Bukobawadau

RUGAMBWA GIRLS FOUNDATION WAKABIDHI VIFAA VYA KUJIKINGA NA CORONAMkuu wa Mkoa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti amepokea msaada waVifaa vya kujikinga na Corona vyenye thamani ya TZS 2,000,000 kutoka kwa taasisi ya Rugambwa Girls Foundation vitakavyo saidia kukabiliana na Maambukizi ya Covid-19 kwa wanafunzi na walimu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Rugambwa iliyopo Bukoba Mjini.Ikiwa ni sehemu ya Kuunga Mkono Jitihada za Serikali na Maelekezo ya Wataalam wa Afya kwa kunawa Mikono ili kuzuia Maambukizi ya Corona kwa wanafunzi waliorejea Vyuoni na Mashuleni.

Mwakilishi wa Rugambwa Girls Foundation Bi Beatrice Van Arkadie akikabidhi msaada wa vifaa vya kujikinga na Ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya Corona ikiwa ni sehemu ya Kuunga Mkono Jitihada za Serikali na Maelekezo ya Wataalam wa Afya kwa kunawa Mikono ili kuzuia Maambukizi ya Corona kwa wanafunzi waliorejea shuleni hapo.

Muonekano wa vifaa vilivyotolewa na Rugambwa Girils Foundation vilivyokabidhiwa kwa Uongozi wa Shule ya Sekondari Rugambwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mkuu wa Mkoa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti

Bi Beatrice Van Arkadie Mwakilishi wa Rugambwa Girls Foundation (RGF) inayoundwa na wahitimu wa Rugambwa Sekondari yenye jumla ya wanachama 40 akisoma Risala mbele ya Mgeni Rasmi.

RISALA FUPI YA KUKABIDHI VIFAA VYA KUJIKINGA NA UGONJWA WA COVID 19 UNAOSABABISHWA NA VIRUSI VYA CORONA , ILIYOTOLEWA NA RUGAMBWA GIRLS FOUNDATION (RGF), TAREHE 3. JUNI. 2020. KATIKA SHULE YA SEKONDARI YA RUGAMBWA, BUKOBA

Ndugu Mgeni Rasmi –Mkuu wa Mkoa Mkoa

 Afisa Elimu- Mkoa ,Mkurugenzi Mtendaji-Bukoba Manispaa,
Mkuu wa shule- Rugambwa, Wanachama wa RGF,   Wana jumuiya ya Rugambwa,

Wageni waalikwa, Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana, Itifaki imezingatiwa.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Kwanza kabisa Sisi wana RGF tunamshukuru Mungu aliyetufikisha siku hii ya leo. Kwetu sisi wana RGF, hii ni hatua kubwa katika kufikia malengo ya Umoja huu. Pili, Tunatoa shukurani za pekee kwa Mgeni rasmi kwa kukubali kuwa nasi katika makabidhiano haya ya vifaa vya kupambana na ugonjwa wa COVID-19, na nyote mlio hudhuria tunasema asanteni sana.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Rugambwa Girls Foundation (RGF) imesajiliwa Novemba 2015, kwa namba ya usajili na 5216 kwa sheria Cap 318 R.E 2002. RGF inaundwa na wahitimu wa Rugambwa Sekondari., hadi sasa Foundation hii ina wanachama 40 walioko katika mikoa mbalimbali ya Tanzania. Jumuiya yetu haizalishi faida (Non-Profit Organization). Lengo kuu la RGF ni kusaidia mtoto wa kike kujitambua na kupambana na changamoto mbalimbali za elimu. Pamoja na hayo, RGF pia inajihusisha na sekta ya Afya, Mazingira na Ujasiliamali. Pamoja na kusaidia jamii kwa kutumia fedha tunazojichangisha, pia tunasaidiana wenyewe kwa wenyewe katika ugonjwa, sherehe, misiba na majanga mbalimbali, kwa kutumia miongozo tuliyojiwekea. RGF Tuna malengo ya muda mrefu na muda mfupi, ikiwamo kuanzisha Benki, kujenga mabweni, na kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum shuleni Rugambwa, na kuwapa huduma.

Ndugu Mgeni Rasmi,
Miaka ya nyuma kwa kushirikiana na ofisi yako tuliweza kufanya kampeni ya kuhamasisha wanafunzi wa Rugambwa juu ya kujitambua. Mikutano miwili ilifanyika shuleni Rugambwa na vilevile tumeweza kuwasaidia wanafunzi wasiojiweza na wenye ulemavu mbalimbali. Wenye uoni na usikivu hafifu na wenye ulemavu wa ngozi kwa kuwapatia bima za afya na mahitaji kama vile madaftari, kalamu, taulo za kike na mafuta ya ngozi kazi ambayo inaendelea. Vilevile, tulifanya harambee kuchangisha fedha za kuweza kuinua miundo mbinu ya Rugambwa Sekondari ambapo kwa kushirikiana na TEA na wadau mbalimbali tuliandaa andiko lililofanikisha TEA kuipatia shule ya Wasichana Rugambwa jumla ya Shilingi milioni 129 ambazo zimetumika kukarabati miundo mbinu hapa shuleni na kuboresha miundo mbinu ya walemavu.. Msukumo huu pia ulitoka shuleni ambapo walituomba tuweze kusaidia pale tunapoweza. Tunaamini juhudi hizi zimepelekea matokeo ya Rugambwa kuwa mazuri. Kwa rejea Picha za matukio hayo zinapatikana katika Tovuti ya taasisi ya RGF (www.rugambwafoundation.blogspot.com)

Ndugu Mgeni Rasmi,
Leo hii tuko hapa Kuunga juhudi za Mhe. Rais wetu aliyeruhusu shule kufunguliwa kwa kidato cha sita. Tuko hapa pia kuungana na wazazi, walimu, walezi na wanajumuiya wa Rugambwa na wanafunzi wa kidato cha sita kuunga juhudi za elimu kwa mtoto wa Kike. Kwa wadogo zetu wa Kidato cha Sita, tuna waunga mkono na kuwatakia kila la kheri katika mitihani yao. Katika hili RGF imetoa vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa Covid 19 vyenye thamani ya TZS 2,000,000. Tunaomba vifaa hivi viwekwe kwenye milango ya mabweni, Madarasani, assembly , ofisi za walimu na mahali ambapo uongozi wa shule utaona inafaa. Tunasaidia kuinua Elimu ya Rugambwa kama tulivyoinuka sisi.

Baada ya kusema hayo tunakushukuru sana tunaomba kukabidhi vifaa vya kupambana na ugonjwa wa Covid 19
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Wanafunzi wa Rugambwa Sekondari wakipiga makofi kufurahia jambo wakati mara baada ya Risala kukabidhiwa kwa Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti

Neno na Shukrani kwa Rugambwa Girls Foundation kutoka kwa Mkuu wa Mkoa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti

Muendelezo wa Matukio ya Picha follow Insta @Bukobawadau
P.O. Box 75209, Dar es Salaam, Tanzania.
Email: rugambwagirls@gmail.com
www.rugambwafoundation.blogspot.com
Next Post Previous Post
Bukobawadau