TAARIFA YA MKUU WA MKOA KUHUSU HATUA ZINAZOENDELEA KUCHUKULIWA NA SERIKALI KUKABILIANA NA JANGA LA TETEMEKO LA ARDHI KAGERA SEPTEMBA 17, 2016
Ndugu
Waandishi wa Habari, Kama
mnavyojua Mkoa wetu wa Kagera ulipatwa na janga la tetemeko la ardhi tarehe 10.09.2016,
kutokana na janga hilo Serikali kwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa
maendeleo pamoja na wananchi tulichukua hatua za haraka ili kukabiliana na
janga hilo, na leo nimewaiteni ili niwape taarifa tulizochukua mpaka sasa ili
kunusuru wahanga waliokumbwa na janga hilo katika mkoa wetu.
Ndugu
Waandishi wa Habari,
Mara baada ya tetemeko hilo kutokea, kwenye mkoa mzima wananchi waliojeruhiwa
ni 440 na kati ya majeruhi hao 253 walifika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, pia majeruhi
151 walilazwa ambapo majeruhi 113 tayari wametibiwa na kuruhusiwa. Katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wamebaki majeruhi 38 na kati ya hao majeruhi 23
walihitaji huduma za upasuaji na tayari wote wameishafanyiwa upasuaji huo na
wanaendelea vizuri.
Aidha, majeruhi 187 walifika katika
vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Kagera na walitibiwa
na kuruhusiwa na kufikia jumla ya majeruhi ambao walitibiwa na kuruhusiwa 412
kati ya 440. Vifo vilivyosababishwa na janga hilo ni 17 hadi kufikia siku ya
leo.
Ndugu
Waandishi wa Habari,
Tetemeko la ardhi mkoani Kagera hadi sasa limesababisha nyumba 2,063 kuanguka,
Nyumba zenye uharibifu hatarishi 14,081. Nyumba zenye uharibifu mdogo 9,471. Aidha, wananchi walioathirika na wanahitaji
misaada ili kurudi katika mfumo wa kawaida wa maisha yao ni 126,315
Ndugu
Waandishi wa Habari,
Kufuatia madhara hayo yaliyojitokeza mahitaji mablimbali ya kibinadamu ya muda
mfupi na muda mrefu yanahitajika. Mahitaji
hayo ni madawa na vifaa tiba, Chakula,
Vifaa vya Ujenzi kama simenti, misumari, mabati na mbao.
Hadi kufikia sasa Kamati ya maafa ya Mkoa
wa Kagera tayari imepokea msaada wa mahitaji mbalimbali ikiwa ni Madawa na
vifaa tiba, Chakula, (Matrubali, mahema mashuka na mablanketi), vifaa vya
ujenzi kama mbao, misumari, mabati na simenti vyenye gharama ya zaidi ya
shilingi milioni 431,715,800/=
Ndugu
Waandishi wa Habari, Kwa
upande wa dawa na vifaa tiba wadau mbalimbali pamoja na Serikali wameweza
kuchangia dawa na vifaa tiba vya kutosha hadi sasa hakuna upungufu wa dawa na
vifaa tiba katika hospitali zetu.
Aidha kwa mahitaji ya haraka tayari
Kamati ya mkoa imegawa chakula kwa wahanga katika mkoa mzima kama ifuatavyo:
unga wa sembe kilo 3750, mchele kilo 1850, sukari tani 6.5, maharage kilo 3470,
bisukuti katoni 2600, na maji ya kunywa katoni 615. Pia wahanga wamegawiwa mahitaji
muhimu kama mablanketi 480 mahema 119 na matrubali 320. Huo ulikuwa ugawaji wa
mahitaji wa awali na kamati zinaendelea kugawa mahitaji hayo katika maeneo
yaliyoathirika na yataendelea kugawiwa kadri tunavyopokea misaada ya mahitaji
hayo.
Ndugu
Waandishi wa Habari,
Napenda sasa kutoa taarifa ya michango mbalimbali ambayo tayari tumeipokea
kutoka kwa wadau mbalimbali; Katika Harambee tuliyoifanya jana tarehe
16/09/2016 tuliweza kukusanya kiasi cha fedha taslimu pamoja na hundi 7,800,000/=, ahadi ya fedha na vifaa ni
shilingi milioni 770,502,000/= kama
wadau hawa wote watatoa michango yao jumla tutakuwa tumepata shilingi milioni 778,302,000/=
Kupitia Akaunti yetu iliyoko Benki ya CRDB inayojulikana kama “KAMATI YA MAAFA KAGERA CRDB BUKOBA” Akaunti
Namba 0152225617300 tayari tumekusanya kiasi cha shilingi 623, 624,200/=. Aidha, baada ya Mhe,
Waziri Mkuu kuzindua namba za simu za kuchangia maafa Kagera tayari wananchi
wameanza kuchangia michango yao kupitia namba hizo ambazo ni (M.PESA 0768 196 669), (AIRTEL MONEY 0682
950 009), (TIGO PESA 0718 069 616).
Ndugu
Waandishi wa Habari,
Napenda kuwashukuru wananchi na wadau mbalimbali wote wanaoendelea kujitoa kwa
kuchangia maafa yaliyotupata katika Mkoa wetu wa Kagera pia natoa wito kwa kila
Mwananchi, Mdau, Taasisi mbalimbali ambao hawajachangia kuendelea kuchangia
kupitia akaunti ya benki na namba za simu zilizotajwa hapo juu kwani mahitaji
bado ni makubwa sana.
Ndugu
Waandishi wa Habari,
Kabla ya kuhitimisha naomba kueleza mkakati wa Kamati yangu tunaondelea nao
kuwa ni kugawa mahitaji mbalimbali kwa wahanga kadri tunavyoupokea. Pia wajumbe
wote wa Kamati wamegawanywa katika maeneo mbalimbali ya mkoa yaliyopatwa na
majanga ili kusimamia zoezi la kugawa mahitaji na kuhakikisha hakuna mwananchi
aliyeathirika na janga la tetemeko ameachwa bila kusaidiwa.
Ndugu
Waandishi wa Habari,
Mwisho napenda kuwashukuru Waandishi wote wa Habari pamoja na vyombo vyao vya
habari kwa kufanya kazi yao kwa ushirikiano mkubwa na Kamati yangu kwa
kuwafikishia habari wananchi habari muhimu kuhusu janga lililotupata mkoa wetu.
MWISHO