Bukobawadau

Tunahitaji matokeo makubwa au uelewa mkubwa?


Na Prudence Karugendo
SERIKALI  ya CCM haiishi vituko. Kituko kimojawapo ni cha kukigeuza karibu kila kitu kiwe katika mfumo wa kisiasa, kwake kila kitu ni siasa! Wananchi wenye mahitaji, kikikosekana cha kuwaahidi wanaweza wakaahidiwa daraja hata kama mahali walipo hakuna mto, ilmradi ahadi. Hizo ndizo siasa za CCM, kila kitu kinatazamwa kisiasa!
Hebu angalieni kisa hiki; kufuatia matokeo mabaya katika mitihani ya fainali kwa miaka ya karibuni yanayozihusu shule zetu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilipeleka wataalamu wake katika kitu kinachoitwa Maabara ya Elimu. Wataalamu hao wakaibuka na mkakati unaoitwa Matokeo Makubwa Sasa “Big Results Now” (BRN).
Huo eti ni mkakati wa kuondoa matokeo mabaya kwa watoto wetu wanaofanya mitihani ya fainali, iwe ya kumaliza darasa la saba, kidato cha nne na hata kile cha sita.
Hapa kinacholengwa ni matokeo na wala sio kile kilichomo kwenye matokeo hayo, nitaeleza.
Mkakati huo umeonekana kuwafurahisha sana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Jumanne Kawambwa, na naibu wake, Philipo Mulugo, kwa vile unawapa ahueni kutokana na aibu inayowapata kufuatia zaidi ya nusu ya wanafunzi kushindwa mitihani ya fainali kila mwaka.
Sasa mawaziri hao wameigeukia siasa kwa kuibua hiyo kaulimbiu ya “Big Results Now”. Lakini ieleweke kwamba hii ni kaulimbiu ya kisiasa kama zilivyo kaulimbiu nyingine nyingi zinazoishia tu kwenye maneno bila kuziona juhudi zozote kivitendo zinazozishadidia kaulimbiu hizo.
Mfano, tunayo kaulimbiu ya Kilimo ni Uti wa Mgongo, Kilimo Kwanza na nyingine nyingi za kutoa tu matumaini kwa wananchi bila kutibu lolote.
Ni kweli, kwa sasa wananchi wamechoshwa na ubovu wa elimu yetu unaojionesha katika taifa hili. Bilashaka serikali inaliona na kulitambua hilo, na ni wazi kwamba linaifadhaisha sana. Kwahiyo kwa harakaharaka serikali imeamua kulidaka na kulifanyia kazi kama tulivyoona.
Kazi yenyewe si nyingine bali ya kuwafurahisha wananchi kwa kutoa matokeo yaliyo makubwa bila kujali uzuri wake, kwa maana ya wanafunzi kushinda kwa wingi kuliko matokeo yalivyo kwa sasa, hata kama ukubwa wa matokeo haumaanishi ukubwa wa maarifa. “Big Results Now”.
Lakini hatahivyo sidhani kama hiki ni kitu kipya, tulishuhudia mwaka juzi karibu robo ya wanafunzi, waliomaliza darasa la saba, wakipitishwa kwenda kidato cha kwanza wakiwa hawajui kusoma wala kuandika! Naamini “Big Results” ilishaanza kimyakimya.
Bilashaka huu mkakati wa sasa umetangazwa kufunika hasira za wananchi zilizojitokeza kufuatia matokeo mabovu ya mtihani wa mwaka jana wa kidato cha nne.
Sababu mimi sioni kama ulikuwepo ulazima wa kuutangaza mkakati huo, kwa sasa, unaodaiwa ni wa kuboresha matokeo ya mitihani. Kama kweli kuna umakini uliodhatitiwa katika jambo hili ingeachwa tu ili baadaye tuone matokeo yake. Hiyo ni kwa sababu hatuwapigii kura wanafunzi ili washinde, kushinda kwa wanafunzi kunatokana na juhudi zinazofanyika ndani ya darasa, sio juhudi za kukitangaza kitakachofanyika. Sasa kampeni za nini?
Kwa maana hiyo, ndiyo sababu nauchukulia mkakati huo kama wa kisiasa zaidi kuliko kielimu. Matokeo ya mitihani au mafanikio ya kielimu hayapaswi kuhamasishwa kwa njia ya makongamano, matamasha wala mikutano ya hadhara kwa kuhusisha umma wote.
Hii ni kwamba serikali inataka kuwafurahisha wananchi na matokeo mazuri ya watoto wao wanapofanya mitihani ya fainali. Lakini kinachotafutwa shuleni ni zaidi ya matokeo mazuri. Tunawapeleka watoto shuleni ili wakapate maarifa, wakaelewe. Siwezi kufurahi hata kidogo kumsikia mtoto wangu aliyemaliza darasa la saba bila kujua kusoma wala kuandika akichaguliwa kwenda kidato cha kwanza.
Hii “Big Results” inaweza ikatuonesha mambo mengi ya ajabu. Mtoto anaweza kwenda kidato cha kwanza, akamaliza kidato cha nne, akapanda kwenda kidato cha tano na mwisho kumaliza kidato cha sita bila kuelewa kusoma na kuandika, si ni “Big Results”?
Katika haya Matokeo Makubwa tunategemea kuwapataje watabibu, wahandisi, wanasheria nakadhalika walio bora? Si yataishia kuwa yaleyale ya Naibu Waziri wetu wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi aliyekwenda kuitangazia dunia kuwa Tanzania ni muungano wa visiwa vya Pemba na Zimbabwe! Huyo ni Waziri wa Elimu, je, itakuwaje kwa mwanafunzi? “Big Results”!
Ieleweke kwamba nchi inahitaji uelewa, tusihangaike na matokeo kama hakuna uelewa. Haya ya kuuhangaikia ushindi wa mkupuo wa pamoja ni ya kujidanganya sisi wenyewe kama mazuzu iwapo tutakaokuwa tukishangilia ushindi wao hawaelewi lolote.
Kwa maoni yangu, ni bora wanafunzi wakakosa kufaulu lakini wakiwa nacho wanachokifahamu vichwani mwao, kuliko kuwaona wakifaulu wote wakati ndani yao wamo wasiojua kusoma na kuandika.
Hebu tuliangalie hili kwa lugha nyepesi. Mtoto anamaliza darasa la saba anaambiwa kachaguliwa kwenda kidato cha kwanza, wazazi wanashangilia, babu yake anamuita akamwandikie barua kwa njia ya imla mtoto hawezi! Kweli furaha ya wazazi ya kumuona mtoto wao anachaguliwa kwenda kidato cha kwanza itakuwa na maana yoyote kweli? Si ni bora aliyekosa kwenda kidato cha kwanza lakini anaweza kumuandikia barua babu yake kwa njia ya imla?
Tunataka maarifa, sio ushindi wa kishindo huu unaoitwa Matokeo  Makubwa Sasa. Huu ushindi wa “Big Results” ni njia ya kisiasa ya kujiondoa aibu kwa wale waliopewa nafasi za kuisimamia elimu yetu nchini.
Kama na wao walizipata nafasi hizo kwa njia ya “Big Results” huu ndio wakati muafaka wa kuwakamata vizuri. Ni bora wakajiwajibisha wenyewe, kwa maana ya kujiondoa, kuliko kutuletea vituko hivi vya Matokeo Makubwa yasiyo na chochote ndani yake.
Sasa tufanye nini ili tupate maarifa yanayokidhi haja? Mtawala wa Uganda katika miaka ya 1970, Idd Amin Dada, alikuwa mtu ambaye hakwenda shule kabisa. Alifundishwa kusoma aeiou na baba yangu mkubwa wakiwa kwenye Vita ya Pili ya Dunia nchini Burma, ambayo kwa sasa inaitwa Myanmar. Lakini ajabu Amin alikuwa na maarifa ya kutosha katika kuishughulikia elimu.
Wakati wa utawala wake, 1971 – 78, alilazimisha wanafunzi wote nchini mwake wanaofaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza, kuanzia kidato cha nne na kuendelea, waende kusomea uwalimu. Yeye aliamini kwamba hao wenye akili nzuri ndio waliofaa kuwa walimu bora kusudi wakawafundishe wengine wenye akili za kuchechemea waweze kuelewa. Matokeo yake Uganda iko juu kielimu mpaka sasa, kwa maana ya kimaarifa, ikilinganishwa na Tanzania yenye mikakati ya Matokeo Makubwa.
Cha kuzingatia ni kwamba Amin hakutumia maabara katika kuipandisha juu elimu ya nchi yake.
Lakini katika Tanzania wanaopewa nafasi za kwenda kwenye uwalimu ni wale waliofaulu katika madaraja ya mwisho au kwa maneno mengine waliopata msamaha wa wasahihishaji, na wakati mwingine hata wale waliopata sifuri.
Utawasikia watu wakishangaa, kwa kijana ambaye uelewa wake shuleni ulikuwa mdogo, “..… yaani hata nafasi ya uwalimu amekosa…!”. Hiyo maana yake ni kwamba kwenye uwalimu ndiko pa kupeleka wenye uelewa hafifu!
Kwa maana hiyo asiyeelewa vizuri ndiye anayepewa nafasi ya kwenda kwenye uwalimu ili akawaeleweshe wengine. Hivi kweli uko ni kuelewesha au ni kuwatia wengine uvivu wa kuelewa?
Hayo yote wizara inayaona na kuyaacha yaendelee jinsi yalivyo ili baadaye iibuke na mikakati ya ajabuajabu. Katika mazingira ya aina hiyo tunawezaje kuyapata maarifa tunayoyahitaji? Lakini kwa mkakati wa “Big Results” nadhani hiyo siyo hoja!
Ningependa kumshauri Mheshimiwa Kawambwa kwamba hatutakiwi kutumia aibu kutengeneza aibu nyingine. Kilichopo atengeneze walimu wengi wazuri kutokana na vijana wenye uelewa mzuri, awaandalie mazingira bora ya kufanyia kazi ndipo tuyapate maarifa bora sasa, sio “Matokeo Makubwa Sasa” kama inavyofikiriwa. Mafanikio katika elimu yatokane na maarifa na siyo kubebana kwa njia ya mikakati.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau