Bukobawadau

MKUU WA MKOA WA KAGERA KUWATIA HASIRA WAFANYABIASHARA WA MIPAKANI KUCHANGAMKIA FURSA ZA NCHI JIRANI

• Soko la Tanzania lipo Rwanda ardhi yao haiongezeki watu wanaongezeka – Balozi Mangu
Na: Sylvester Raphael
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti aweka mkakati kabambe wa kuwatia hasira wafanyabiashara wa mkoa wake kutambua na kuzitumia fursa za kufanya biashara na nchi jirani za Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambazo bado hatumiki ipasavyo katika kuinua uchumi wa wa Mkoa na Tanzania kwa ujumla.
Mkuu wa Mkoa Gaguti alionesha nia na matamanio yake hayo baada ya kufanya kikao cha wadau wa Biashara Mkoani Kagera pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Rwanda Mhe. Ernest Mangu ili kujadili fursa zinazopatikana nchini Rwanda na Wafanyabiashara wa Tanzania hasa wa Mkoa wa Kagera wanaweza kuzitumiaje fursa hizo kufanya baiashara.
Katika kikao hicho cha wadau wa biashara kilichofanyika Wilayani Ngara Julai 7, 2019 Mkuu wa Mkoa Gaguti baada ya kusikiliza kwa umakini wasilisho la Balozi Mangu kuhusu fursa za biashara zinazopatikana nchini Rwanda pia na maoni ya wafanyabiashara wa mpakani hasa Rusumo na Kabanga alisema kuwa haoni mwamko au hasira za wafanyabiashara wa upande wa Tanzania hasa Kagera kunuia kufanya biashara ya kweli na jirani zetu Wanyarwanda.
“Nakaribia kumaliza mwaka katika nafasi yangu ya ukuu wa Mkoa lakini sijawahi kuona wafanyabiashara wameleta kero kwangu inayohusu namna wao wanavyofanya biashara au vikwazo vinavowakwaza bali napokea kero za migogoro tu ofisini kwangu sioni kabisa hasira ya wafanyabiashara wetu kutaka kutumia fursa za mkoa huu kupakana na nchi hizi sana sana nimesikiliza maoni yao hapa walio wengi si wafanyabiashara bali madalali tu.” Alisisitiza Mkuu wa Mkoa Gaguti.
Balozi wa Tanzania nchini Rwanda Ernest Mangu akitaja fursa za biashara ambazo hazijawahi kutumika ipasavyo na Watanzania alisema kuwa alipoteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Rwanda jambo la kwanza kulifanya lilikuwa ni kutembelea mipaka yote ya Rwanda kuona biashara zinafanyikaje lakini katika mipaka yote mpaka wa Rusumo ndiyo umedorora sana na haufanyi biashara kama mipaka mingine ilivyo.
Balozi Mangu alisema katika nchi ya Rwanda kuna soko kubwa la Dagaa, Samaki, Ndizi, Mchele, mahindi, Mbogamboga, Saruji pamoja na bidhaa nyinginezo za viwandani. Ukiondoa saruji bidhaa zilizotajwa zinapatikana mkoa wa Kagera na mikoa ya jirani jambo ambalo lingewafanya wafanyabiashara wa Kagera na mikoa jirani kutumia fursa ya uhuhitaji huo kufanya biashara na Wanyarwanda pia na nchi ya Congo kwani kutoka Kagera kwenda Congo ni Kilometa 350 hadi 400 tu.
“Nchi ya Rwanda ina milima na mabonde na kwasasa ina wingi wa watu kuliko ardhi iliyopo kwahiyo wanahitaji chakula hasa ndizi na ndizi hizo zinalimwa hapa Kagera lakini bado sijaona wafanyabiashara wanaojishughulisha na biashara ya ndizi kwenda Rwanda. Pili, Mchele wa Tanzania unapendwa sana na Wanyarwanda lakini pia kuna soko Congo bado Watanzania hatujalichangamkia soko hilo bali Wanyarwanda wenyewe ndiyo wanafanyabiashara.” Alifafanua Balozi Mangu
Balozi Mangu alishauri Halmashauri za Wilaya za mipakani kwa kushirikiana na Wafanyabiashara kujenga maghara ya bidhaa mbalimbali ili bidhaa zinazotakiwa na nchi jirani zipatikane karibu na mipaka kuliko kuzifuata mbali ndani ya nchi mfano Saruji Mtwara, Mchele mpaka Kahama Shinyanga au Mwanza na bidhaa nyinginezo mpaka Kariakoo Dar es Salaam.
Aidha, Balozi Mangu alishauri kuanzishwa kwa magulio au masoko makubwa karibu na mipaka ambapo katika masoko au magulio hayo kila bidhaa ipatikane ili majirani waweza kuwa wanavuka na kununua bidhaa hizo bila kuzifuata mbali na mpaka. “Kwasasa tangu Rwanada ifunge mpaka wake na Uganda Serikali ilielekeza wazi wananchi wake kuwa bidhaa zote wanazozitaka wazipate Tanzania, hilo ni soko kwetu sasa. Alisisitiza Balozi Mangu.
Ili kuhakikisha fursa za biashara zilizopo nchini Rwanda zinachangamkiwa na Watanzania hasa Wafanyabiashara wa Mkoa wa Kagera Kikao hicho cha wadau wa Biashara kiliweka mkakati wa muda mfupi wa maazimio makubwa sita kuhakikisha fursa hizo zinachangamkiwa kisawasawa kama ifuatavyo:
Kwanza ndani ya wiki mbili toka siku ya kikao Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoani Kagera (TRA) kwa kushirikiana na Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) pamoja na Maafisa Biashara wa Wilaya na Mkoa wafanye usajiri wa wafanyabiashara za mipakani wote na si madalari ili kujua ni biashara gani wanafanya ili kusaidiwa.
Pili, ndani ya mwezi mmoja TRA Kagera waandae kikao kikubwa cha wafanyabiashara wote ili kutoa elimu ya biashara ya mipakani ikiwa ni pamoja na Ubalozi wa Tanzania Nchini Rwanda kualikwa kushiriki kutoa elimu juu ya fursa za Kibiashara zinazopatika nchini Rwanda.
Tatu, ndani ya Mwezi mmoja kiandaliwe kikao cha ujirani mwema kati ya Mkoa wa Kagera na Mkoa wa Jirani wa Rwanda ili kuzungumza na kuweka mikakati ya pamoja ya namna bora wafanyabiashara wa mikoa hiyo wanavyoweza kushirikaiana katika biashara.
Nne, Maafisa Biashara wakishirikiana na Wakuu wa Wilaya wafanye utambuzi wa maeneo ya kufanyia biashara mfano kama mfanyabiashara anataka dagaa azipate wapi na sikwenda moja kwa moaj kwa mvuvi au kama ni ndizi asiende moja kwa moja kwa mkulima bali pawepo na soko au eneo anapoweza kupata bidhaa hizo.
Mwisho Halmashauri za Wilaya pamoja na Mkoa kuwa na mpango Mkakati wa kuboresha masoko ya mipakani ambayo tayari yalikuwa yameanza kujengwa mfano soko la Nkwenda na Murongo Wilayani Kyerwa pamoja na soko la Kabanga Wilayani Ngara.
Mara baada ya kikao hicho wafanyabiashara waliohudhuria walimshukuru Mkuu wa Mkoa Gaguti kwa kuwakutanisha na Balozi wa Tanzania nchini Rwanda Ernest Mangu na kuwafungua macho ya kufanya biashara pia na kuwajengea uwezo wa namna gani wanawezaje kulifikia soko la Rwanda wakiwa wafanyabiashara wa Tanzania.

Next Post Previous Post
Bukobawadau