Bukobawadau

MAKALA KWA WANABUKOBA KUTOKA MARUK VANILLAFARMING AND PROCESSING LTD

Wana Bukoba,
Leo ninalo neno la kusema na vijana wenzangu wa Bukoba. Nataka kuwatia moyo; tuna Uwezo wa kuishi Bukoba na kuwa matajiri. Tukiamua tunaweza kuishi Kagera, tukawekeza na kuvuna faida toka pande yoyote ya dunia. Ndiyo. Tunaweza haya yote lakini lazima kwanza tushinde matatizo makubwa ya KUJIDUNISHA, KUJIDHARAU, KUJIONA HATUNA KITU, KUJITENGA na tabia kama hizo.
Kujidunisha ni tofauti na KUJISHUSHA. Unapojidunisha ina maana unajiona dhaifu mbele ya mwenzio na hivyo unajidharau. Ni kwa nadra sana mtu anayejidhani kuwa ni mjinga akafanya mtihani akihisi atashindwa na matokeo yakaja ameshinda! Imani huzaa matokeo. Tusijikweze lakini pia kujidunisha iwe mwiko kwetu katika suala la kutafuta Uhuru wa Kiuchumi na Maendeleo binafsi na ya Jamii.
Ni uwongo ambao asili yake unaanzia kwenye vitabu tunavyosoma toka Elimu ya Msingi mpaka vyuoni ndiyo umetujengea dhana potofu kuwa Waafrika ni maskini, Watanzania ni Maskini, Kagera ni Maskini—hatuna kitu! Ni uongo huo huo tunalazimishwa kuusoma kwenye taarifa za Mashirika Makubwa ya Kimataifa tuwapo makazini ili tudumazwe akili milele na kuamini kuwa sisi ni maskini. Naomba nikuthibitishie leo, usione Marekani na Ulaya eti wanatoa vile wanaita misaada; kiuhalisia Mabara haya ni kapuku na maskini wa rasilimali na kuwalinganisha na Afrika ni sawa na Mto Ngono kuulinganisha na Ziwa Rwelu. Ziko nchi nyingi za mabara haya hazina mafuta, gesi, madini, hifadhi za wanyama, misitu, ardhi ya kilimo, na wakati mwingine hata rasilimali watu waliyonayo ni ndogo sana ukilinganisha na nchi kama Tanzania. Natamani ungekuwepo mpaka wa kuzuia mali-ghafi na chakula kinachosafirishwa toka Afrika kwenda kwenye mabara haya ukafungwa walau kwa siku moja, naamini dunia ingefumbuka macho na kuliamini hili ninaloandika. Vijana wa Bukoba tunazo fursa mbalimbali za kujikomboa. Tusifikirie kufanya Biashara za upagazi tu; za kununua bidhaa iliyokamilika sehemu moja na kuuza sehemu nyingine. Tupanue wigo na tuingie kwenye uzalishaji, uongezaji thamani wa mazao na uwekezaji katika sekta Mtambuka za miundombinu na ujenzi. Tusijifunge kifikra katika kufikiria fursa za uwekezaji. Tuwe na ndoto za kuendesha Biashara ndani na nje ya Mkoa, ndani na nje ya Nchi. Tunayo nafasi kubwa kutimiza ndoto hii ikizingatiwa kuwa Kagera yetu ni Mkoa pekee unaopakana na nchi nyingi kwa mpaka mrefu. Na nchi zote hizi hutegemea Tanzania katika mahitaji mbalimbali. Mara zote ukihubiri kwa maneno haya, vijana wengi huuliza tunapataje mtaji? Hilo nitajitahidi kuligusia katika mistari inayofuata hapo chini.
Miongoni mwa vyanzo haswa vya umaskini na kushindwa kwetu katika harakati mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kijamii ni kutelekeza silaha yetu ya asili—UMOJA! Ile kauli yetu “Umoja ni Nguvu, Utengano ni Udhaifu” imepoteza umaarufu na kupotea kabisa vinywani mwetu. Hata ikitamkwa haiendani kabisa na matendo. Wakati sisi tukifanya hivi, adui zetu (maskini, mabepari, wanasiasa, n.k) wameendelea kutumia vema dhana ya “Wagawe, Uwatawale Milele”. Na sisi tunafurahi kuzidi kuwaneemesha kwa kugawanyika na kubaki kuwa wapambe na washabiki wao. Tubadilike! Tukatae sababu na tukio lolote la kutagawa makundi, tujenge UMOJA wenye mtazamo mpana wa maslahi ya kiuchumi. Kwa wafanyabiashara adui yetu ni mmoja tu—Umaskini. Tupigane naye na tumshinde ili kijikomboa kiuchumi. Kama pesa isivyo na dini wala kabila, adui huyu pia si wa Wakristo wala Waislamu, hawaogopi Wayoza wala hana simile mbele ya Waziba. Anatishwa na kusujudia pale tu tunapoondoa tofauti zetu na kuja kwa pamoja kumkabili. Tukiwa na Umoja mtaji si tatizo. Ninaposema mtaji namaanisha maana pana zaidi ikihusisha rasilimaji watu na pesa, mtandao (who knows who), vitendea kazi, n.k. Wengi neno mtaji linaposemwa hukimbilia kufikiria pesa. Pesa siyo mwarobaini wa mafanikio. Ingekuwa hivyo nchi yenye mabenki yenye fedha nyingi halali na halamu kama Uswizi wananchi wake wote wangekuwa mabilionea. Tunapokuwa na Umoja ulio imara na tukaamua aina ya shughuli za kufanya kwa pamoja, suala la pesa ni dogo sana.
Hakuna wakati ambapo si Bukoba peke yake bali nchi nzima vijana wanahitaji kuwa na umoja madhubuti wa kujikomboa kiuchumi kama sasa. Tunapoelekea kwenye mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, fursa nyingi sana zinajitokeza. Fursa hizi ni kubwa mno na zenye mahitaji makubwa ya kimitaji na ujuzi. Tusipoamka sasa kuunganisha nguvu, rasilimali za umma ndani ya mkoa wetu na nchi yetu kwa ujumla vitageuka kuwa Supermarkets za Wageni. Shamba la kuchuma na kwenda kujenga makwao. Hii dhana ya Ubia ni pana na inahitaji muda muafaka kuielezea kwa ufasaha.
Nisisitize huku nikiweka kalamu chini; vijana Bukoba tutambue thamani yetu, tujithamini, tujionee fahari ya nguvu, maarifa na rasilimali zilizotuzunguka, na kubwa zaidi tujenge na kumarisha Umoja madhubuti katika kujikomboa kiuchumi na kuendeleza Jamii iliyotuzunguka.
Imeandikwa na: Maruk Vanilla Farming and Processing Ltd
Next Post Previous Post
Bukobawadau