Bukobawadau

KAMISHNA GENERALI WA MAGEREZA NCHINI AMPONGEZA RC GAGUTI KUDUMISHA ULINZI NA USALAMA WA KAGERA PIA AGUSWA NA USHIRIKIANO NA JESHI LA MAGEREZA

Kamishna Generali wa Magereza nchini Tanzania Phaustine Kasike afurahishwa na ushirikiano wa Serikali ya Mkoa wa Kagera chini ya Mkuu wa Mkoa Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti na Jeshi la Magereza mkoani humo namna wanavyoshirikiana kutatua changamoto mbalimbali za Jeshi hilo katika kuweka mazingira bora ya utendaji kazi.

Akiwa ofisini kwa Mkuu wa Mkoa Kamishna Generali Kasike Julai 10, 2019 alipofika kumsalimia Mkuu wa Mkoa Gaguti alimpongeza yeye binafsi pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kwa kudumisha ulinzi na usalama hasa kwa kipindi hiki ambacho sasa mkoa wa Kagera umetulia kwa matukio mbalimbali makubwa ya utekaji barabarani
Kamishna Generali Kasike alisema kuwa yupo Mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi hasa kufuatilia maelekezo mahususi yaliyotolewa na kwa Jeshi hilo ya kuhakikisha Jeshi la Magereza linazalisha chakula cha kutosha kuwalisha wafungwa lakini pia ikiwezekana kuzalisha ziada ya chakula kwani nguvu kazi ya kuzalisha chakula hicho ipo ambao ni wafungwa katika Magereza.
“Sisi Jeshi la Magereza Tumeweka mkakati maalumu wa kuzalisha chakula cha kutosha kulisha Magereza yote nchini na katika mkakati huo tulibainisha Magereza kumi nchi nzima ambapo na Gereza la Kitengure la hapa mkoani Kagera lipo kati ya hayo kumi kwani Gereza hilo linazalisha chakula kwa misimu miwili ya vuli na masika.” Alifafanua Jenerali Kasike.
 Pia Kamishna Jenerali Kasike alisema katika kuboresha makazi ya Maafisa wa Jeshi la Magereza wanao mpango mkakati wa Kila Gereza kuzalisha tofali hasa zile za kuchoma ili kujenga makazi mapya ya Maafisa na kukarabati miundombinu ambayo tayari imechoka.
Kwaniaba ya wananchi wa Mkoa wa Kagera Mkuu wa Mkoa Gaguti alimshukuru Kamishna Generali Kasike kwa kuamua kufanya ziara Mkoani Kagera kuja kuona changamoto mbalimbali hasa kwa upande wa chakula cha wafungwa na makazi ya Maafisa wa Jeshi hilo la Magereza.
Mkuu wa Mkoa Gaguti alimhakikishia Jenerali Kasike kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha hasa katika ujenzi wa makazi bora ya Maafisa wa Magereza ili kuboresha zaidi utendaji kazi wa Maafisa hao katika kutekeleza majukumu yao.
Aidha, uongozi wa mkoa utaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Jeshi la Magereza Mkoani Kagera Kagera katika kuzalisha chakula cha kujitosheleza kwa Wafungwa lakini pia kuzalisha chakula cha ziada kwa Magereza ya nje ya Mkoa kwa kuwa Mkoa wa Kagera unayo fursa nzuri ya kilimo na kupelekea uzalishaji wa chakula kuwezekana kwa mimisimu miwili taofauti.
Mwisho Kamishna Jenerali Kasike alisema kuwa ziara yake ni ya mafanikio makubwa mkoani Kagera kwa jinsi alivyopokelewa na uongozi wa mkoa pia alivyohakikishiwa ushirikiano na Mkuu wa Mkoa Gaguti katika kutatua changamoto mbalimbali za Jeshi la Magereza.

Na: Sylvester Raphael 
Next Post Previous Post
Bukobawadau