Bukobawadau

SERIKALI YAAHIDI UJENZI WA STENDI YA KISASA BUKOBA MJINI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa stendi ya kisasa katika manispaa ya Bukoba kwa kupeleka awamu ya kwanza shilingi bilioni moja kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kagera katika uwanja wa Mashujaa wa Mayunga uliopo Bukoba Machi 18, 2022 na kusema kwa kutambua umuhimu wa mradi huo pamoja na ule wa ujenzi wa soko tayari Serikali imejipanga katika kushughulikia changamoto hizo kikamilifu.
Makamu wa Rais amesema Serikali inaendelea kujenga na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ikiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa meli ya MV Mwanza (Hapa Kazi Tu), kwa manufaa ya wananchi wa Bukoba na kanda yote ya ziwa, ujenzi wa Meli hiyo unatarajiwa kukamilika Septemba 2022.
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa amesema bajeti ya kutengeza barabara Mkoa Kagera kupitia Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) kwa mwaka wa fedha 2021/22 imeongezeka hadi Bilioni 22.31 sawa na asilimia 137 ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2020/21 ilikuwa bilioni 9.39
Waziri Bashungwa amesema Mkoa kagera bado kuna changamoto ya barabara lakini Serikali inaendelea kuzifanyia kazi ambapo ameshaielekeza TARURA kuhakikisha mchakato wa manunuzi unafanyika mwanzoni mwa mwaka wa fedha ili vifaa viweze kufika kwa wakati na kazi kuanza bila kuchelewa na kuhakikisha mwaka wa fedha unapoanza kazi ya usanifu inaanza mapema ili fedha inapoingia kazi ianze.
Nae, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles Mbuge ameishukuru Serikali kwa kuupa kipaumbele Mkoa huo ambapo mpaka kufikia mwezi Februari mwaka 2022 tayari serikali imepelekea kiasi cha shilingi bilioni 315 kwaajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya elimu, miundombinu, afya na kilimo.
OR- TAMISEMI 

Next Post Previous Post
Bukobawadau