Bukobawadau

WAZIRI BASHUNGWA, KASEKENYA WAWASILI UJENZI LEO.

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, akiwasili katika ofisi ya Wizara hiyo katika mji wa Serikali Mtumba ambapo amepokelewa na kukaribishwa na menejimenti na baadhi ya watumishi, jijini Dodoma leo tarehe 04 Septemba, 2023.

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, akizungumza na menejimenti ya Wizara hiyo (hawapo pichani), mara baada ya kuwasili na kupokelewa katika ofisi yake mpya, jijini Dodoma. Kushoto ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mha. Godfrey Kasekenya na kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Mha. Aisha Amour.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, akifafanua jambo kwa menejimenti ya Wizara hiyo, mara baada ya kupokelewa na kukaribishwa katika ofisi za Wizara hiyo, jijini Dodoma tarehe 04 Septemba, 2023.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Eng. Aisha Amour, akitoa taarifa ya Wizara kwa Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, mara baada ya kuwasili na kupokelewa katika mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma tarehe 04 Septemba, 2023.


 

WAZIRI BASHUNGWA, KASEKENYA WAWASILI UJENZI LEO

Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Innocent Bashungwa, amewataka  watendaji na wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi kuongeza ubunifu na uadilifu ili kufikia malengo ya Serikali ya Awamu ya ita  katika Sekta ya ukuaji na uendelezaji wa miundombinu nchini.

Akizungumza mara baada ya kuwasili Wizarani hapo Mhe. Bashungwa amesema kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha miundombinu ya barabara, madaraja, majengo na wataalam katika Sekta hiyo wanaongezeka kwa wingi na ubora ili kuleta tija kwa Taifa.

“Siri ya mafanikio yoyote katika utendaji ni ushririkiano, hivyo naomba tushirikiane, tufanye kazi kwa weledi na ubunifu ili kujenga Taifa hili”, amesema Bashungwa

Aidha, Mheshimiwa Bashungwa amewataka wafanyakazi wote kufanya kazi kwa malengo yanayopimika ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo na kuleta tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Amemshukuru Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa na Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya pamoja na watendaji wengine kwa mapokezi mazuri na uandaaji wa taarifa ambayo itamuwezesha kuanza vizuri majukuu yake mapya.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara hiyo Eng. Godfrey Kasekenya, amemkaribisha Waziri Bashungwa Wizarani hapo na kumhakikishia kuwa Wizara hiyo ina timu yenye watu weledi watakaomsaidia kutimiza malengo ya Serikali katika kuliletea Taifa maendeleo katika sekta ya muindombinu.

Eng. Kasekenya amewataka watumishi wa Wizara hiyo kuendana na kasi ya mabadiliko ili kufikia matarajio ya Serikali na kila mtumishi kwa nafasi yake ahakikishe anakuwa mbunifu katika eneo lake la kazi.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Mhandisi Aisha Amour, amemhakikishia  Waziri Bashungwa kuwa miradi inayotekelezwa na Wizara hiyo inaendelea vizuri na ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na jengo la Wizara ambalo kwa sasa limefikia asilimia 68 .6 na ujenzi wa barabara zinazojengwa kwa utaratibu wa uhandisi, ununuzi, ujenzi na fedha (EPC+F) ambazo zina jumla ya kilometa 2035.

Kuwasili kwa viongozi wa Wizara ya Ujenzi ambao ni Mheshimiwa Waziri Innocet Bashungwa, Naibu Waziri Godfrey Kasekenya, Katibu Mkuu Balozi Mhandisi Aisha Amour na Naibu Katibu Mkuu Ludovick Nduhiye kunafuatia mabadiliko madogo yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Baraza la Mawaziri na Makatibu wakuu pamoja na kuifuta iliyokuwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Agosti 30, 2023 na kuunda Wizara mpya mbili za Ujenzi na Uchukuzi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi.

 


 


 


 

Next Post Previous Post
Bukobawadau