Bukobawadau

WAKULIMA WA KAMACHUMU WAJIKOMBOA NA MUCOGA

Mkuu wa wilaya Muleba katikati mwenye Kaunda suti na   viongozi wa MUCOGA
Mkuu wa wilaya Muleba, Francis Isack, akitoa hotuba ya  uzinduzi
Muhandiki akiongea kwenye ufunguzi wa MUCOGA
Wana MUCOGA Muhandiki wa tatu toka kushoto waliokaa


Na Prudence Karugendo
HATIMAYE  kilio cha siku nyingi cha wakulima wa zao la kahawa mkoani Kagera kimeelekea kufika mwisho baada ya baadhi ya wakulima kubuni njia zao wenyewe za kujikomboa kwenye lindi la manyanyaso na hujuma. Ubunifu huo wa kujikomboa toka kwenye makucha ya mfumo onevu wa kuwageuza watumwa, kwa maana ya kuwalazimisha kuzalisha wasichonufaika nacho, umeshangiliwa na wakulima wote wa kahawa mkoani Kagera.
Sanasana kilichofanya ubunifu huo ukashangiliwa kwa furaha sana na hata wakulima ambao hawajajiunga na ubunifu wenyewe ni mwanga mzuri uliojionyesha wa juhudi za wakulima hao, wazalishaji wa kahawa, walizokuwa wakizifanya kutaka kuyaona manufaa ya zao lao hilo kuu la kibiashara kwa miongo nendarudi bila kuyaona matunda yake ndani ya mfumo mkongwe unaotumika kwa sasa wa ushirika, ambao kusema ukweli ni kama umekwama na kushindwa kuwakwamua wakulima kiuchumi.
Wabunifu wa njia hiyo ya kujikomboa kiuchumi ni wakulima wa kahawa wa Kamachumu, wilayani Muleba, Kagera, wakiongozwa na Archard Felician Muhandiki, aliyekuwa mwakilishi wao katika chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd. lakini baadaye akafanyiwa mizengwe ya kifisadi na kuondolewa kwenye uwakilishi wake ili kuzima kelele zake za kutaka kuuwajibisha uongozi mbovu wa chama hicho cha ushirika.
Baada ya mizengwe hiyo iliyofanyika kwa nguvu kubwa zilizowezeshwa na kipato cha ushirika, ambacho lakini hakitumiki kuwawezesha wanaushirika wenyewe kiuchumi, ndipo Muhandiki, kwa kushirikiana na baadhi ya wakulima aliokuwa akiwawakilisha katika ushirika huo, walipoamua kubuni njia mbadala za kulishughulikia zao lao la kahawa nje ya mfumo wa ushirika.
Wakabuni Jumuiya ya Wazalishaji wa kahawa wa Muleba na kuipa jina la Muleba Coffee Growers Association (MUCOGA), na kisha kuitafutia usajili katika wizara ya Mambo ya Ndani chini ya kitengo cha Vyama vya Kijamii na baadaye kupata leseni ya kufanya biashara ya kahawa.
Wameamua kufanya hivyo ili kuondokana na urasimu wa ushirika unaoonekana unawalazimisha wakulima kuutumikia mfumo huo bila wao kupata chochote.
Baada ya taratibu zote kukamilika, uzinduzi rasmi wa MUCOGA ulifanyika tarehe 29 April, 2015, kwa baraka za mkuu wa wilaya ya Muleba, Francis Isack, ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika sherehe hiyo. Sherehe hiyo ya uzinduzi ilifunguliwa na mwenyekiti wa muda wa MUCOGA, Dauda Mahamud.
Katika nasaha zake za uzinduzi wa MUCOGA, mkuu huyo wa wilaya ya Muleba, Francis Isack, alikumbusha kwamba mikakati ya kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ilipata Baraka za mtangulizi wake wilayani humo, na yeye akapata bahati ya kuizindua. Akasema kwamba hilo ni lazima linamfurahisha mtangulizi wake kule aliko, kwahiyo akawaomba wana MUCOGA kuiendeleza jumuiya hiyo ili ishamiri kusudi hata yeye atakapokuwa amehamishiwa kwingine akiendelea kusikia mafanikio yake awe anajivunia kushamiri kwake, kwamba ni yeye aliyeizindua kama anavyofurahi mtangulizi wake aliyeuanzisha mchakato wa kuwepo kwake.
Alisema kuwepo kwa jumuiya inayojihusisha na kitu ambacho tayari kinashughulikiwa na chombo kingine ni jambo jema kwa vile kunaleta ushindani, akaongeza kwamba ushindani ndio unaochochea maendeleo ya eneo lolote. “Sababu huyu akisema niboreshe hivi na huyu anasema nizidishe ubora kwa njia hii, kinachopatika katika ushindani wa aina hiyo ni maendeleo ya sehemu zote mbili”, akasema Isack.
Akaongeza kwa kusema kwamba uwepo wa MUCOGA ni lazima utawapatia tija hata wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. kwa vile chama hicho kitajitahidi kuwanufaisha wanachama wake ili kiendelee kuwepo. Kwamba chombo kikibaki kimoja kinajisahau na kubweteka kutokana na kukosa changamoto na hivyo kuyafanya maendeleo kuyeyuka.
“Nawaomba muendeleze moyo huu wa kijumuia bila mifarakano ili kuyafikia malengo, yaani mafanikio mliyoyakusudia, yaliyo mfano wa kuigwa”,  alisema mkuu huyo wa wilaya ambaye anaonekana bado ni kijana, tena anayependelea kujichanganya sana na wananchi wa wilaya yake, ikizingatiwa kuwa ana muda mfupi tangu ahamishiwe kwenye wilaya hiyo ya Muleba.
Deocres Rutabana, katibu mkuu wa muda wa MUCOGA, alisema katika risala aliyoisoma mbele ya mgeni rasmi, kwamba MUCOGA ni kwa ajili ya wakulima wote wa kahawa wilayani Muleba wanaojisikia kujiunga na jumuiya hiyo. Pia akaongeza kwamba MUCOGA imefungua milango yake hata kwa wakulima wa kahawa wa nje ya mipaka ya wilaya ya Muleba ambao wanayaona manufaa ya muundo huo wa kulishughulikia zao la kahawa na kuwapa tija wazalishaji wake.
Vilevile walikuwepo waalikwa toka chama cha ushirika cha Magata, Muleba, kilichojitenga na chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd. ikiwa ni kuonyesha kwamba pamoja na MUCOGA kujiendesha nje ya utaratibu wa ushirika bado haina uhasama na ushirika.
Kiongozi wa msafara wa waalikwa hao toka Magata, Enock Babu, katika salaamu zake toka kwa wanaushirika wa Magata aliwashauri wana MUCOGA kuweka pembeni itikadi za kisiasa na kidini na kuangalia tu suala moja la kiuchumi. Akasema kwamba wana MUCOGA wahakikishe jumuiya yao inawafikisha kwenye malengo yao ambayo ni mafanikio ya kiuchumi bila kugawanywa na mambo ya itikadi za kisiasa wala imani za kidini.
Naye muasisi wa wazo la kuwa na jumuiya hiyo ya wazalishaji wa kahawa wa Muleba, Archard Felician Muhandiki, aliamua kuitumbuiza hadhara iliyokuwa kwenye uzinduzi huo kwa wimbo uliokuwa na maneno haya; “Ekyomwantumile nakileta, Kihanja Ihangiro milembe” wenye maana ya kwamba (mlichonituma nimekileta, Kihanja Ihangiro kote mambo salama. Kihanja ndiko liliko eneo la Kamachumu, au kwa ramani ya kisiasa likiitwa Muleba Kaskazini. Ihangiro,  kwa ramani ya kisiasa ndiko Mulena Kusini.
Katika kuonyesha jinsi walivyojipanga, wana MUCOGA wameanzisha salaamu yao mpya iliyo tofauti na ile ya wanaushirika wa KCU (1990) Ltd., inayosema (ushirika mwitikio wake ukiwa ni pamoja tujenge uchumi). Salaamu ya MUCOGA inasema (MUCOGA mwitikio wake ukiwa ni tujenge uchumi imara).
Baada ya uzinduzi huo uliofana sana watu wa maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kagera wakaanza kupiga simu kuulizia utaratibu wa kujiunga na jumuiya hiyo, kitu kinachoonyesha kuwa wamechoshwa na utaratibu unaotumika kulishughulikia zao lao la kahawa kwa sasa.
Kwa mujibu wa katiba ya jumuiya hiyo uongozi uliopo kwa sasa ni wa mpito kwa ajili ya maandalizi ya jumuiya hiyo mpya. Baadaye utaitishwa uchaguzi mkuu kwa ajili ya kuwapata viongozi wa kudumu kulingana na muda uliowekwa na katiba hiyo.
0784 989 512  
Next Post Previous Post
Bukobawadau