Bukobawadau

#BUKOBA RC GAGUTI AWATAKA MAWAKILI WA KUJITEGEMEA KUWA WAKWELI KWA WATEJA WAO NA WANANCHI KAGERA WAYAAMINI MAAMUZI YA MAHAKAMA

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti azindua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini Mkoani Kagera kwa kupokea maandamano ya wadau mbalimbali wa Sheria wakiongozwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba Mhe. Lucia Gamuya Kairo.
Katika hotuba yake ya uzinduzi Mkuu wa Mkoa Gaguti alitoa kilio chake kwa Mawakili hasa wale wa kujitegemea kuwa wakweli na kumtanguliza Mungu katika kutekeleza majukumu yao ya huduma kwa wananchi katika masuala ya kisheria.
 “Kwa moyo wa dhati kabisa niwaombe Mawakili hasa wa kujitegemea muwe wakweli kwa wateja wenu, mwananchi anapokuja kwako na hoja yake msikilize kwa umakini ukiona hoja yake haina mashiko mbele ya sheria mwambie ukweli kuwa hata akienda Mahakamani hawezi kushinda kesi hiyo kuliko kumdanganya na kupoteza muda na fedha zake Mahakamani. “ Alisisitiza Mkuu wa Mkoa Gaguti.
Pia Mkuu wa Mkoa gaguti aliwataka Mawakili hao kumtanguliza Mungu katika kazi zao ili wanapokuwa wanatoa msaada wa kisheria kwa wananchi wasiongozwe na tama za kibinadamu ili wateja wanaowatetea washinde mashauri yao kwa haki bila dhuruma au kupindisha haki.
Kwa upande wa wananchi Mkuu wa Mkoa Gaguti alitoa rai kwao hasa katika Mkoa wa Kagera kuwa nao wanapaswa kuridhika na maamuzi ya Makama pale yanapotolewa. “Unakuta kesi ilishaamuliwa mpaka Mahakama ya Rufani lakini mwananchi haridhiki akiona huko hakushinda anakuja kwa Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya kushinikiza kufuta hukumu jambo ambalo si sawa.” Alisema Mhe. Gaguti.
Katika hatua nyingine Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba Mhe. Lucia Gamuya Kairo alisema kuwa katika Maadhimisho ya Wiki ya Sheria Mahakama itatembelea maeneo mbalimbali mkoani Kagera kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi na maeneo hayo ni Magereza, Shule mbalimbali za Sekondari, na maeneo ya wazi kama soko kuu na kituo kikuu cha Mabasi Bukoba.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti azindua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini Mkoani Kageraleo tarehe 1 Januari,2020 katika viwanja vya mahakama kuu Mjini Bukoba.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa Gaguti alivitaka Vyombo vya Habari Mkoani Kagera hasa Redio za Kijamii kuitumia Wiki ya Sheria nchini iliyozinduliwa rasmi Mkoani Kagera Februari 1, 2020 kurusha vipindi mubshara kutoka katika maeneo mbalimbali wadau wa Sheria watakakokuwa wanatoa misaada ya kisheria ili kutoa elimu kwa wananchi walioko manyumbani.
Mwisho Mkuu wa Mkoa Gaguti akizungumzia Kaulimbiu ya Mwaka huu 2020 isemayo “Uwekezaji na Biashara: Wajibu wa Mahakama na Wadau kuweka Mazingira Wezeshi ya Uwekezaji.” Aliwasisitiza wadau wote wa uwekezaji wanaopenda kuja kuwekeza katika mkoa wa Kagera kuhakikisha wanafuata na kukamilisha taratibu zote za kisheria ili kuepuka migogoro isiyokuwa ya lazima hapo mbeleni.
 Maadhimisho ya Wiki ya Sheria imezinduliwa leo Februari 1, 2020 na kilele chake kitakuwa tarehe 6/02/2020. Ikumbukwe kuwa mkoa wa Kagera unahitaji watendaji wa kutosha katika masuala ya kisheria kutokana na wingi wa watu. Kagera ni mkoa wa tatu kwa wingi wa watu ukiacha mikoa ya Dar es Saalam na Mwanza kwa takwimu za mwaka 2019 ambazo zimetolewa hivi karibuni Kagera kuna jumla ya watu 3,127,908 ukilinganisha na takwimu za mwaka 2012 watu 2,458,023.
   NINI MAADHIMISHO YA WIKI YA SHERIA NCHINI
Maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini ni kiashiria cha kuanza rasmi kwa shughli za kimahakams baada ya likizo ya Mahakama ambayo huanza kila tarehe 15 Desemba ya kila mwaka.Kwa mwaka huu wa 2020 maadhimisho haya ya wiki ya sheria nchini yameanza rasmi jana tarehe 31 Januari.2020 na kilele chake kitakuwa tarehe 6 Februari,2020 yakiwa na kauli mbi isemayo ''UWEKEZAJI NA BIASHARA ; WAJIBU WA MAHAKAMA NA WADAU KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI YA UWEKEZAJI
Kauli mbiu ambayo ndiyo dira ya Mwaka mzima kwa mahakama  katika kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kutoa haki kama ilivyoainishwa katika ibara ya 107A ya katiba ya Jamhuriu ya Muungano wa Tanzania
 Kama ilivyo kawaida katika maazimisho haya ya wiki ya sheria nchini Mahakama kwa kushirikiana na wadau wa s sekta ya sheria ikiwemo Polisi,Ofisi ya Mkuu wa Mashtaka ya Taifa,Mawakili wa kujitegemea Magereza ,Uhamiaji TAKUKURU,Ustawi wa Jamii,Baraza la Ardhi na Nyumba,Tume ya Usuluhishi na Uamuzi wa migogoro ya kazi na Taasisi zitoazo huduma ya msaada wa kisheria ikiwemo MUHOLA watashiriki katika zoezi la utoaji wa elimu ya kisheria katika mambo muhimu ikiwemo taratibu za ufugaji wa mashauri,ada za ufunguaji wa mashauri ya madai,sheria na taratibu zinazotumika katika uendeshaji wa mashauri ya jinai na madai,
 Taratibu za mashauri ya mirathi,taratibu za uendeshaji wa mashauri ya madai na jinai,namna ya kuwasilisha lalamiko,maoni au mapendekezo ya namna ya kuborsha huduma za kikimahakama na sekta nzima ya sheria na elimu ya mfumo wa TEHAMA KATIKA Ufunguaji na uendeshaji wa mashauri katika mahakama kuu na mahakama za hakimi mkazi wa wilaya.
 Maeneo ambayo huduma hiyo ya uelimishaji itatolewa ni pamoja na viwanja vya mahakama kuu Bukoba kuanzia tarehe 31 Januari mpaka tarehe 5 Februari,kuanzia saa 3:00 asubuhi mpaka saa 11:00 jioni,Mafunzo kwa mawakili wa kujitegemea ya namna ya kusajili mashauri ya madai kupitia mfumo wa TEHAMA ukumbi wa Mikutano wa mahakama kuu kuanzia saa 5:40 mpaka 6:40,Gereza kuu Bukona kuanzia saa 6:00 mchana mpaka saa 8:30 mchana,Stendi kuu ya mabasi Bukoba saa 6:00 mchana mpaka saa 8:00 mchana na Katoma Sekondari kuanzia saa 8:00 mchana mpaka saa 9:00alasiri
 Muendelezo wa matukio ya picha maadhimisho ya wiki ya sheria.
Muendelezo wa matukio ya picha kutoka viwanja vya Mahakama kuu Bukoba.
 Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba Mhe. Lucia Gamuya Kairo pichani
Uwanja wa Uhuru Mjini Bukoba, mwanzo wa maandamano ya Maadhimisho ya Wiki ya sheria nchini yaliyoongozwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba Mhe. Lucia Gamuya Kairo pichani katikati.
 Maandamano yakiendelea katikati ya Mji wa Bukoba
 Maandamano ya kielekea barabara ya Jamhuri Manispaa Bukoba
Mahakama kwa Ujumla wanatoa wito kwa Wananchi wote wa Manispaa ya Bukoba na katika maadhimisho yatakayofanyika katika ngazi ya wilaya katika Wilaya ya Biharamulo ,Muleba, Karagwe na Ngara kufika maeneo huduma za elimu ya kisheria zitakapokuwa zinatolewa na endapo wanamalalamiko   yoyote,maoni au mapendekezo ya uboreshaji wa huduma za Mahakama kutumia muda huu wa wiki ya sheria nchini
Next Post Previous Post
Bukobawadau