Bukobawadau

Tanzania inahitaji jeshi la kulinda amani

Na Prudence Karugendo

JUMA lililopita nilindika kuhusu kinachodaiwa ni ugaidi. Nilipingana na tafsiri inayotolewa kiujanja kuwa ugaidi ndiyo “terrorism” inayotajwa na mataifa makubwa ya Magharibi, hususan Marekani, na kulitumia neno hilo kama waranti (hati) ya kuwakandamiza kimanyanyaso wanyonge na wadhaifu ilihali “terrorists” wenyewe ni mataifa hayo makubwa.

Lengo la makala yangu hiyo lilikuwa ni kuchokoza hisia za wasomaji ili wakautafakari ukweli huo, wakauondoe ulikojificha na kuuweka katika matumizi ya kweli. Kusudi tusiendelee kunyanyaswa na mataifa makubwa yenye nguvu kwa visingizio vilivyo wazi kabisa kwa sisi kujifanya vipofu huku tukiigiza kuwa hatuvioni visingizio hivyo. Visingizio vya kwamba mataifa makubwa yana mpango wa kutokomeza “terrorism”, ambayo sisi tumeamua kuibatiza ugaidi, wakati mataifa hayo ndiyo yanayokitengeneza kitu hicho.

Nimefarijika kwamba wasomaji wengi wamenielewa. Ila karibu wote niliowasiliana nao wametoa maoni kwamba kabla hatujayashughulikia haya maneno, “terrorism” na ugaidi, katika uwanda wa kimataifa, ni bora kwanza tuangalie yanavyotugusa sisi na kuathiri mustakabali wetu hapa nyumbani kwetu.

Msomaji mmoja katoa maoni yake kwamba makala yangu ya Jumapili iliyopita ingependeza sana kama ingerudiwa kuchapishwa lakini ikiwa imeondolewa maneno dunia na Marekani. Yeye kapendekeza badala ya neno Marekani niandike CCM, na badala ya neno dunia niandike Tanzania. Kasema hiyo maana yake ni kwamba hisani huanzia nyumbani.

Kaongeza kwamba tusianze kuyaangalia yanayofanywa na Marekani, nchi inayotamani kuitawala dunia kwa mabavu, tukasahau ya CCM, chama kinachotamani kuitawala Tanzania kwa mabavu milele yote.

Tukirudi kwenye hoja tutaona kwamba ni katika tamaa hiyo ya Marekani kutaka kuitawala dunia, taifa hilo likatumia uwezo wake kiuchumi na kijeshi kutengeneza ubabe, “terrorism” ili kumuogofya kila anayetaka kuupinga mpango wake wa kutaka kuitawala dunia kiubabe. Papo hapo Marekani ikageuza kibao na kudai kwamba anayejaribu kupinga mpango wake huo ni “terrorist” na ni lazima Marekani imshughulikie.

Ndani ya ujanja huo uliojaa hila Marekani ikawa imetengeneza kitu inachodai ni “terrorism” na kukipachika kwa wengine kusudi kitumike kama fimbo ya kuwachapia wanaoushuku mpango wake wa kibabe wa kujifanya kilanja wa dunia.

Chama tawala hapa nchini kwetu, CCM, kimeshabihiana na Marekani kwa kila kitu. Kimuonekano CCM ni chama kikubwa kuliko vyote hapa nchini. Kiuwezo, kwa maana ya uchumi, ni chama kinachopaswa kuwa tajiri kuliko vyama vyote kutokana na ukweli wa kwamba uchumi wake umechangiwa na kila Mtanzania tena kwa njia ya kulazimishwa enzi za siasa za kiimla za chama kimoja. Ni kama uchumi wa Marekani ulivyochangiwa, kwa njia moja au nyingine, na mataifa mbalimbali duniani.

Pamoja na hayo bado CCM inao upenyo wa kuugeuza uchumi wa nchi uonekane ni uchumi wake kutokana na mfumo wake wa ajabu wa kuendelea kujiona ni chama dola.

Ugonjwa ilio nao CCM, uliojigeuza na kuonekana kama udhaifu wa kinga katika mwili wa binadamu, ni wa kukosa makada watendaji wa kukisimamia kile kinachoaminiwa na chama hicho kuwa ni halali yake huku ushawishi ukiwa umejengwa kwa wananchi ili wabaki wakiamini kwamba maslahi yao yanalindwa.

Ni ugonjwa huo ambao umekifanya chama hicho tawala kianze mikakati ya kubuni vitisho kwa mtindo wa heri lawama kuliko fedheha dhidi ya wapinzani wake, hasa baada ya kuishiwa njia zote za ushawishi kwa wananchi.

Kwa sasa tunashuhudia jinsi amani ya nchi yetu ilivyovurugika. Kutekana nyara, kushambuliana na hata kuuana yanaanza kuwa mambo ya kawaida katika nchi yetu iliyokuwa ikijitambulisha kama kisiwa cha amani kwa muda mrefu.

Jambo linalovuta hisia za watu ni la kuuona uovu wote huo ukielekezwa na kuulenga tu upinzani dhidi ya chama tawala na serikali yake. Haijatokea tukaona chama tawala nacho kikishambuliwa kwa njia ileile, kitu kinachoweza kutufanya tuhisi kuwa pengine upinzani nao unalipiza kisasi.

Ni upinzani pekee ndio unaofanyiwa vituko na kukoseshwa amani. Jambo la kusikitisha na kukatisha tamaa ni kwamba vyombo vya dola vinajionyesha wazi jinsi vilivyoegemea upande mmoja tu wa chama tawala huku navyo vikiushambulia upinzani waziwazi!

Matukio mengi, kama siyo yote, ya uvunjifu wa amani katika shughuli za vyama vya upinzani yamesababishwa na vyombo vya dola, kinyume na mategemeo ya wananchi kwamba vyombo hivyo vinapaswa kulinda usalama na amani ya wananchi mahali popote bila kujali itikadi ya mtu.

Inawezekana vyombo vya dola vinafanya hivyo katika kuonyesha utiifu kwa Amiri Jeshi Mkuu aliye pia mwenyekiti wa chama tawala. Lakini kinachojionyesha zaidi bila kuacha chembe ya shaka ni chama tawala kutumia njia hiyo ya vyombo vya dola kuwa chini ya mwenyekiti wake na chenyewe kuonekana kiko juu ya vyombo hivyo vya dola na hivyo kuviamrisha vitende jinsi kinavyotaka.

Mbali na hilo kuna kikundi cha hatari kinachomilikiwa na chama tawala kinachoitwa Green Guard. Inasemekana kikundi hicho ni cha vijana wanaoshughulika na ulinzi wa CCM. Suala la ulinzi ndani ya chama si gumu kueleweka, ndiyo maana karibu vyama vyote nchini vilivyopanuka kiasi cha kutosha vina utaratibu huo.. Tunasikia Blue Guards, Red Brigade nakadhalika.

Tofauti iliyopo kati ya vikundi vya ulinzi vya vyama vingine na Green Guard, inayokifanya kikundi hicho kionekane ni hatari, ni kwamba kikundi hicho kinaonekana kupata mafunzo rasmi ya kijeshi. Katika matukio mbalimbali vijana wa Green Guard wameonekana wakitoa salaamu za kijeshi, gwarige la kijeshi na wakati mwingine kuonekana wamebeba silaha mbalimbali za moto na za kijadi.

Mfano katika uchaguzi mdogo wa Igunga, takriban miaka mitatu iliyopita, vijana wa Green Guard walionekana mjini Igunga huku karibu kila mmoja akiwa amebeba panga mithili ya Interahamwe wa Rwanda! Interahamwe ndio waliofanya mauaji ya kimbari kule Rwanda.

Polisi kule Igunga walikuwa wanawaangalia vijana hao wa Green Guards na silaha zao za jadi wakiwa wameridhika na hali hiyo bila kuthubu kumgusa hata mmoja wao, pamoja na kesi nyingi zilizopelekwa polisi kuhusiana na mwenendo muovu na wa hatari wa vijana hao wa CCM.

La kushangaza ni kwamba Chadema waliposema wanakusudia kuanzisha makambi kwa ajili ya kuwapatia mafunzo ya ukakamavu vijana wao wa ulinzi ikawa nongwa. Yakajitokeza madai ya kwamba chama hicho kinataka kuunda jeshi, mara wanataka kuanzisha vikundi vya ugaidi nakadhalika. Lakini yote niliyoyaeleza kuhusu CCM hayatajwi kama ugaidi, neno linalotumika vibaya kumaanisha uvunjifu wa amani.

Hayo yote yanayofanywa na CCM ni ubabe usio na tofauti yoyote na ubabe unaofanywa na mataifa makubwa dhidi ya mataifa madogo na dhaifu. Ubabe ambao waathirika wake wakijaribu kufurukuta mara moja wanavishwa sifa ya ugaidi au “terrorists”.

Lakini hatahivyo, uhalisia unatuonyesha kwamba mfumo wowote dhalimu, iwe kwa binadamu, wanyama na hata mimea, hutengeneza mfumo mwingine wa kujilinda na udhalimu. Ndiyo maana baadhi ya mimea ilibidi iote miba ili kujilinda na udhalimu wa kuguswaguswa ambao ungeweza kuiangamiza mimea hiyo kwa njia hiyo.

Kwa mwanadamu hali inapofikia hapo ndipo kwa sasa tunasikia kwamba linahitajika jeshi la kulinda amani lisiloegemea upande wowote. Ni katika kuwaepusha watu wasiote miba katika kujihami na udhalimu.

Kwa hali ilivyo hapa nchini kwetu kwa sasa hatupaswi kuiacha miili yetu ikaota miba ili kujilinda yenyewe dhidi ya udhalimu, sababu miba ikishaota milini mwetu inaweza kuleta madhara makubwa, na kuiondoa miba hiyo ni gharama kubwa sana na isiyowezekana kuimudu wakati mwingine.

Kwahiyo kama kweli Tanzania ulikuwa mfano mzuri wa nchi iliyo na amani, huu ndio wakati muafaka wa kuleta jeshi la kulinda amani, hasa ikizingatiwa kuwa tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa kufa na kupona wa 2015. Siyo isubiriwe mambo yawe kama ya Darfur ambako mili iliyoota miba tayari kujilinda haitaki kuwaona walinzi wa amani. Maana kule hakuna tena kitu kinachoitwa amani kinachohitajika kulindwa, sanasana kufanya mipango ya kuirudisha amani. Tusingoje kufikishwa huko.

prudencekarugendo@yahoo.com

0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau