Bukobawadau

Yanga yainyatia Simba kileleni


Dar es Salaam. Vinara wa Ligi Kuu Simba wameendelea kujichimbia kileleni baada ya kuichapa Prisons kwa bao 1-0, huku watani zao Yanga wakivunja mwiko kwa kuichapa Kagera Sugar 2-1, kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera.
Kwa matokeo hayo Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 18, wakifuatiwa na Yanga yenye pointi 15, kabla ya mechi za leo kati ya Azam yenye pointi 14 dhidi ya JKT Ruvu na Mbeya City (14) dhidi ya Mgambo JKT.
Uwanja Taifa, kiungo Jonas Mkunde aliifungia Simba bao la pekee kwa shuti la juu la umbali wa mita 18, akimalizia mpira wa kona uliookolewa vibaya na mabeki wa Prisons katika dakika 57.
Prisons walipoteza nafasi ya kufunga katika dakika ya 2, baada ya mshambuliaji wake Peter Michael kumlamba chenga kipa Abel Dhaira na kupiga shuti, lakini beki wa Simba, Joseph Owino aliokoa mpira huo kwa kichwa na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Kagera; Mabao ya Mrisho Ngassa na Hamisi Kiiza yalitosha kuipa Yanga ushindi muhimu na kuvunja mwiko wa kuitoifunga Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba katika miaka ya karibuni.
Mshambuliaji Ngassa ameendeleza kasi yake ya kuzifumania nyavu baada ya kuwatoka mabeki wa Kagera Sugar na kuifungia Yanga bao la kuongoza katika dakika ya 4.
Kagera walijibu mapigo na kufanikiwa kusawazisha bao hilo katika dakika ya 49, kupitia Godfey Wambura aliyemalizia vizuri pasi ya Paul Ngwai.
Uzembe wa mabeki wa Prisons katika dakika ya 60, ulitoa mwanya kwa Hamis Kiiza na kuipachikia Yanga bao la pili kwa shuti kali.
Chamazi, Tamba Sued aliibuka shujaa baada ya kufunga mabao mawili katika mchezo ulioshuhudia mwamuzi Antony Kayombo akitoa penalti mbili ndani ya dakika 20, wakati vibonde wa ligi hiyo Ashanti United wakiichapa Coastal Union kwa mabao 2-1 kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Kiungo, Jerry Santo aliifungia Coastal Union bao la kuongoza kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 3 baada ya Bwana Hamisi kuchezewa vibaya kwenye eneo la hatari.
Ashanti United kusawazisha bao hilo kwa penalti iliyopigwa na Sued katika dakika ya 23, baada ya Joseph Mahundi kufanyiwa faulo kwenye eneo la hatari.
Sued aliihakikishia Ashanti ushindi katika dakika 86, kwa shuti ambalo beki wa Coastal aliushika mpira kabla ya kuingia wavuni.

Kocha wa Union, Hemed Morocco alitolewa nje baada ya kufanya fujo kwa kupinga bao hilo.

Azam, Mbeya City vitani
Kivumbi cha Ligi Kuu Bara mzunguko wa tisa kinaendelea leo kwa timu nane kushuka dimbani kusaka pointi tatu muhimu.
Macho yatakuwa kwa Azam na Mbeya City zinazowania kujiweka katika nafasi nzuri za ligi hiyo.
Azam FC itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wake wa Chamazi wakati Mbeya City watakuwa wageni wa
Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Katika Uwanja wa Manungu mjini Morogoro, Mtibwa Sugar itakuwa ikicheza na Oljoro JKT ya Arusha, huku Ruvu Shooting ikimenyana na Rhino Rangers ya Tabora Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani.
Kocha wa Azam FC, Stewart Hall aliliambia gazeti hili kuwa kikosi chake kimejiandaa vya kutosha na mchezo na kusisitiza lengo lao kubwa ni kushinda na kuzidi kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.
Naye Kocha wa JKT Ruvu, Mbwana Makatta alisema:
“Mchezo uliopita tumepoteza dhidi ya Mtibwa, nafikiri ni wakati wetu kufuta makosa yalijitokeza mechi iliyopita, hatuwezi kukubali kirahisi tena kufungwa na Azam FC,”
Kwa upande wa Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Maxime alisema: “Siwezi kusema lolote kwa sasa, nafikiri dakika 90 ndizo zitakazotoa majibu, kwa ujumla tumejiandaa vizuri na hatuwezi kuibeza Oljoro.”
Next Post Previous Post
Bukobawadau