Bukobawadau

FNB YAZINDUA MASHINE ZA MALIPO KWA NJIA YA KAD

Meneja Masoko wa First National Bank Tanzania, Bi. Blandina Mwachang’a (Kushoto), na Mkuu wa kitengo cha bidhaa na huduma za kimtandao, Bw. Silvest Arumasi ( kulia) wakionyesha Mashine za malipo kwa njia ya kadi ambazo benki hiyo imezindua ili kuimarisha matumizi kadi za benki kama mbadala wa fedha taslimu Katikati ni Meneja wa Huduma za Kadi, Bi. Emma Kilimba akiwa ameshikilia tuzo ya ufanisi wa mashine hizo za malipo kwa mwaka 2016.
Na Cathbert Kajuna.
First National Bank Tanzania (FNB) imezindua rasmi mashine za malipo kwa njia ya kadi (POS Devices) jijini Dar es salaam kama hatua ya kuimarisha matumizi ya kadi za benki kwa ajili ya malipo ya bidhaa na huduma kwa njia salama, rahisi, na kwa gharama nafuu na zitatumika kama mbadala wa fedha taslimu.
Mkuu wa bidhaa na huduma za dijitali wa benki hiyo, Silvest Arumasi alisema benki itatoa mashine za kuweka maeneo mbalimbali ya biashara kubwa na biashara ndogo au za rejareja. Vilevile benki hiyo itatoa mashine ndogo za kubeba kama simu ambazo zitatumika kwenye sekta ya utalii na mahoteli pamoja na biashara nyingine hasa zile zinazohama hama kwani mashine hizo zinatumia mtandao wa Intaneti kama simu.
“Biashara yoyote inaweza kutumia mashine za malipo kwa njia kadi (P0S Device) kupokea malipo ya bidhaa au huduma. Huduma hii inatarajiwa kuongeza tija kwenye maeneo ya biashara kwa kupunguza hatari zitokanazo na utunzaji fedha taslimu na pia itapunguza safari za wafanyabiashara kwenda katika matawi ya benki kuweka fedha na sasa wataweza kutumia muda mwingi zaidi kuendesha biashara. Mashine za malipo kwa njia ya kadi zinaweza kuwekwa sehemu ya kudumu karibu na wateja au kubebeka kulingana na mahitaji ya mteja” alisema.
Alisema kuanzishwa kwa huduma hiyo kutaboresha huduma za kidijitali za benki hiyo kwani sasa wateja wataweza kuangalia na kupakua taarifa za mihamala na fedha kila siku na za kila mwezi jambo ambalo litawasaidia wafanyabiashara katika kutunza mahesabu.
Uzinduzi wa mashine hizo ni sehemu ya mkakati wa FNB kuwa kiongozi katika huduma za benki na sehemu ya mpango wa benki hiyo kuchangia ukuaji wa uchumi kwa kuwawekea wafanyabiashara mazingira mazuri ya kuendesha shughuli zao.
Arumasi alisema kuwa sambamba na uzinduzi huo, benki hiyo imepokea tuzo ya ufanisi wa kadi za fedha na malipo za VISA kwa mwaka 2016 baada ya kuwa imekidhi viwango vya ubora kimataifa na kuwa benki bora nchini katika utoaji wa huduma kupitia kadi hizo. Hii ni kutokana na huduma bora kwa wateja, ufanisi, na mfumo wa kuaminika katika kuendesha shughuli za kibenki.
Programu ya tuzo za viwango vya ubora za VISA kimataifa ilianzishwa mwaka 1992 ili kutambua taasisi za kifedha dunia nzima zinazotoa huduma bora kwa watumiaji wa kadi za VISA kwenye maeneo mbalimbali. Kila mwaka tuzo hizo utolewa kwa taasisi hizo kutokana na kukidhi viwango vya ubora katika utendaji, ufanisi na mifumo madhubuti ya kudhibiti udanganyifu.
Next Post Previous Post
Bukobawadau