Bukobawadau

IGUNGA HAPATOSHI,UBABE,TIFU,FITNA ,UKAHUZU NA RISASI NJE NJE!!!!!!!!

HALI ya usalama katika Jimbo la Igunga inazidi kuwa tete baada ya milio ya risasi kurindima usiku wa kuamkia jana katika tukio lenye utata mkubwa, huku vyama vya Chadema na CCM vikiendelea kushutumiana.Wakati CCM) ikidai risasi hizo zilifyatuliwa na Mratibu wa Kampeni wa Chadema, Mwita Waitara, Chadema wanadai risasi hizo zilifyatuliwa na Mbunge wa Sumbawanga mjini, Aishi Hilal wa CCM.

Tukio hilo lilitokea saa 8:00 usiku wa kuamkia jana nje ya nyumba ya kulala wageni ya Misana Lodge ambapo magari mawili aina ya Toyota Landruicer na Toyota Prado yalivunjwa vioo.

Gari hiyo ya Toyota Landcuiser linaelezwa kumilikiwa na Mbunge Hilal na Prado inadaiwa kuwa ni ya Mbunge wa Viti Maalumu CCM, Ester Bulaya, ambaye CCM kinadai kuwa wafuasi wa Chadema walitaka kumteka.
Eneo lilipotokea tukio hilo ndiko ambako wafuasi wa Chadema wanalala ikiwamo kulaza magari yao yakiwamo yanayotumika katika kampeni na magari ya wabunge hao yapo katika Kituo cha Polisi Igunga kwa uchunguzi.

Naibu Kamishina wa Polisi Isaya Mngulu, ambaye ndiye Msemaji wa Polisi katika Uchaguzi Mdogo Jimbo la Igunga alithibitisha jana kuwapo kwa tukio hilo na kueleza kuwa silaha iliyotumika ni bastola yenye kipenyo cha milimita tisa.

“Hatujafanikiwa kuipata bastola hiyo lakini kutokana na maganda mawili ya risasi tuliyoyaokota eneo la tukio, inawezekana silaha iliyotumika ni bastola ya milimita 9,”alisema Mngulu.

Naibu Kamishina huyo alisema tayari watu zaidi ya 10 wamekwishahojiwa na polisi na kuandikisha maelezo yao wakiwamo Wabunge hao wawili, Waitara na walinzi watatu walioshuhudia tukio hilo lenye utata.
“Mpaka sasa hatuwezi kusema vioo vya magari yale vilivunjwa kwa kutumia risasi au mawe na hili ni moja kati ya mambo tunayoyachunguza, ikiwamo ni nani hasa aliyefyatua risasi zile,” alisema Mngulu.

Katika tukio hilo, kada mmoja wa CCM aliyekuwamo katika gari la Mbunge Bulaya aliyetajwa kwa jina la Ramadhan Twaha, alidai kuwa amejeruhiwa kwa risasi katika mkono wake wa kushoto na kutibiwa kisha kuruhusiwa.
Lakini Kamishina huyo wa polisi alisema kuwa, asingependa kuingia kwa undani kuhusu tukio hilo, ila polisi wameshaanza uchunguzi.
Kwa mujibu wa Kamishina huyo, polisi walipekua chumba anachoishi Waitara pamoja na cha dereva wa moja ya magari ya Chadema, lakini hawakukuta bastola yeyote ndani ya vyumba vyao.

Eneo kulipotokea tukio hilo ni umbali wa meta 20 hivi kutoka Hoteli ya Peak ambayo wamefikia viongozi wa kitaifa wa CCM.
CHANZO GAZETI LA MWANANCHI
Next Post Previous Post
Bukobawadau