USICHUKULIE POA NYUMBA NI CHOO KUZINDULIWA KANDA YA ZIWA MKOANI KAGERA KUPAMBWA NA MRISHO MPOTO PAMOJA NA FAINALI ZA JPM BODABODA CUP 2019
Na: Sylvester Raphael
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuzindua Kampeini ya Kitaifa ya Usafi wa Mazingira yenye kauli mbiu isemayo “Usichukulie Poa, Nyumba ni Choo” katika mkoa wa Kagera Mei 25, 2019.
Akitoa ufafanuzi wa Kampeini ya “Usichukulie Poa, Nyumba ni Choo” Mkuu wa Mkoa Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti katika mkutano na vyombo vya habari alisema kuwa anaishukuru Serikali kuamua kufanya uzinduzi wa kampeini hiyo kwa Kanda ya Ziwa katika Mkoa wa Kagera ili kuhamasisha wananchi kujenga vyoo bora katika ngazi ya kaya na taasisi.
Kabla ya Kampeini ya Usichukulie Poa, Nyumba ni Choo’ kuanza nchini mwaka 2012 katika mkoa wa Kagera asilimia 35 ya kaya hazikuwa na vyoo kabisa ambapo vyoo bora ilikuwa ni asilimia 20% tu. Lakini kutokana na juhudi za mkoa hasa kupitia idara ya Afya kuhamasisha wananchi na kufanya ukaguzi wa kaya kwa kaya hadi sasa kaya zisizokuwa na vyoo zimepungua kutoka asilimia 35% hadi asilimia 5% tu.
Aidha, vyoo bora katika kaya mkoani Kagera vimeongezeka kutoka asilimia 20% hadi asilimia 55% na lengo ni kuhakikisha ifikapo Juni 2021 angalau asilimia 80% ya vyoo bora iwe imefikiwa katika . Vilevile Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kuwa mkoa umejipanga katika kipindi cha miezi mitatu kufikia Agosti 2019 kila kaya lazima iwe na choo na kukitumia ili kuondoa asilimia 5% ya kaya ambazo hazina vyoo kabisa kwa sasa.
Pia kwa kunesha mfano Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kuwa uhamasishaji wa vyoo bora unajikita kwa wananchi tu lakini taasisi mbalimbali za Serikali na zisizokuwa za Serikali zinasaulika na kwa kulitambua hilo ndiyo maana yeye Mkuu wa Mkoa akishirikiana na wadau mbalimbali aliamua kujenga choo bora katika uwanja wa Kaitaba kuzikumbusha taasisi mbalimbali kuwa nazo zinatakiwa kuwa na vyoo bora katika maeneo yao.
Vilevile Mkuu wa Mkoa Gaguti alikemea tabia ya kujisaidia ovyo ijulikanayo kama kuchimba dawa kwa wasafiri na madereva wa vyombo vya moto katika barabara kuu za Bukoba hadi nyakanazi na Bukoba hadi Mtukula kuwa kwa sasa hakuna haja ya kusingizia kuwa hakuna vyoo na kujisaidia hovyo na kuchafua mazingira wakati kuna maeneo yenye huduma za vyoo bora vya kujisaidia.
“Naagiza Wakuu wote wa Wilaya katika Mkoa wa Kagera kuhakikisha wanasimamia uchafuzi huu wa mazingira ili kuzuia kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza kama kuhara na kuhara damu, kipindupindu na minyooo.” Aliagiza Mkuu wa Mkoa Gaguti.
Naye Bw. Anyikite Mwakitalima mwakilishi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika mkutano huo wa Mkuu wa Mkoa na Waandishi wa Habari alisema kuwa wakati kampeini ya “Usichukulie Poa, Nyumba ni Choo” inaanza mwaka 2012 kitaifa kaya ambazo hazikuwa na vyoo bora zilikuwa milioni 1.4 lakini hadi kufikia sasa kutokana na kampeini hiyo takwimu hizoo zimeshuka hadi kufikia kaya elfu 70,000 tu nchini.
Naye Msanii Maarufu wa kughani mashairi Mrisho Mpoto maarufu kama Mjomba alisema kuwa katika mkoa wa Kagera mkoa wenye watu wanaojipenda, mkoa wenye wasomi wa kutosha haamini kuwa asilimia 5% ya kaya hazina vyoo na kusisitiza kuwa pengine hizo ni takwimu za miaka mingi iliyopita.
Mrisho Mpoto alisema kuwa labda angependa kuona mwenyewe kama ni kweli wakati akifanya uhamasishaji katika Wilaya zote za mkoa wa Kagera kwenye kampeini ya “Usichukulie Poa, Nyumba ni Choo”.
Kampeini ya “Usichukulie Poa, Nyumba ni Choo” itazinduliwa rasmi Mei 25, 2019 katika uwanja wa Kaitaba Manispaa ya Bukoba ambapo uzinduzi huo utapambwa na Fainali ya mechi ya mpira wa miguu ya kombe la John Pombe Magufuli (JPM BODABODA CUP 2019) ambapo ligi hiyo iliyoanzishwa Machi 30, 2019 na kufadhiliwa na Mkuu wa Mkoa Gaguti na kuwahusisha vijana waendesha Bodaboda katika Manispaa ya Bukoba ili kuwaleta pamoja na kuwapa elimu juu ya ujasiliamali.
Katika Fainali hizo mshindi wa kwanza atanyakua zawadi ya shilingi milioni tatu pia na zawadi nyingine nyingi zitatolewa kwa washiriki wananchi wa mkoa wa Kagera hasa Manispaa ya Bukoba wanakaribishwa kushiriki katika uzinduzi huo utakaopambwa pia Msanii Maarufu Mrisho Mpoto (Mjomba).