Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Mkuu
Mpya mmoja wa Mkoa na kuwahamisha vituo vya kazi wengine sita kuanzia
jana, Jumamosi, Desemba 6, 2014.
Taarifa iliyotolewa
leo, Jumapili, Desemba 7, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi
Ombeni Sefue mjini Dar es Salaam inasema kuwa Rais amemteua Mkuu wa
Wilaya ya Karatu, Mkoa wa Arusha, Ndugu Daudi Felix Ntibenda kuwa Mkuu
wa Mkoa wa Arusha.
Ndugu Ntibenda ataapishwa kesho, Jumatatu, Desemba 8, 2014, saa nne asubuhi, Ikulu, Dar Es Salaam.
Taarifa hiyo inasema
kuwa wakuu waliohamishwa vituo vya kazi ni Mheshimiwa Elaston Mbwilo
anayehamishwa kutoka Mkoa wa Manyara kwenda Mkoa wa Simiyu ambako
anachukua nafasi ya Mheshimiwa Paschal Mabiti aliyepewa likizo ya
ugonjwa, Mheshimiwa Joel Nkanga Bendera aliyehamishwa Mkoa wa Manyara
kutoka Mkoa wa Morogoro na Mheshimiwa Dkt. Rajabu M Rutengwe
anayehamishwa Mkoa wa Morogoro kutoka Mkoa wa Tanga.
Wengine ni Mheshimiwa
Magalula Saidi Magalula anayehamishiwa Mkoa wa Tanga kutoka Mkoa wa
Lindi, Mheshimiwa Mwantumu Bakari Mahiza anayehamishiwa Mkoa wa Lindi
kutoka Mkoa wa Pwani na Mheshimiwa Mhandisi Evarist B. Ndiliko
anayehamishiwa Mkoa wa Pwani kutoka Mkoa wa Arusha.
Wakuu wengine wa mikoa wanaendelea kubakia katika vituo vyao vya sasa vya kazi
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam
6 Desemba, 2014
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comment:
Post a Comment