Bukobawadau

WATENDAJI WA KATA NA VIJIJI MNAYO MAMLAKA MAKUBWA MNAVAA KOFIA ZOTE ZA ULINZI NA USALAMA KATIKA MAENEO YENU

Na: Sylvester Raphael
Watendaji wa Kata na Vijiji mnavaa kofia zote za vyombo vya Ulinzi na Usalama wa nchi, nyinyi watendaji ni Askari Polisi, Uhamiaji, Usalama wa Taifa na ni askari Jeshi wa ulinzi wetu katika maeneo yenu ya kazi, simamieni majukumu yenu kwa nguvu zote bila kupepesa macho hakuna wa kuwababaisha.
Maneno hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti Septemba 16, 2019 wakati akizungumza na Watendaji wa Kata na Vijiji katika Halamashauri ya Wilaya ya Missenyi alipokuwa akiwakumbusha wajibu wao wa utendaji wa kazi katika maeneo yao.
Mkuu wa Mkoa Mhe. Gaguti aliwakumbusha watendaji hao kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali ya ugatuzi wa madaraka kuwa wanao wajibu wa kuhakikisha suala la ulinzi na usalama linamarishwa na mtu wa kwanza kuwajibika ni Mtendaji wa Kijiji akifuatiwa na Mtendaji wa Kata kuzuia uhamiaji haramu na vitendo vya uvunjifu wa amani.
“Mimi kama Mkuu wa Mkoa sitegemei kupokea kero yoyote katika ofisi yangu ambayo Mtendaji hajashughulika nayo, ninyi mnatakiwa kuhusika na kila jambo la mwananchi hakuna jambo lolote ambalo Mtendaji anatakiwa asilijue katika kijiji chake au Kata yake hata kama ni jambo la kifamilia.” Alisisitiza Mkuu wa Mkoa Gaguti
Pia Mhe. Gaguti aliwakumbusha Watendaji hao kusimamia miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kujihusisha na kero za wananchi akitolea mfano wa Vyama vya Msingi katika maeneo yao kuwa wakulima wakati wakihangaika kulipwa fedha zao Watendaji wanakaa pembeni kama jambo hilo haliwahusu kumbe wao wanatakiwa kufanya ufuatiliaji kuhakikisha kila mkulima amelipwa au apewe majibu sahihi kwanini hajalipwa.
Mwisho Mkuu wa Mkoa Gaguti aliwakumbusha Watendaji hao kutoa utumishi uliotukuka kwa wananchi, kuwapokea, kuwasikiliza na kutatua kero zao tena kwa kuwapa maandishi si maneno tu. Pia aliwakumbusha kuwa wasiwe miungu watu bali wawe watu wa chini kabisa na kutoa huduma iliyotukuka kwa wananchi ili kusukuma gurudumu la maendeleo mbele vile vile Watendaji hao wawe mstari wa mbele katika kukusanya kodi ya Serikali
Katika hatua nyingine Watendaji hao wa Kata na Vijiji walimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa changamoto kubwa kwao ni migogoro ya ardhi kwa maeneo wanayoyaongoza ambapo aliwaelekeza wakae na wahusika na kuimaliza migogoro hiyo na kuwashauri wananchi wanaomiliki ardhi hizo kuzipima ili kuondoa migogoro ya kesho.
Next Post Previous Post
Bukobawadau