Bukobawadau

IRENE UWOYA- MACHO MBELE NJE YA NCHI

Katika kile kinachoonekana waigizaji wa kike kutaka kukuza tasnia ya uigizaji kwa kuvuka mipaka ya nchi, mwigizaji Irene Uwoya amesema kuwa anataka atambulike nje ya nchi kuliko ndani.
Akiweka hoja yake sawa, mwanadada huyo anayedaiwa kuendelea kuwa na mvuto katika tasnia ya filamu alisema anajua kuwa siyo jambo rahisi kufanya vizuri nje ya nchi, lakini huko ndiko anakotaka kufika, hivyo inyeshe mvua au liwake jua, atajitahidi kuhakikisha kwamba ndoto zake zinatimia.
Uwoya alisema kuwa alijaribu kutengeneza mtandao wa kazi na wasanii wa nje wakati anatayarisha filamu ya ‘Kisoda’ ambayo picha zake zilipigwa nchini Afrika Kusini na Uturuki. Alifafanua kama wakati mwingine siyo lazima kusafiri, kuna wakati wasanii wa nje wanaweza kuja Tanzania kikazi, ujio wao ni nafasi ya pekee kwao, au kwa kufanya nao kazi hapahapa, ama kuchukua mawasiliano na kuwafuata baadaye kwa ajili ya kufanya nao kazi.
“Tena nawaambia wale wote wenye nafasi au wanaofahamiana na watu wanaopenda kwa dhati kufanya kazi na waigizaji wa Tanzania, wasikose kuwaambia hata mimi napenda na ninaweza kufanya hivyo, ”alisema Uwoya.
Mwigizaji huyo alifafanua kuwa njia pekee ya kutangaza kazi za ndani Kimataifa ni kufanya kazi na waigizaji wa nchi nyingine ambao watakuwa na hamu ya kukufuatilia na kufuatilia kazi zetu nyingine pia. Aliongeza kuwa kwenye muziki angalau kuna mwanga, lakini kwenye uigizaji bado juhudi inahitajika kwani baada ya kufariki dunia kwa mwigizaji Steven Kanumba, mbio za kujitangaza kama zimefifia.
Kauli hiyo ya Uwoya imekuja wakati waigizaji kadhaa wakionyesha nia kama yake akiwamo Wastara anayenadi filamu mpya ya ‘Mateso wanayopata Watanzania nje ya nchi’ na mwigizaji anayedaiwa kuwa na nguvu ya kukubalika kwenye jamii Wema Sepetu akiwa amerudi juzi kutoka nchini Ghana ambako alikwenda kupiga picha za filamu yake iitwayo ‘After Death’.
Next Post Previous Post
Bukobawadau