Bukobawadau

RAI YA JENERALI Utegemezi, utawala wa kifalme, makaburi ya maendeleo**Kumbuka kisa cha mkuu wetu na kahaba wa Hollywood**

WIKI jana niliandika kwamba iwapo tunayo hamu kubwa ya kupiga, basi tuamue kupiga, ila tu tukubaliane ni akina nani wanastahili kupigwa. Niliainisha aina ya makosa ambayo yametendwa, mengi yakiwa na harufu ya jinai, ambayo walioyatenda wangestahili “kupigwa” kwa jinsi moja au nyingine.
Na pia nilisema, kwamba maendeleo tunayoyataka, tunayoyahitaji na tunayostahili hayawezi kupatikana kwa kutegemea Wachina, Wamarekani, Wajapani, Waturuki, Wakorea, Wahindi, au watu wengine wowote duniani isipokuwa sisi wenyewe.
Hakuna nchi duniani, na katika historia, iliyowahi kuendelezwa na nchi yoyote nyingine. Nchi zinaweza kushirikiana, nchi zinaweza kusaidiana kila inapotokea haja ya kusaidiana, nchi zinaweza kuunganisha nguvu zake kukabiliana na matatizo mahsusi, na kadhalika, lakini nchi moja haiwezi, haijaweza na haitaweza kuisaidia nchi nyingine kuendelea.
Kwa hiyo tunatakiwa kujikomboa kifikra na kutambua kwamba maendeleo yetu yatapatikana tu iwapo sisi wenyewe tutafanya kazi kwa bidii na maarifa kwa kutumia rasilimali zetu kwa umakini mkubwa na kwa kujali maslahi yetu na maslahi ya vizazi vyetu vijavyo, kwa mtazamo wa masafa marefu.
Pamoja na kwamba maneno ninayoyasema hapa si mapya, lakini utendaji wetu mara nyingi umeonyesha kwamba si maneno tunayoyajali sana. Bado tunaenenda kana kwamba wapo watu duniani ambao jukumu lao ni kutuangalia sisi na matatizo yetu na kufanya kila wawezalo kutusaidia tuweze kuondokana na matatizo yetu; ni ujuha mkubwa.
Ni ujuha mkubwa kwa sababu tunatakiwa tujue kwamba kila serikali, na kila jamii, ina jukumu moja kuu la msingi, nalo ni kuangalia maslahi ya watu wake na kuyasimamia. Kwa nguvu na akili zake zote. Hakuna serikali au jamii ya nchi moja ambayo inalo jukumu la kusimamia na kutetea maslahi ya serikali na jamii ya nchi nyingine. Hivi na hili nalo ni gumu kulielewa?
Inaelekea bado ni gumu. Watawala wetu wanaelekea kuamini kwamba kadiri tutakavyopata misaada ndivyo ambavyo tutaweza kuendelea, hata kwa mambo ambayo ni ya kipuuzi hivi kwamba kukubali msaada kuhusu mambo hayo ni kukubali kutukanwa na kutukanisha nchi.
Miaka takriban minane iliyopita mkuu wa nchi yetu alisafiri kwenda Uswisi kuhudhuria kikao cha uchumi wa dunia (Sijui huwa tunatafuta nini huko). Akiwa huko, katika dhifa yalimo jadiliwa matatizo ya ugonjwa wa malaria, aliinuka kahaba mwandamizi wa Hollywood na kuwataka walaji na wanywaji wachangie dola moja moja, tano tano au kumi kumi kusaidia vita dhidi ya malaria nchini Tanzania.
Kahaba huyo alikusanya dola 10,000, ambazo alimkabidhi mkuu wa nchi yetu, naye akazipokea! Kwa thamani ya leo hizo ni takriban shilingi 16,000,000 (milioni kumi na sita tu), ambazo hazitoshi hata kununua daladala ya abiria 25 kutoka Japan hadi kuileta nchini, achilia mbali kununua magari aina ya “shangingi,” magari vipenzi vya serikali yetu, na huo ndio mchango wa “changudoa”wa gharama kubwa kutoka Hollywood. (Huyu ndiye mwanadada aliyewahi kutamka hadharani kwamba ili kufanikiwa Hollywood unachohitaji ni uchi wa kike (neno halisi halichapishiki) pamoja na mtazamo fulani). Atukanwaye hajui katukanwa!
Haishangazi, basi, kwamba katika maeneo yetu mbalimbali tunajirahisi na kujidhalilisha kila siku. Kwa mfano tunaweza kutangaza, na picha zikapigwa, kwamba “mfadhili” amekabidhi matundu matatu, matano au kumi, ya choo cha shule ya msingi.
Katika migodi yetu inayonyonywa bure kabisa na “wawekezaji” (ambao kwa kweli tungewaita wahamishaji) kampuni inayochimba inajitangaza kwamba imefanya “social responsibility’ kwa kujenga madarasa mawili ya shule na kutoa kompyuta moja kwa ajili ya katibu muhtasi wa mkuu wa wilaya!
Ni matusi, lakini ni matusi ambayo tumeyakubali, si kwa sababu nchi yetu ni masikini bali kwa sababu watu wake, na hasa watawala wetu, wana umasikini wa fikra. Umasikini huu hautokani na wao wenyewe kuwa wajinga, la hasha. Baadhi yao ni watu wenye akili nyingi sana, na baadhi wanashahada zilizopangana mithili ya misahafu ya Pangani.
Lakini wanakosa umahiri wa kujua ni nini kilicho bora kwa wananchi wao, kimsingi kwa sababu hawaongozwi na falsafa yoyote inayoenda mbali ya wao kuwa madarakani na kuangalia maslahi yao binafsi na maslahi ya familia zao na maswahiba wanaowazunguka tangu waingie madarakani.
Huu ni ugonjwa wa kudumu (endemic) ila tu unaathiri familia na makundi mbalimbali kadri familia na makundi wanavyorithishana hatamu za dola. Kila mkuu wa familia anayeingia madarakani anajikuta (au anahakikisha) kwamba amezungukwa na wanafamilia na maswahiba zao.
Mke wake anakuwa mfadhili wa wanawake, wanawe wanakuwa washauri wakuu, wengine wafanyabiashara wakuu, na wengine wakandarasi wakubwa na maarufu katika fani wasizozijua kabisa!
Hii ni rushwa inayofanyika katika nchi zetu zilizo nyingi, ni ufisadi, ni utawala mbovu…lakini watu hawasemi lolote isipokuwa pembezoni, gizani. Halafu akiondoka mkuu mmoja anaingia mwingine, naye anafanya hivyo hivyo. Haishangazi, kwa hiyo, kwamba kila mmoja anayejipima na kuona kwamba anao uwezo wa kuwa mkuu wa wilaya, naye anatamani kuwa mkuu wa nchi, kwa sababu maslahi makubwa ya kutosha kuneemesha ukoo mzima yako katika ngazi ya taifa. (Imekuwa kama ilivyo kwa familia za akina Al Saoud, Al Makhtoum, Al Sabbahna Al Thani wa Arabuni, lakini bila utajiri wao).
Kwa jinsi hii tumejitengenezea mazingira ya kudumaa, utaratibu wa kuvia, mipangilio ya kutufanya tuendelee kwa kwenda chini, na kwenda nyuma. Hakuna njia ya kuiendeleza jamii ya aina hii, jamii isiyokuwa na uongozi unaotafuta maslahi ya jamii nzima bali ina utawala unaotaka umma mzima utumike kwa maslahi ya familia moja au ukoo mmoja.
Kwa wale wanaotaka kupiga, nasema pigeni, lakini mtakachopata ni wananchi wengi watakaojaa ngeu mwilini na ghadhabu mioyoni, lakini jambo moja naweza kuwahakikishieni: katu hamtapata jamii iliyoendelea, na hamtapata wananchi watakaowaheshimu na kukumbukia mema mliyowatendea.
Kinyume chake mtapata wananchi watakaowalaani chini chini mkiwa bado madarakani na wazi wazi mkiisha kuondoka madarakani; wananchi watakaolipiza kisasi dhidi yenu wenyewe au dhidi ya uzao wenu mkiisha kuyoyoma, mara tu watakapopata fursa ya kufanya hivyo.
Haya sijayatunga, wala sijayabuni, na wala sikisii au kubahatisha. Hii ndiyo sheria ya jamii zinazofanana na yetu.
Next Post Previous Post
Bukobawadau