Bukobawadau

CCM NA TATIZO LA 'ORUMBUGU' “ Na Prudence Karugendo

“ORUMBUGU” ni neno la Kihaya linalomaanisha mmea mmoja wenye usumbufu mkubwa kwa wakulima. Mmea huo unaotambaa chini kwa chini huweza kuonekana juu ya ardhi lakini pia ukiwa umejikita zaidi chini ya ardhi kuliko hata unavyoonekana juu ya ardhi na hivyo kulifanya zoezi la kuung’oa liwe kitendawili kisicho na mteguaji.
Kwa maana hiyo njia ya uhakika ya kuung’oa mmea huo msumbufu ili kuhakikisha shamba linakuwa katika hali ya usalama ni kuhakikisha mazao na mimea yote iliyomo shambani vinang’olewa kwanza. Hiyo ni kwa sababu mmea huo wa orumbugu una kawaida ya kujikita ardhini hasa chini ya mimea iliyomo shambani. Kwahiyo kitendo chochote cha kuung’oa mmea huo huku ukiwa umeyaonea huruma mazao yaliyomo shambani ni cha kuufanya mmea huo uzidi kustawi kinyume kabisa na inavyokuwa imekusudiwa.
Kwa ufupi ni kwamba wakulima waliodhamiria kuondokana na tatizo la “orumbugu” ni lazima wayasafishe mashamba yao bila kujali mazao yaliyomo mashambani mwao yamestawi kiasi gani katika kutimiza kile ambacho Wahaya hukiita “okufora orumbugu”, sina tafsiri sahihi, pengine kwa tafsiri sisisi tunaweza kusema kutifua orumbugu.
Tukija katika siasa tutaona kwamba chama tawala hapa nchini, CCM, kina tatizo, au matatizo, ndani ya mfumo wake kinaotumia kuitawala nchini. Tatizo hilo kililo nalo ni sawa kabisa na tatizo la orumbugu kwenye shamba. Sasa kinataka kufanya kazi ya kulitifua, kuling’oa tatizo hilo, eti kwa lengo la kuondokana nalo.
Tatizo la ziada linalojitokeza kwa CCM ni kwamba chama hicho kinakuwa na kitu ambacho Waingereza hukiita “double standard”, kuliona tatizo na kulitambua pamoja na kunuia kulifanyia kazi lakini wakati huohuo chama hicho kikijinufaisha na madhara yanayotokana na tatizo husika Sitaki nataka. Ni kwamba CCM haiko tayari kulisafisha shamba kwa kuyang’oa mazo yote yaliyomo kwa lengo la kulimaliza kabisa tatizo la orumbugu.
Baada ya vyama vya upinzani kulinyooshea kidole tatizo linaloisumbua CCM, na kuanzia hapo tatizo hilo likaenea na kuanza kuitesa nchi, hasa kutokana na chama hicho kuwa chama tawala, chama hicho kwa sasa kimezinduka kama vile kimetoka usingizini, na kukurupuka kuanza mikakati kinayodai ni ya kulishughulikia tatizo linalotajwa na vyama vya upinzani ikiwa ni pamoja na kujiimarisha sanjari na kujiimarisha kwa wananchi, hasa dhidi ya wapinzani.
Kuna habari kwamba CCM kwa sasa inaanza mkakati wa kujinadi upya kwa wananchi ili kukabiliana na wimbi la upinzani la kujinadi kwa wananchi. CCM yenye umri wa zaidi ya miaka 50 ikiwa madarakani eti nayo inajinadi kama chama kipya! Kwa nini CCM ijinadi kama chama kipya? Hapo ni lazima kuna mambo yanayofunikwa, tena yaliyo machafu na ya hatari. Nitaeleza.
Vyama vya upinzani havingekuwa na la kuwaeleza wananchi kama CCM ingekuwa imeweka kila kitu sawa. Lakini sasa CCM, kwa uzembe wake, imetibua kila kitu na kukiweka shaghalabaghala, huku ikiki yenyewe kwa kinywa kuwa inaelea ndani ya uozo. Ndipo ikaja na usemi wa kujivua gamba, kuwatimua wala na watoa rushwa pamoja na mafisadi toka ndani ya chama. Na kwa kufanya hivyo CCM ikawa imewarahisishia wapinzani kazi ya kuwaonyesha wananchi kwa nini chama hicho hakifai kuendelea kutawala nchi.
Kama ni shamba basi wapinzani wanawashauri wananchi waachane nalo sababu limeishaenea lote magugu mabaya ya aina ya orumbugu ambayo kuyaondoa ni lazima ufyeke na kung’oa kila kitu shambani. Kinyume cha hapo ni kupalilia na kuzidi kustawisha orumbugu mmea ambao ni hatari kwa mazao shambani.
Ninachotaka kusema hapa ni kwamba uozo wote ulioichafua nchi yetu, rushwa, ufisadi, utovu wa uadilifu, utovu wa uzalendo nakadhalika, haviwezi kuondoshwa kwa kuendelea kuwakumbatia walewale walioviasisi. Mfano, ni vigumu kuiondoa rushwa huku ukiwa umemkumbatia mtu anayeiona rushwa ndio mhimili wa kila kitu.
Kama ipo dhamira ya kweli ya kuiondoa rushwa na kujaribu kuifuta kabisa katika jamii hapanabudi kuhakikisha mfumo mzima ulioingiliwa na rushwa unang’olewa na kuwekwa pembeni.
Kwa mantiki hiyo, uchafu wote uliomo kwenye Chama Cha Mapinduzi na chama hicho kikiamini kabisa kwamba uchafu wake unawachefua wananchi, lakini kwa upande mwingine chama hicho kikiamini kwamba uchafu huo ndio unaokifanya kidumu madarakani, kamwe hauwezi kutoweka kama wananchi wanaendelea kukipa chama hicho ridhaa ya kuendelea kubaki madarakani. Sababu hiyo ni sawa na kuuchukia mmea wa orumbugu huku ukiendelea kulitia shamba mbolea na kuufanya mmea huo ustawi na kuzidi kujichimbia zaidi chini ya ardhi.
Kama nilivyosema mwanzo, dawa pekee ya kuufutilia mbali mmea mchafu wa orumbugu ni kulifyeka shamba na kutifua kila kitu kilichomo shambani. Hivyo kama kweli CCM wangekuwa wanakerwa na uchafu uliokigubika chama chao wasingesubiri kufyekwa na kung’olewa kama mazao kwenye shamba lililoandamwa na orumbugu, wangeamua kujing’oa wenyewe kwenye madaraka na kuanza kazi ya kukisafisha chama chao kikiwa nje ya madaraka.
Kwa nini nasema hivyo? Ni kwamba CCM ikiwa nje ya madaraka wataweza kumuoa kiurahisi yupi mwenye uumini wa kweli wa chama hicho na yupi anakitumia kama chaka la kujitafutia maslahi binafsi. CCM ikiwa nje ya madaraka ni lazima wale wote wanaokitumia chama hicho kama kichaka cha kufanyia uhalifu watajiondoa wenyewe bila hata kulazimishwa. Sababu watakuwa hawana uhakika wa kichaka chao hicho kuwalindia uhalifu wao usionekane. Chama kitabaki salama na watu salama wasiohofiwa kuleta madhara yoyote kwa nchi na wananchi.
Vilevile zile tambo za kwamba gamba limekwamia kiunoni haziwezi kujitokeza tena. Ni lazima gamba litavulika kiurahisi kwa vile hakuna atakayekuwa akilitamani tena gamba lisiloweza kumlinda na chochote.
Kwahiyo inabidi tuelewe kwamba mkakati ulioandaliwa na CCM wa kuwatuma makada na wasiokuwa makada wa chama hicho kuizunguka nchi wakiwaiga wapinzani eti nao wanakitangaza chama chao, ni ghiliba za kukifanya chama hicho kiendelee kuuhifadhi uchafu kilio nao.
Kawaida uchafu hautakiwi, lakini kama wapo wanaonufaika nao ni wazi wataulinda hata kama kwa kufanya hivyo wanahatarisha maisha ya jamii nzima waliyomo.
Tunaweza kujiuliza, ni kipi ambacho CCM wameshindwa kukinadi kwa miaka zaidi ya 50 wakiwa madarakani, hususan katika kipindi cha kiaka kama 30 wakiwa wao tu bila wapinzani, waje kukiona leo baada ya kuwaona wapinzani?
Eti wanaonyesha barabara kama mojawapo ya mafanikio ya chama chao! Kwani barabara hizo zinatengenezwa kwa michango ya wana CCM peke yao? Kweli hayo ni mafanikio ambayo chama tawala kinatakiwa kijivunie? Mambo yanayofanyika kwa kuzitumia kodi za wananchi wote yanapaswa yahesabike kama mafanikio ya chama tawala? Tena yakiwa yamecheleweshwa kwa zaidi ya miaka 50!
Wapinzani wanachokifanya ni kuwaeleza wananchi mapungufu yaliyomo kwenye yale yanayoitwa mafanikio ya CCM na kuwahakikishia wananchi kwamba wakipewa fursa ya kuongoza nchi ni lazima waitumie vizuri fursa hiyo kuiondoa nchi ilipokwamia na kuipaisha.
CCM ilichotakiwa kukifanya sio kujinadi ikiwaiga wapinzani, bali kutekeleza kwa vile tayari ina fursa ya kufanya hivyo. Lakini kiukweli ni kwamba imeshindwa, na sasa inarudi kujinadi kwa wananchi ikiwa imesahau kwamba iko madarakani. Kuomba kitu ambacho tayari unacho mikononi mwako ni dalili za kushindwa kukimudu kitu husika. Unapaswa unyang’anywe.
Tuipende tusiipende, kiukweli ni kwamba CCM imechafuka. Kujisafisha kwake inabidi kuwe kwa faragha. Kwahiyo haiwezi kujisafisha ikiwa imekikalia kiti cha enzi, nafasi hiyo haina ufaragha wowote. Kama chama hicho hakina uthubutu wa kujiweka faragha chenyewe itabidi wananchi tukisaidie kufanya hivyo ili kikajisafishe na kujiondolea kero ya kufuatwafuatwa na nzi kama kibudu. Tuifyeke na kuing’o CCM kama kweli tumedhamiria kuachana na mmea wa orumbugu.
prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau