ya Katoke mwaka 1977 hadi 1980 kwa kufuata malezi na maadili ya Seminari hii nimeweza kusoma hadi ngazi za juu sana na kuwa Profesa na nimefanya kazi sehemu mbalimbali lakini siri kubwa ni malezi na maadili niliyoyapata hapa. Pia Mhe. Rais Magufuli alipita hapa sasa unaweza kuona namna ya utendaji kazi wake ni kutokana na alichokipata hapa.” Alitoa ushuhuda Profesa Kamuzora.
Katika mahubiri yake wakati wa ibada takatifu ya kuwapongeza wanafunzi 24 wahitimu wa kidato cha sita Padre Fortunatus Bijura alisema kuwa ibada hiyo iliadhimishwa ikiwa ni ibada ya Mtakatifu Joseph mchapakazi ili kuwakumbusha vijana hao 24 pamoja na wanafunzi wengine wanaosoma katika Seminari hiyo kuwa kuchapa kazi ndiyo msingi wa mafanikio ya kila kitu katika maisha ya mwanadamu.
Padre Bijura pia aliwapongeza na kuwakumbusha wahitimu wa kidato cha sita katika ibada hiyo kuwa Mungu hujua wito wa kila mtu kabla hajazaliwa na kumaliza kidato cha sita ndiyo mwanzo wa wito wa upadre kwani baada ya hapo kuna miaka minane au tisa mpaka mtu awe padre. Wanafunzi walitakiwa kuchapa kazi kwa bidii hasa katika masomo yao na kuzingatia misingi ya maadili waliofunzwa katika Seminari hiyo.
 Padre Bijura pia aliwapongeza na kuwakumbusha wahitimu wa kidato cha sita katika ibada hiyo kuwa Mungu hujua wito wa kila mtu kabla hajazaliwa na kumaliza kidato cha sita ndiyo mwanzo wa wito wa upadre kwani baada ya hapo kuna miaka minane au tisa mpaka mtu awe padre. Wanafunzi walitakiwa kuchapa kazi kwa bidii hasa katika masomo yao na kuzingatia misingi ya maadili waliofunzwa katika Seminari hiyo.
“Maisha si starehe tu, sisi Watanzania bado tupo nyuma sana katika kuchapa kazi nitatoa mfano kwa wenzetu Wajerumani na Wamarekani hawa wanachapa sana kazi, wanakula sana na wanakunywa bia sana lakini wanaheshimu sana muda wao wa kupumzika. Lakini hapa Tanzania utawasikia vijana wakisema hebu twende kijiweni kupoteza muda kidogo, sijui muda huo wanautoa wapi.” Alisisitiza Padre Bijura ambaye ni mwalimu wa somo la Kiingereza Katika Seminari ya Katoke
Padre Bijura alimalizia mahubiri yake kwa kuwaasa vijana 24 wahitimu wa kidato cha sita kwa kuwataka kuwa mfano bora wa kuchapa kazi na wale ambao walichagua kutoendelea na wito wa upadre kuwa mabalozi wema uraiani kwa kuchapa kazi, pia wakitunza muda wao vizuri na kutokuchagua kazi bali kuthamini na kuipenda kazi (Sense of Belonging) lakini kazi hiyo isiwafanye wakamsahau Mungu.
Kwa upande mwingine Padre Jovine Bampabula ambaye ni Padre mlezi wa wanafunzi wa Seminari ya Katoke lakini pia alisoma katika Seminari hiyo kuanzia mwaka 1975 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akihojiwa juu ya Seminari hiyo kuzalisha viongozi bora alisema kuwa ni kutokana na malezi na maadili yanatolewa katika Seminari hiyo ya Katoke.
Seminari hii inazalisha Mapadre na wataalam wengine ambao huja kuwa watu wakubwa katika fani mbalimbali kwenye taifa letu na nje ya nchi. Mfano mimi nilisoma na Rais Magufuli tangu mwaka 1975 hapa mimi nilipata upadre yeye sasa ni Rais wa nchi, watu wengi wanashangaa ujasiri wa kutoa maamuzi na kupambana na Mafisadi lakini mimi sishangai kwani najua kuwa ujasiri ule ni kutokana na maadili na malezi bora aliyoyapata kutoka katika Seminari yetu hii ya Katoke.
Wafanyakazi katika shamba la Bwana ni wengi lakini Wateule ni wachache; Wanafunzi waliohitimu kidato cha Sita Seminari ya Katoke mwaka 2019 jumla ni 24 lakini walianza kidato cha tano wakiwa 27 katika mahafali yao ya kuhitimu Mkuu wa Seminari hiyo Padre Datius Rwegoshora alisema kuwa wanafunzi ambao walikuwa tayari wamejitafakari na kuamua kuendelea na wito wa upadre kati ya 24 ni sita tu ambao walipewa barua kuendelea na wito na kuitwa Mafrateli kuanzia siku hiyo.
Tuwaombee vijana hawa ili waifikie ndoto yao ya kuwa wachungaji wa Kondoo wa Bwana na kuhudumu katika shamba la Bwana. Seminari ya Mtakatifu Karoli Lwanga Katoke ilianzishwa mwaka 1964 Wilayani Biharamulo Mkoani Kagera ikiwa chini ya Jimbo Katoriki la Rurenge.
Next Post Previous Post
Bukobawadau