Bukobawadau

MAWAKALA WA KAMPUNI BINAFSI WANAOWAPOTOSHA WAKULIMA VIJIJINI KUHUSU MFUMO SERIKALI WA UKUSANYAJI WA KAHAWA WAKAMATWE MARA MOJA – RC KAGERA

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti aagiza kukamatwa mara moja kwa Mawakala wawili wa Kampuni binafsi wanaopita vijijini katika Wilaya za Karagwe na Kyerwa kuwaposha na kuwalaghai wakulima wa kahawa wasikubaliane na mfumo wa Serikali wa kukusanya kahawa katika vyama vya msingi na kuiuza kwa mfumo wa ushirika ulionzishwa na Serikali.
Mkuu wa Mkoa Gaguti alitoa maelekezo hayo Julai 21, 2019 katika mkutano wa viongozi wa Vyama vya Msingi, Watendaji wa Kata na Viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha KDCU Limited Wilayani Karagwe mara baada ya kukagua viwanda vitatu vya kukoboa kahawa vya Karim Amri, ASU Company Limited na KDCU Limited kuona namna vinavyoendelea kuchakata kahawa.
“Nimeona nije kujionea msimu unaendeleaje na kama kuna changamoto yoyote tuitatue kwa pamoja na si kusubiri msimu umeisha. Pia ninazo taarifa kuwa kuna mawakala wawili wa Kampuni binafsi wamekuwa wakipita vijijini kupotosha wakulima wasifuate mfumo wa Serikali ili baadae waje wanunue kahawa yao kwa bei ndogo tu namuagiza Kamanda Polisi Mkoa Mawakala hao wakamatwe mara moja.” Aliagiza Mkuu wa Mkoa Gaguti
Pia MMhe. Gaguti alisema kuwa maelekezo ya Serikali yapo wazi kuwa kama kuna mfanyabiashara yeyote anataka kununua kahawa awasiliane na ofisi yake lakini awe na bei inayomnufaisha mkulima. “Tayari tumepokea maombi kadhaa ya kununua kahawa kutoka kwa wanunuzi binafsi lakini maombi yote hayamnufaishi mkulima bei yao ipo chini sana hatuwezi kumruhusu mkulima anyonywe. Alisitiza Mkuu wa Mkoa Gaguti
Kuhusu bei kwamba wakulima wanapunjwa Mkuu wa Mkoa Gaguti aliitolea ufafanuzi kuwa mpaka mkulima analipwa malipo ya kwanza tayari Vyama Vikuu vya Ushirika vinakuwa vimeondoa gharama za uchakataji kiasi cha shilingi 600 na kupelekea kilo moja kufika hadi 1700/= lakini bado bei katika soko la dunia ikitangazwa mkulima anaongezewa fedha nyingine wakati makato yote ya Serikali na gharama za uchakataji zinakuwa zimelipwa tayari.
Aidha, Mzee Thomas Kasimbazi mkulima kutoka Chama cha Msingi Nyabwegira Kata Ndama aliiomba Serikali inapokuwa na mipango mizuri iwashirikihe wananchi ili waweze kuelewa hasa suala la mkulima kulipiwa benki ambapo mzee Kasimbazi alisema kuwa wazee wengi hawajui na hawaelewi kwanini wanalipiwa Benki baada ya kukusanya kahawa yao katika Vyama vya Msingi ambapo wakipata elimu wapo tayari kutoa ushirikianao kwani Serikali inalenga kulinda fedha zao ziwafikie walengwa moja kwa moja.
Akifafanua Mkuu wa MkoaGaguti alisema kuwa tayari elimu inaendelea kutolewa chini ya uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ikishirikiana na mitandao ya simu, TCRA, na Benki zinazohusika katika malipo wanapita kwa wakulima na kuwaelimisha faida za kulipiwa benki pia Mkuu wa Mkoa Gaguti aliagiza Wakuu wa Wilaya kubaini maeneo yenye changamoto ya mitandao na wakulima wenye fedha chini ya Tshs 100,000/= kupelekewa fedha zao taslimu bila kuzipitisha benki.
Vyama Vikuu vya Ushirika Mkoani Kagera vya KCU 1990 LTD na KDCU LTD tayari vimekusanya kahawa kilo milioni 8.5 sawa na asilimia 20% ya malengo ya ukusanyaji katika msimu huu wa mwaka 2019/20 na jumla ya shilingi bilioni 6.2 tayari zimelipwa kwa wakulima aidha, KDCU LTD tayari kimekusanya kahawa ya maganda kilo milioni 5.8 na shilingi bilioni 5.3 zimelipwa kwa wakulima sawa na asilimia 15% ya matarajio ya makusanyo.
Mnada wa kahawa katika msimu huu wa 2019/20 unatarajiwa kufanyika ndani ya wiki mbili kutoka sasa katika Manispaa ya Bukoba badala ya Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo baada ya mnada huo bei kamili ya kahawa itatangazwa rasmi ili mkulima ajue kwa kila kilo atauza kwa shilingi ngapi na kupatiwa malipo ya pili baada ya kulipwa shilingi 1100/= malipo ya awali.
Akimalizia mkutano wake Wilayani Karagwe na viongozi mbalimbali wa vyama vya Msingi Mkuu wa Mkoa Gaguti aliwaeleza vingozi hao kuwa dhamira ya Serikali ni kulinda maslahi ya wakulima wa kahawa na si vinginevyo pia kuwahimiza wakulima kukubali mfumo wakulipiwa benki kwa usalama wa fedha zao na wao wenyewe ikiwa ni pamoja na kudhibiti ubadhirifu wa baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi kutumia fedha za wakulima kwa matumizi yasiyokubalika.
Katika msimu huu wa mwaka 2019/20 Vyama Vikuu vyote vya Ushirika Mkoani Kagera vimekisia na vinatarajia kukusanya kahawa kilo milioni 52 ambapo msimu uliopita wa mwaka jana 2018/19 vyama hivyo vilikusanya kahawa kilo milioni 58.9
Next Post Previous Post
Bukobawadau