Bukobawadau

Wanaushirika KCU (1990) Ltd. wambebesha Chiza mzigo wa lawama

Na Msiba Pakia

WAZIRI wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Kajoro Chiza, mbele ya Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, kalazimika kuutamka ukweli ulio mchungu kwake. Mbele ya Kamati hiyo kakiri kwamba vyama vya ushirika nchini ni eneo mojawapo linaloongoza kwa ufisadi, wizi, dhuluma na uwajibikaji dhaifu.

Huo ni ukweli ambao muda wote wanaushirika wameupigia kelele bila mafanikio ya kuyaona mabadiliko yake, kiasi cha wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. wa mkoa wa Kagera kufikia kuandika barua ya malalamiko na kuifikisha kwa waziri mwenyewe Chiza.

Barua hiyo iliyokuwa ikieleza madhambi yote yanayofanywa na viongozi pamoja na watumishi, waajiriwa, wa chama hicho cha ushirika, ikiwa imeambatanishwa na nakala za nyaraka mbalimbali za kiofisi zinazoushadidia ufisadi unaofanyika ndani ya chama hicho, haikujibiwa wala kuchukuliwa hatua yoyote kama yalivyokuwa mategemeo ya wanaushirika hao. Badala yake wanaushirika walishangaa kumsikia Waziri Chiza ameipeleka barua hiyo KCU ili kuwafanya mafisadi wanaoshitakiwa kwake wazidi kujidhatiti!

Kitendo hicho cha waziri walikifananisha na kitendo cha hakimu kumpelekea kesi mtu anayetuhumiwa na wizi ili yeye, mtuhumiwa, akawahukumu mwenyewe watu wanaomtuhu kwa wizi!

Ni kitendo hicho kinachowafanya wakulima, wanaushirika wa KCU, waanze kukosa imani na Waziri Chiza wakimshuku kuwa kuna namna atakayokuwa anashirikiana na uongozi wa KCU kuwahujumu, kitu kinachodhihirisha jinsi Rais Kikwete alivyo katika wakati mgumu wa kuwahakikishia wananchi wake maisha bora kwa kila mmoja wao.

Wanasema haiwezekani mtu aliyeaminiwa na rais na hivyo kumfanya msaidizi wake, afanye mambo ya aina hii halafu yaendelee kuwepo mategemeo ya kumuona rais anafanikiwa katika ahadi zake.

Pamoja na hiyo, wanaushirika wa KCU pia wameyakosoa baadhi ya maneno ya Chiza aliyoyatoa mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Profesa Msorwa, yanayosema kwamba serikali ilianzisha vyama vya ushirika. Wanasema wao walianzisha ushirika hata kabla ya uhuru, wakiuita ushirika wao Bukoba Co-operative Union (BCU). Wakasema serikali hii imeukuta ushirika wao huo na kuamua kuusimamia kama ilivyosimamia mambo mengine yote baada ya uhuru.

Kwa maoni ya wanaushirika hao ni kwamba Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza, hajafanya lolote kwa upande wa ushirika tangu ateuliwe kushika wadhifa huo. Wanadai kwamba yeye ndiye ameufanya ushirika nchini kuwa taabani kiasi hiki kutokana na kuzipiga danadana tuhuma zinazotolewa na wanaushirika dhidi ya viongozi wao mafisadi.

Eti ndiyo maana kwa sasa analazimika kupeleka mswada wa vyama vya ushirika Bungeni ili kufuta sheria namba 20 ya 2003 ambayo ni kama inawafanya viongozi wa ushirika kuamua kufanya lolote walitakalo hata kama ni la kifisadi.

Wanaushirika hao wanasema iwapo Waziri Chiza angekuwa makini, akifanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuacha kuwatazama usoni viongozi wa ushirika walio mafisadi au kufanya nao urafiki kama anavyofanya hivi sasa, eti hali ya ushirika isingekuwa mbaya kama ilivyo kwa sasa. Eti ushirika ungenawiri kama ulivyokuwa miaka ya nyuma, ukiwafanya wakulima kuutamani na kuongeza bidii ya kuchapa kazi katika kilimo.

Katika kuthibitisha madai yao wana KCU wameeleza walichomwandikia Waziri Chiza. Walimwandikia, pamoja na mambo mengine, kwamba kwa miaka kadhaa chama chao kimekuwa kikitumia pesa nyingi kuliko mapato yake halali, na kwamba hakujawahi kufanyika jitihada zozote kubaini matumizi ya ziada yanavyogharamiwa. Hivyo walitaka ufanyike uchunguzi ili, pamoja na mambo mengine, ijulikane kwa nini ushirika huo unashindwa kujiendesha wakati unazo rasilmali nyingi.

Pia walimwandikia waziri kwamba katika Mkutano Mkuu wa KCU (1990) Ltd. uliofanyika tarehe 15 Aprili, 2009. Iliazimiwa kuwa ushirika uuze hisa 26,666,667 kati ya hisa 42,880,000 uliokuwa nazo katika benki ya CRDB, kwa ajili ya kuunda mfuko wa kununulia kahawa kutoka kwa wakulima badala ya kutegemea mikopo toka kwenye benki iliyo na riba kubwa.

Jambo linalowaduwaza wanaushirika hao ni kwamba haijulikani pesa hiyo iliyofikia kiasi cha shilingi bilioni 3.4, baada ya kuuza hisa mil. 21,000,000, ilikowekwa kutokana na chama hicho kushindwa kununua kahawa kwa pesa tasilimu kwa misimu kadhaa kwa madai ya kutokuwa na pesa.

Wanaushirika wakazidi kusema kwamba katika nyaraka rasmi za KCU (1990) Ltd., kwa kutumia mahesabu ya mizania iliyokaguliwa, inathibitishwa kuwa chama hicho kimepata hasara kwa karibu miaka 7 mfululizo tangu mwaka 2002/3. Hasara hiyo inaainishwa kama ifuatavyo.

Mwaka 2002/3 mapato yalikuwa shilingi mil. 255.0, matumizi shilingi mil. 835.2, pungufu shilingi mil. 579.3. Mwaka 2005/6, mapato yalikuwa shilingi mil.585.9, matumizi shilingi mil. 1,230.4, pungufu kwa shilingi mil.644.5. Mwaka 2006/7 mapato yalikuwa shilingi mil. 600.2, matumizi yalikuwa shilingi mil.926.8, pungufu kwa shilingi mil. 326.6.
Mwaka 2007/8, mapato yalikuwa 336.3, matumizi shilingi mil. 1,296.0, pungufu kwa shilingi mil. 959.7. Mwaka 2008/9 mapato yalikuwa shilingi mil. 1,025.8, matumizi shilingi mil. 1,418.1, pungufu kwa shilingi mil. 392.3. Mwaka 2009/10, mapato yalikuwa shilingi mil. 764.4, matumizi yalikuwa shilingi mil. 1,398.4 pungufu kwa shilingi mil. 634.0. Na mwaka 2010/11 mapato yalikuwa shilingi mil. 1,060.8, matumizi yakawa shilingi mil. 1,488.0 pungufu kwa shilingi mil. 427.2.

Hiyo maana yake ni kwamba kwa mwaka wa fedha wa 2010/11 KCU (1990) Ltd. ilikuwa imelimbikiza deni la shilingi milioni 3,790.1 ambalo lingeweza kukua na kuwa kubwa zaidi kwa mwaka wa fedha wa 2011/12 na 2012/13.

Katika barua hiyo, wana KCU walimweleza waziri kwamba, upoteaji wa limbikizo la madeni na ukuaji wa hara wa limbikizo la faida unaojitokeza kwa njia zisizoweza kutolewa maelezo, ni baadhi ya mambo yanayohitaji kutiliwa shaka. Hoja hii inapewa nguvu zaidi, hasa kutokana na kauli ilitolewa na Baraza la Wafanyakazi wa COASCO, ya kwamba kuna nyakati ambapo Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo amekuwa akila njama na watendaji wa vyama vya ushirika kupotosha hali halisi ya vyama hivyo ilivyo hapa nchini.

Kwahiyo kinachowashangaza wanaushirika hao ni wapi zilikopatikana shilingi bilioni 1.2 zilizotumika kama gharama ya ujenzi wa kinachoitwa kitegauchumi cha ushirika huo, jengo la ghorofa 3 lililoko katika mtaa wa One Way mjini Bukoba?

Kwahiyo wanaushirika wa KCU wanashauri kwamba wakati Mhandisi Christopher Chiza akijiandaa kupeleka Bungeni muswada wa vyama vya ushirika, angepaswa kuisafisha nyumba yake kwanza, wizara yake, kwa kuwashughulikia wale wote aliodai kuwa kila akiwatuma kwenda kuihakiki KCU inawahonga ili waseme uongo.

Kwa maneno yake mwenyewe, waziri, anakiri na kusema jinsi ofisi yake ilivyo na watu wasio waaminifu, watu wanaotumwa kuuangalia ufisadi unaowatesa wakulima ndani ya chama cha ushirika wakaishia kuhongwa na mafisadi walewale waliotumwa kuwakagua.

Bila Chiza kuwashughulikia watu hao, yote aliyowaeleza wajumbe wa tume ni lazima yaonekane ni kazi bure, sababu hata mabadiliko anayotaka kuyafanya kwenye mswada anaouandaa yatawakuta watu wake waendeleze tabia ileile anayotaka kuikwepa. Kwahiyo cha msingi ni kuwashughulikia watu wake kwanza.

Vilevile anatakiwa kuhakikisha kwamba viongozi wenye mtazamo hasi kama wa kwake kuhusu vyama vya ushirika wanajirekebisha pia, akiwemo yeye mwenyewe, ndipo ushirika uweze kushamiri nchini kwa miaka ijayo.

mpakia@yahoo.com
Next Post Previous Post
Bukobawadau