DKT JINGU AZINDUA KAMATI YA MAKAO YA TAIFA YA WATOTO KIKOMBO.
Serikali
inaendelea kuweka mazingira mazuri na rafiki kwa ajili ya ustawi wa
watoto nchini kupitia utekelezaji na uimarishaji wa afua mbalimbali
hususan watoto waliotokea katika mazingira magumu.
Na WMJJWM-Dodoma.
Hayo
yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu katika uzinduzi wa Kamati ya
makao ya Taifa ya Watoto Kikombo Septemba 04, 2025 Katika ukumbi wa
Wizara jijini Dodoma.
Dkt.
Jingu ameeleza kwamba uwepo wa Kamati hiyo ni moja ya uimarishaji wa
afua ya kuboresha ustawi wa watoto hasa waliotokea katika mazingira
magumu ili kuhakikisha wanapata malezi na makuzi stahiki kama yale
yanayopatikana watoto waliopo kwenye familia ili waweze kufikia
utimilifu wao kupata taifa bora.
“Sote
tunafahamu kuwa sehemu sahihi na muhimu ya kumlelea mtoto ni kwenye
familia lakini sababu ya changamoto mbalimbali baadhi ya watoto hujikuta
kulelewa kwenye familia imeshindikana na hapo ndipo nguvu ya taifa
inaingia ili kuhakikisha watoto hao wanapatiwa malezi yanayotakiwa
ikiwemo kuwaanda kukabiliana na changamoto mbalimbali za dunia ili
wanapofikia umri wa kujitegemea waweze kumudu kuendesha maisha yao”
amesema Dkt. Jingu.
Aidha
Dkt Jingu ametoa rai kwa Kamati hiyo kuhakikisha inaongeza thamani
katika makao hayo kwa kuja na mikakati mizuri zaidi ya kuwalea watoto
hao na kuwafikisha katika utimilifu wao.
“Inabidi
mje na ushauri na mawazo yatakayo weza tusaidia kwenda mbele na
kuboresha makao hayo hata yaweze kuwa ya mfano kwa makao mengine ya
kulelea watoto nchini kwani Wizara ipo tayari kuwapa ushirikiano wa
kutosha utakao wawezesha kufanya kazi yenu vizuri.”amesema Dkt Jingu.
Naye
Mwanakamati Josephine Mwaipopo ambaye ni Afisa Ustawi wa Mkoa wa
Dodoma amesema kwamba makao hayo yamekua mfano mzuri na wa kuigwa kwa
makao ya kulelea watoto nchini kwani yana vigezo sahihi vya marejeo hata
kwa wamiliki wa vituo na makao binafsi hivyo ni jukumu la Kamati
kuhakiksha makao hayo yanazidi kuwa bora.
Kwa
Upande wake mwanakamati kutoka Abbot Fund Alfred Magala amesema wadau
hao wako tayari kutoa ushirikiano unaohitajika ili kuweza kusukuma
ustawi wa watoto na jamii kwa ujumla .
Kamati
hiyo yenye wajumbe 12 ikiongozwa na Deodatus Orotha ambae ni Mkuu wa
chuo cha Veta inatarajia kufanya kazi kwa muda wa miaka mitatu.
MWISHO.






